Ni Desemba 11 mwaka 2021. Ni mechi ya watani wa jadi itakayochezwa saa 11 jioni kwa saa za Tanzania na Afrika mashariki ndani ya dimba la Benjamin Mkapa. Ni mechi ya wakongwe wa soka na Ligi Kuu Tanzania Bara. Ni mfululizo wa Ligi kuu Tanzania Bara kwa msimu 2021/2022, ambapo timu zote mbili zinafukuzana, Yanga wapo kileleni mwa Ligi wakiwa na pointi 19, huku Simba wakiwa nafasi ya pili kwa kujikusanyia pointi 17.
Ni mchezo muhimu kwa pande zote mbili, kutafuta alama tatu na kutengeneza heshima. Ili uchukue ubingwa unapaswa kuhakikisha hufungwi na timu kubwa, angalau unatafuta alama moja.
Unapomfunga mshindani wako unamdhibiti katika kasi yake, na hivyo mechi zinazofuata huwa ni kuhakikisha unawabutua timu ndogo zote kadii unavyojisikia. Yanga waliwafunga Simba kwa bao 1-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii lililofungwa na Fiston Mayele, lakini Simba wanaonekana kutaka kulipa kisasi.
TANZANIASPORTS inaangazia masuala muhimu ambayo kwa kawaida mchezo mkubwa unaohusisha timu kubwa lazima kuwe na mambo ya aina yake. ni mambo ambayo yanaonesha uwezo,ubora,weledi,uchu na matamanio ya kunyakua ubingwa kwa kuwachapa washindani wao wakubwa.
WABABE WA DAKIKA 90
Timu zote zina wachezaji wababe ndani ya dakika 90. Simba wapo wabeb kama Pascal Wawa, Jonas Mkude,Taddeo Lweanga,Joash Onyango,Kennedy Juma na Bernard Morrison. Yanga wanao wababe wao kama vile Khalid Aucho,Bakari Mwamnyeto,Djuma Shaban,Yannick Bangala. Wachezaji hawa wanasifika kwa matumizi ya nguvu kwa kiasi kikubwa. Wana uwezo wa kukabiliana na wapinzani wao kwa mabavu bila kuchoka ndani ya dakika 90.
WACHEZAJI WA KUCHUNGWA
Mchezo wa aina hiyo kwa kawaida unatawaliwa na wachezaji wenye matukio ya kushangaza au wale ambao wanapaswa kuchungwa kwa muda wote wanaokuwepo uwanjani.
Wachezaji wa Yanga wanafahamu ukali wa Bernanrd Morrison wa Simba na bila shaka walimtazama katika mechi zote mbili alizocheza hivi karibuni dhidi ya Red Arrows ya Zambia kwenye mchezo wa kufuzu hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la soka Afrika.
Kasi ya Morrison na uwezo wake wa kukaa na mpura ulikuwa mwiba kwa wachezaji wa Red Arrows. Hata walipokuja kutulia na kujairbu kumdhibiti walikuwa wameshachelewa. Hivyo safu ya kiungo cha Yanga watakuwa na kibarua cha kumchunga nyota huyu.
Simba wao watataka kuhakikisha wanavuruga mipango yote inayoandaliwa kumfikia Fiston Mayele. Kiuchezaji Mayele anategemea mpangilio wa mashambulizi na kusogezewa mpira hadi eneo la hatari.
Kazi hiyo inategemewa kufanywa na Feisal Salum kuwavuruga mabeki wa Simba. Ili Feisal Salum afanye kazi yake vizuri atategemea uwezo wa Tonombe Mukoko,Zawadi Mauya, Khalid Aucho na Yannick Bangala, na mabeki wa pembeni Kibwana Shomari na Djuma Shaban. Kazi nyingine ya Simba itakuwa kuwadhibiti mawinga wa Yanga, Jesus Moloko na Farid Mussa kwa sababu walikuwa mwiba katika mchezo uliopita.
Simba nao wanaye kiungo wao Hassan Dilunga ambaye ameibuka kuwa mchezaji hatari,kasi na mbinu nzuri za kutafuta mabao. Mabeki wa Yanga wa pembeni Djuma Shaban,Kibwana SHomari,Mustafa Yassin na Bryson Rafael watakuwa na kibarua kuhakikisha kiungo huyo haleti madhara.
Dilunga amekuwa mchezaji anayebadilika kila siku, na ubora wake umeongezeka. Katika michezo miwili ya Kombe la Shirikisho amekuwa katika kiwango kizuri kutengeneza na kufunga. Spidi na uwezo wa kukaa na mpira pamoja na kuwasoma wapinzani wake ni silaha ya Pablo Franco Martin.
ROHO ZA PAKA
Timu zote mbili zina wachezaji wenye roho ya Paka katika safu za ulinzi. Simba wanao walinzi wawili weenye roho za paka, Pascal Wawa na Joash Onyango, wakati Yanga wanaye Bakari Mwamnyeto, Yannick Bangala na Dickson Job. Mabeki hawa Job N Mwamnyeto wamekuwa wagumu kupitika na wameonesha umahiri katika mechi mbalimbali za Ligi Kuu. Mtihani walionao washambuliaji wa Simba na Yanga ni kuwazidi maarifa mabeki hao kisha kupachika mabao. Je itawezekana?
WAKALI WA NDANI YA BOKSI
Fiston Mayele sio mshambuliaji wa kukokota mpira kutoka mbali kama ilivyo kwa Herieter Makambo. Mayele kwa Yanga na Medie Kagere kwa Simba wanapenda kujipanga katika boksi, kisha kupata nafasi ya kutupia mabao. Kagere na Mayele sio aina ya washambuliaji ambao wanakokota mpira kutoka mbali kuingia eneo la hatari, badala yake hawa wanatupia wavuni wakiwa ndani ya boksi. Kuwaacha katika eneo hilo bila kuwazuia ni hatari kwa timu pinzani.
USHINDANI MKALI
Simba hawataki kufungwa tena na Yanga kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii Septemba 29 mwaka huu. Yanga hawataki kufungwa na wanataka kuendeleza ubabe kwa kuwachapa watani hao. Simba watataka kurudia kile walichokifanya Julai 7 kwenye fainali ya Kombe la ASFC kwenye uwanja wa Lake Tanganyika kwa kuwachapa bao 1-0 lililofungwa na Luis Miquissone. Yanga nao watataka kuendeleza ubabe kama ule waliofanya kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar ambako waliifunga Simba kwa penati 4-3. Simba watakuwa na uchungu mwingine wa Julai 3 mwaka huu baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 toka Yanga lililofungwa na kiungo mkabaji Zawadi Mauya.
MIFUMO YA KUAMUA MATOKEO
Makocha wa timu zote mbili watakuwa na kibarua cha kuchagua mifumo sahihi ya kuwafunga wapinzani wao. Timu zote mbili zimekuwa katika mifumo mitatu rasmi; 3-4- 3, 4-3-3 na 4-2-3-1.
Mifumo yote hiyo inatengeneza mshambuliaji wa kucheka na nyavu akiwa peke yake huku akizungukwa na mawinga na viungo wa kupachika mabao.
Pablo Franco Martin na Nasredine Nabi watakuwa na kibarua kigumu kuwatuliza wachezaji wao kwa sababu mechi kubwa kama hiyo huambatana na matukio ya kushangaza,presha na kusababisha kupoteza umakini ndani ya dakika 90. Vyovyote vile itakavyokuwa ni mechi kubwa na yenye kila aina ya shinikizo kwa makocha,viongozi na wachezaji.
MAREFA KUNG’ARA?
Heri Sassi kutoka mkoa wa Dar es salaam ndiye mwamuzi aliyekabidhiwa jukumu la kuziamua Yanga na Simba. Ni mwamuzi ambaye anakabiliwa na kibarua kigumu kusafisha nyota ya waamuzi wa Ligi kuu Bara baada kukosolewa kutokana na maamuzi mabovu waliyofanya mara kwa mara. Katika mchezo huo waamuzi wa pembeni yaani washika vibendera ni Kassim Mpanga kutoka Dar es salaam na Hamdani Said kutoka mkoani Mtwara, wakati mwamuzi wa akiba ni Ahmada Simba kutka mkoani Kagera. Bila shaka matokeo yataonekana kama wamefanikiwa kuonesha umahiri au watafeli.
Comments
Loading…