*Bendtner wa Arsenal matatani tena
Tottenham Hotspur wamejiweka katika nafasi ngumu ya kufuzu robo fainali ya Ligi ya Europa baad aya kukubali kichapo cha mabao 3-1.
Wakicheza nyumbani White Hart Lane, Spurs wanaofundishwa na Kocha Tim Sherwood walitarajiwa kuwadhibiti Benfica wa Ureno, lakini waliwaacha washabiki wao wakisononeka na kuondoka vichwa chini usiku wa Alhamisi hii.
Benfica msimu uliopita walikwenda gadi fainali na kupoteza kwa mabao 2-1 kwa Chelsea msimu uliopita na sasa wanapewa nafasi kubwa zaidi ya kusonga mbele, watakaporudiana na Spurs jijini Lisbon Alhamisi ijayo.
Spurs ambao Jumapili hii wanachuana na mahasimu wao wa London Kaskazini, Arsenal kwenye Ligi Kuu ya England, watatakiwa kupata mabao matatu dhidi ya Benfica Alhamisi ijayo ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele, kibarua ambacho ni kigumu mbele ya mashabiki wa wapinzani wao.
Sherwood alikuwa ameshawaonya wachezaji wake, akisema kwamba kiwango wanachoonesha ni kwa ajili ya hatima yao, hasa baada ya kukung’utwa na Chelsea 4-0 kwenye EPL Jumamosi iliyiopita, akatarajia kwamba wangejibu mapigo kwa mchezo mkali, maana wenyewe wana majina makali.
Sherwood naye aliingia matatani na kocha wa Benfica, Jorge Jesus akisema kwamba hajiheshimu na hana hadhi, tofauti na alivyowaona wachezaji wake.
Kocha huyo wa Benfica alishangilia bao lao la tatu kwa kuonesha vidole vitatu mbele ya benchi la ufundi la Spurs, kitendo kilichomuudhi Mwingereza huyu na baada ya kipenga cha mwisho hawakupeana mikono ya kwa heri.
Sherwood alionekana kutaka kumvaa Jesus lakini mwamuzi wa akiba aliwatenganisha na wawili hao wakabaki wakihasimiana kwenye eneo lao la kujidai, lakini Sherwood akiumia kwa jinsi alivyoipoteza mechi na kwa mabao mengi.
BENDTNER AZUA BALAA TENA
Mshambuliaji wa kati wa Arsenal, Nicklas Bendtner ameingia matatani baada ya kufanya makosa mawili.
Moja ni kutoroka London na kusafiri hadi Copenhagen wiki hii, lakini pia kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 aliyeisha makali ya kupachika mabao anadaiwa kupigana baada ya kunywa pombe kupita kiasi.
Kocha Arsene Wenger amethbitisha kwamba Bendtner ambaye mkataba wake na Arsenal unamalizika mwishoni mwa msimu huu hakuruhusiwa kusafiri, ataadhibiwa kwa kutozwa faini na kwamba makazi yake Arsenal yanaelekea mwishoni.
Mdanishi huyo ameshapata miksa mingine kadhaa ya utovu wa nidhamu, ikiwa ni pamoja na kuvunja kitasa cha bafu kwenye bwawa la kuogelea usiku baada ya kupata kinywaji akifurahia ushindi wa Arsenal dhidi ya Liverpool na pia kwa kushusha kaptura yake ili kuonesha tangazo la kampuni ya umeme lililokuwa kwenye nguo yake ya ndani.
Comments
Loading…