Menu
in , , ,

Maswali matano uhamisho wa ‘Tshabalala’ Yanga

Tanzania Sports

Aliyekuwa nahodha wa klabu ya Simba, Mohammed Hussein ‘Tshablala’ ametangazwa kusajiliwa na klabu ya bingwa wa Ligi Kuu Tanzania, Yanga. Usajili huo umefanyika kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake katika klabu ya Simba. Sifa za nyota huyu si haba. Ni aina ya mabeki waliotikisa na kutawala katika nafasi ya beki wa kushoto. Mohammed Hussein ni jina kubwa katika kandanda nchini. Uhamisho wake kwenda Yanga unahitimisha tetesi za kuondoka klabuni hapo na kwenda kutafuta malisho sehemu nyingine. Miongoni mwa timu zilizoibuliwa katika tetesi hizo ilikuwa Kaizer Chiefs, ambapo mashabiki wake wameonesha hisia za huzuni baada ya nyota huyo kutangazwa kuwa mali ya klabu ya jangwani. Katika mitandao mbalimbali Afrika kusini mashabiki wa Kaizer Chiefs wanalalamikia sheria ya usajili wa wachezaji wa kigeni, ambayo imewabana na wanatamani ingeongezwa idadi ya kusajili. Katika makala haya TANZANIASPORTS inakuleta maswali matano muhimu na kukupa majibu maridhawa kutokana na maoni ya wataalamu wa soka nchini Tanzania. 

Simba wana pengo lake?

Iliwachukua muda mrefu kwa klabu ya Arsenal kuziba pengo la Patrick Viera baada ya kusajiliwa kwenda Juventus. Hali kadhalika klabu mbalimbali zimewahi kuhaha kupata wachezaji sahihi wa kuziba pengo linaloachwa na mchezaji aliyemaliza muda wake au aliyeuzwa kwa maslahi ya pande zote mbili. Klabu ya Simba ina kibarua cha kuhakikisha inawaridhisha washabiki wake kuwa usajili mpya wa beki wa kushoto ni yule mwenye uwezo wa kucheza viwango vya kimataifa kama Mohammed Hussein. Kuziba pengo la mchezaji si kazi rahisi. 

Taifa limechukua muda mrefu tangu alipoondoka Alphonce Modest katika soka la Tanzania hadi kupatikana kwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’. Hili linaweza kuonekana ni jambo kawaida, lakini hakuna namna ambayo unaweza kubeza mchango wa Kapteni wa Simba, Mohamed Hussein. Ligi Kuu Tanzania imeshuhudia nyota wengi kutoka nje ya nchi na ndani wakicheza kwa muda mrefu. 

Nafasi mbalimbali kama ushambuliaji, winga, kiungo na beki wa kati wamejitokeza wachezaji kadhaa na kupotea, lakini Mohamed Hussein alidumu katika ushindani Simba kwa zaidi ya kipindi cha miaka 10. Hali kadhalika pacha wake Shomari Kapombe ni miongoni mwa mabeki wakali wa Simba kama ilivyokuwa kwa Said Sued ‘Scud’. 

Imewachukua miaka mingi Simba kumpata Shomari Kapombe tangu walipoondokewa Said Sued katika nafasi ya beki wa kulia. Said Sued alikuwa miongoni mwa mabeki wakali, uwezo w akukukota mpira, chenga, kukaba muda wote wa dakika 90, kushambulia kupitia winga wa kulia, ilikuwa habari nyingine. Nyota ya Alphonce Modest ilihamia kwa Mohammed Hussein kwa kipaji, uimara, nidhamu na kutumikia Simba kwa upendo. 

Modest aliibukia Mtibwa Sugar, kisha kucheza soka bora kabisa na kuzivutia Simba na Yanga. Lakini ni kama vile kipaji chake kilikuja kuwanyima nafasi wengine kwani tangu alipoondoka kwenye soka namba tatu haikupata mchezaji wa maana. Ujio wa Mohammed Hussein uliipa Simba kujiamini na kutamba kuwa timu yenye beki bora.

Ni kitu gani cha ziada alichonacho Mohamed Hussein? 

Ujuzi, ufundi, uzoefu, umakini na uwezo mkubwa wa beki huyo wa kushoto kupachika bao katika mazingira ambayo mwenye ujuzi zaidi ni mshambuliaji. Mohamed Hussein anatukumbusha mabao ya Achraf Hakimi, mtoto wa Real Madrid alnayetamba katika klabu ya PSG. Hakimi anafunga mabao mengi kana kwamba ni mshambuliaji. Hicho ndicho kilichotokea kwa Mohammed Hussein, ana akili ya mpira, umri wake unampa uzoefu, amecheza mechi kubwa na zenye ushindani wa Kimataifa pamoja na kuwa nahodha wa timu kubwa. 

“Mo Hussein, huwezi kumweka benchi huyu kijana, kitakachomweka benchi labda mwenyewe ajichanganye kwa kufanya makosa mchezoni hasa mechi za derby, kupunguza ushindani na vitu vya kushusha kiwnago chake, lakini kama unazungumzia kazi yake, huyu ni mchezaji ana nidhamu sana, Zimbwe ni kati ya mabeki wazuri sana Afrika hapa anaweza kucheza timu yoyote unayoijua hapa kwenye timu za waarabu ana namba yake pale hilo halina ubishi.

Kiufundi, si mchezaji wa kumwambia vitu vingi, kama kocha namwambia Tshabalala, unaijua kazi yako, nenda kafanye. Au unafikiri mtu kama yule kocha wa Brazil, Luiz Felipe Scholari alikuwa na Roberto Carlos kwenye timu yake, hawezi kumwambia kingine, itakuwa hivi nenda kafanya kazi yako. Hawa ni wachezaji wenye baraka kiakili, nidhamu, na kiufundi,” amesema kocha maarufu nchini Tanzania (jina linahifadhiwa). Kocha huyo aliongeza kwa kusema, “tukiwa makini, tuanze kutafuta mrithi wake, pale Stars atastaafu, kama nchi na vilabu tuna mpango gani? Kingine huyu kiufundi anapokea mabailiko, walimu wanampa kazi mbili kulinda na kushambulia. Kama umeona baadhi ya mechi anaingia hadi eneo la ulinzi wa kati kuwasaidia namba 4 na 5.

Huu ufundi hupati kwa kila mchezaji,  hiki anachokifanya kilifanywa sana na Paolo Maldini, beki mkali wa kushoto halafu akawa anapewa kazi kuingia eneo la namba 4 na 5. Unamwona Hakimi pale PSG anaingia kwenye ushambuliaji, ni kazi, mwalimu anajua uzuri wa mtu huyu. Mwangalie Pascal Msindo anaweza kucheza wingi ya kushoto bila shida pale Taifa Stars, kazi unaona. Hawa ni wachezaji wa tofauti sana, tuandae wengine sasa.”

Je, amejifunza chochote kwa Cletous Chama?

Kiungo mshambuliaji Cletous Chota Chama alihama klabu ya Simba na kujiunga na Yanga. Tangu alipoondoka Simba, TANZANIASPORTS iliandika kutoa tahadhari kuwa nyota huyo asipokuwa makini anaweza kukosa namba kikosi cha kwanza. Cletous Chama licha ya kupangwa na makocha kadhaa waliopita jangwani, hakuwahi kuwa mchezaji chaguo la kwanza. Yanga wana wachezaji wenye ushindani mkali katika kila idara. Mchezaji anayepewa nafasi kikosi cha kwanza anajituma ili asiwekwe benchi mechi inayofuata. Mohammed Hussein amesajiliwa katika timu yenye ushindani mkubwa. Yeye ni mfalme wa Simba na Taifa Stars, lakini kwenye klabu ya Yanga kuna watu wa kazi kutoka nje. Lakini pia usajili huu unatuonesha kuwa Yanga wanataka huduma ya nyota huyu kuimarisha idara ya beki wa kushoto kwahiyo kujenga ufalme mpya pale Jangwani inahitajika kazi nzito.

Mashabiki wanasemaje?

Ingawa wachezaji wanasajiliwa kila mara kutoka Simba kwenda Yanga au mchezaji wa Yanga kwenda Simba. Wapo wengi kama Ibrahim Ajibu, Mrisho Ngassa,Edibily Lunyamila, Jean Baleke, Bernard Morrison, Jonas Mkude na wengineo wengi. Kwahiyo mashabiki wa Simba wanampenda Mohammed Hussein na kila mahali unaona wanamtakia heri aendako na mchezaji mwenyewe amewashukuru sana. huu ni utamaduni ambao umezoeleka sasa washabiki kuona jambo la kawaida kipenzi chao kwenda upande  mwingine wa timu. 

Je uongozi wa Simba umefeli?

Jibu lenye uhakika ni kuwa viongozi wa Simba wanafahamu umuhimu, maarifa na nguvu ya aliyekuwa nahodha wao, Mohammed Hussein hali kadhalika kocha wake Fadlu Davids. Mara kadhaa kocha wake Fadlu Davids amekuwa akimabadilisha kipindi cha pili na kuingiza beki mwingine ili kuimarisha safu ya ulinzi. Lakini huyu ni mchezaji ambaye alikuwa panga-pangua. 

TANZANIASPORTS inafahamu kuwa uongozi wa Simba uliafikiana na nahodha wao Mohammed Hussein tangu katikati ya msimu uliopita. Duru za kihabari zinasema uamuzi wa kuondoka Mohammed Hussein ulichukuliwa kipindi hicho na uongozi ulifahamu hilo. Kwa kuzingatia muktadha huo uongozi wa Simba unafahamu kuwa pengo la nyota huyo litazibwa. Hivyo basi mashabiki wa Simba kama ambavyo waliwaamini viongozi hao kumpa kitambaa cha unahodha Mohammed Hussein na kuishi naye miaka yote hiyo basi wanatakiwa kuwaamini tena katika usajili mwingine. Ndiyo mchezo wa soka ulivyo.

Written by Israel Saria

I have been involved with sports in Tanzania as a Volleyball Coach for many years—and was a Tanzania Amateur Volleyball Association (TAVA) leader. I studied sports management at Leipzig University in Germany and understand the science behind sports. That led me to work as a football pundit, with the BBC ( Swahili service) in London. That experience and exposure took me to covering the 2010, World Cup in South Africa. This provided me with a great insight into international level football commentary and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics.I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany, Italy, Belgium, Ireland, France, Kenya etc, and visited almost all of the key football stadiums across United Kingdom, and Europe.

Leave a Reply

Exit mobile version