Timu ya taifa ya soka Taifa Stars imekubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa washindani wao wa Kundi J Benin katika mfululizo wa mechi za kuwania kufuzu kwa Kombe la dunia mwaka 2022 nchini Qatar.
Mchezo huo ulichezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa umeonesha mambo hasi na chanya kwa kikosi cha Taifa Stars huku mashabiki wakitazama mchezo huo kupitia Televisheni baada ys Shirikisho la soka Afrika CAF kuzuia mashabiki kuingia viwanjani kama njia ya mbadala ya kupambana na corona.
KILIO CHA SAMATTA
Tathmini ya dakika 90 za mchezo huo, Benin haikuwa timu tishio mbele ya kikosi cha Taifa Stars, ndio maana baada ya mchezo huo nahodha wake Mbwana Samatta alielekea benchi huku akiwa amefunika kitambaa cha unahodha usoni na kuketi huku akiangusha kilio. Ni ishara ya wazi kuwa mzigo anaobeba ni mkubwa na timu imefanya jambo kubwa lakini haikupata mabao katika nafasi zote za wazi walizopata.
Ni bahati mbaya Taifa Stars kupoteza mchezo huo nyumbani ambapo kabla ilikuwa inaongoza Kundi J. Taifa Stars imefungwa ikiwa imetoka kuonesha kiwango bora katika mchezo wake na DRC ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 1-1 mjini Kinshasa. Pia ilicheza vizuri dhidi ya Madagascar na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 ndani ya dimba la Benjemin Mkapa.
Benin na Tanzania ndizo timu zilizokuwa zinaongoza Kundi J kabla ya kukutana zikiwa na pointi 4 kutokana na michezo miwili. Lakini sasa Benin wameibuka na ushindi ambao unawapa nafasi ya kuongoza Kundi J kwa kujikusanyia pointi 7 kutokana na michezo mitatu.
TAIFA STARS YENYE CHANYA NA HASI
Taifa Stars ilikuwa na kiwango bora, mbinu, uchezaji wa kitimu na hakika wachezaji walioonesha kiu ya ushindi pamoja na kusaka bao la mapema. Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilishuhudia Taifa Stars ikikosa mabao matatu ya wazi kupitia Simon Msuva n, John Bocco ambao walishindwa kutumbukiza mpira kimyani.
Huwezi kumlaumu kocha Kim Poulsen kwa makosa ya wazi ya washambuliaji wake kushindwa kufunga mabao. Hatari zilizoelekezwa lango la Benin zilipaswa kuzalisha mabao ya ushindi mapema kabla ya kuingia kipindi cha pili.
Kim Poulsen ametengeneza kikosi ambacho kinampa kiburi kuwa ni kizuri na wachezaji wameonesha kujiamini,kutulia,ufundi na namna gani kizazi hiki kinaweza kusonga
mbele kwenye mchezo wa soka. kutengeneza nafasi tatu za kufunga ina maana timu inao uwezo kupachika mabao zaidi. hilo ni jambo chanya, lakini hasi ni namna nafasi zinazopatikana hawakutumia vizuri matokeo yake tukaadhibiwa kwa nafasi moja waliyopata Benin.
NANI MCHEZAJI BORA?
Kwangu mimi Novatus Dismas anakuwa mchezaji wa aina yake kwa muda wa dakika 45 alizokuwepo uwanjani. Alikuwa kiungo mkabaji ambaye alikaba kila upande, aligawa mpira, alisaidia kushambulia, alichangia uwiano mzuri kati ya ulinzi na ushambuliaji.Kuna wakati alikuwa anapiga pasi ndefu kama za Xabi Alonso au Steven Gerard, nap engine kufanana na ‘mipasi’ ya Virjil van Diyk au Toni Kroos.
Dismas si kiungo wa daraja la nyota wa hapo, lakini anaonekana kuimarika zaidi katika mchezo huu. Katika mechi dhidi ya DRC alionesha ugeni lakini alimudu kutuliza akili a miguu uwanjani.
Mchezo dhidi ya Madagascar ulimpa nafasi ya kutengeneza jina lake katika kikosi na midomoni mwa mashabiki. Kwenye mchezo dhidi ya Benin nampa kura yangu Novatus Dismas kuwa mchezaji bora wa mechi.
KUNA MCHEZAJI PUNDA MWINGINE?
Sidhani kama kuna mchezaji anayejua kufanya kazi chafu uwanjani kwa sasa kama Muzamiru Yassin. Katika kipindi cha kwanza a,ishirikiana vme ana Novatus, na ilionekana mwenzake huyo alikuwa anamiliki dimba hilo na kutoa maelekezo namna ya kupanga amshambulizi kuanzia eneo hilo lililokuwa na viungo wakabaji wawili.
Baada ya Novatus kutolewa, Muzamiru akabaki peke yake eneo hilo, akafanya kazi nguvu ya kukimbia,kukaba, na matumizi ya nguvu. Muzamiru ndiye mchezaji anayesadikika kuwa Punda kuanzia klabu yake ya Simba hadi timu ya Taifa.
Mchezaji Punda ni yule ambaye anakuwa kama injini ya timu katika mchezo, anakaba,anacheza rafu,anadhibiti mbinu zote za wapinzani katika eneo lao la kiungo kila wanapopanga amshambulizi. Haikushangaza refa alipomuonya kwa kadi ya njano.
Huyu ni aina ya viungo wanaofanya kazi za kiungo mshambuliaji zionekane kuwa rahisi. Ndiye anarahisisha kazi za akina Rally Bwalya pale Simba au Feisal Salum katika timu ya taifa.
KIZAZI KIPYA BILA KEVIN JOHN?
Kuna kizazi kipya cha soka kinazidi kuibuka. Jambo zuri ni muunganiko wa kikosi cha vijana chini ya miaka 17 kilichocheza kwenye fainali za vijana huko Gabon miaka kadhaa iliyopita.
Kim Poulsen amekilinda kizazi hiki, Israel Mwenda, Dickson Job,Novatus Dismas,Meshack Abraham,Nickson Kibabage,Ramadhani Kabwili,Shomari Kibwana ni wachezaji waliokuwepo katika kikosi cha vijana.
Lakini mbele yao kuna Kibu Denis,Lusajo Mwaikenda,Reliant Lusajo kwa kuwataja wachache. Hata hivyo kwa aina ya washambuliaji wetu waliopo, ni dhahiri kinda wa KRC Genk, Kevin John anaweza kuchukua nafasi ya mtu pale mbele.
Mchezaji ambaye anaweza kutumikia muda mrefu katika kikosi cha Kim Poulsen ni Kibu Dennis, kwa sababu ni mchezaji anayepangua ngome ya adui, ana nguvu na uwezo mzuri wa kumiliki mpira. Hili ni msaada kwa Taifa Stars lakini mpango wa pili usitegemee kwa Kibu peke yake bali hata kuitwa Kevin John ni uamuzi mzuri.
KINARA WA KUNDI
Hadi sasa kinara wa kundi ni Benin ambaye anazo pointi 8 baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare mmoja. DRC wanashika nafasi ya pili kwa kushinda mechi moja na kutoka sare mbili hivyo wana pointi 5. Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa pointi 4, huku Madagascar ikiwa inaburuza mkia. Mchezo mwingine DRC wamemfunga Madagascar mabao 2-0. Bado Taifa Stars inayo nafasi katika michezo mitatu ijayo dhidi ya DRC nyumbani na mbili za ugenini nchini Madagascar na Benin.
Comments
Loading…