TAMASHA kubwa nchini limefanyika. Tamasha la klabu ya Simba lilianzishwa miaka 15 iliyopita na aliyekuwa Mwenyekiti wake, Hassan Dalali. Wakati maelfu ya washabiki wa mpira nchini wakitupia macho tamasha la Simba tayari walishaona lingine la watani wao wa jadi Yanga. Kila tamasha limekuwa na vivutio vyake, lakini hili la Simba limeonesha namna walivyo tayari kwa ushindani na zaidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameonesha namna alivyo ‘mtu poa’.
Ni mtu poa kwa namna pozi alilosimama na wachezaji wa Simba, amejiachia, tabasamu nene, wachezaji wameduwaa huku wakijawa na matabasamu. Irudie tena ile picha kisha waone wachezaji wa Simba. Mtazame Kennedy Juma aliyesimama nyuma ya Rais Samia, kisha mgeukie Mwenyekiti wao Murtaza Mangungu, halafu mtazameMtazame Kennedy Juma, kwa hakika utaona kuwa Simba walijawa na furaha kubwa kuheshimishwa na rais wa nchi.
Hali kadhalika utambulisho na shughuli nzima ya tamasha la Simba ilijaa vitu vizuri,wachezaji wazuri, benchi la ufundi zuri na uongozi uliopania kufanya vizuri kwa kusimamia kila kitu kuwa katika hali nzuri. Hao ndiyo Simba, shime kwa viongozi wake wazidishe kuleta furaha hiyo bila kusingizia chochote.
Sasa, baada ya furaha na shamra sharma za tamasha hili limebaki swali moja kwa msimu ulopo mbele yetu. Je Simba atanguruma tena? Ikumbukwe Simba wameshanguruma mara nyingi, na wameutwaa ubingwa misimu minne mfululizo kabla ya kupepesuka kidogo na kumwacha mtani wao Yanga akitamba misimu miwili.
Katika misimu yote minne Simba walikuwa na makocha tofauti na mbinu zimekuwa tofauti. Hata hivyo Simba wamebahatika kitu kimoja; kulinda uti wa mgongo wa timu. Kama kusajili wamekubali kubakiza nyota wao, huku baadhi wakiwaondoa. Lakini Simba imebaki kuwa katika msingi wa kuhakikisha kikosi chao kinakuwa na uti wa mgongo imara.
Ligi Kuu NBC
Msimu ujao mambo yanatakiwa kuwa moto. Simba wameonesha kikosi chao, kuna wachezaji wana miili mirefu, miguu inayonasa mipira kama wameweka gundi. Uwezo wa kikosi kizima ni wa juu, uwezo binafsi nao uko juu. Pia timu inaundwa na wachezaji wachanga na wenye uzoefu. Kwahiyo msimu ujao Simba wanatakiwa kunguruma mbele ya watani wao wa jadi bila kujali wanatumia mfumo gani kiuchezaji. Simba hii si ile ya kusubiria mpinzani wake ateleze bali ni timu yenye kila sababu ya kufanya vizuri.
Msimu ujao unaonesha wazi timu zimejipanga kwa kuangalia namna zinavyosajili. Msimu uliopita timu zilizoleta changamoto ni Singida Fountain Gate na Azam Fc. Kwa usajili wao, msimu ujao pia utakuwa na changamoto nyingi kwa Simba. Kwa ukubwa wake, kwa umahiri wake, Simba wanaweza kupindua matokeo kwa timu yoyote. Hapo sasa mashabiki wanatakiwa kuambiwa wasubiri taji la Ligi Kuu.
Mabao kila kona
Msimu uliopita Simba walikuwa wanafunga mabao kutokea kila upande. Hili halizungumzwi sana, lakini ukweli upo wazi. Simba wanaweza kukusumbua kutokea upande wowote, iwe wingi ya kulia au kushoto, ama washambuliaji wa kati pamoja na viungo wao. Ufungaji wa mabao wa Simba unaleta homa, tena homa kali sana. Saido Ntibazonkiza ametengeneza mabao na kufunga mengi msimu uliopita.
Katika mechi ya tamasha la Simba alitengeneza mabao na kudhihirisha licha ya kutaniwa kuwa ni mzee bado ana moto mkali mguuni. Saido anawapa changamoto hata wachezaji vijana wa Simba kuwa ili kumpokonya namba wana kazi kubwa ya kufanya.
Kufunga mabao mengi ndiyo siri inayowapa Simba kufukuzia ubingwa kimya kimya. Kwa vile safu ya ushambuliaji haijabomolewa, bila shaka mashabiki watakuwa na kiu ileile ya kuona uwingi wa mabao msimu ujao. Kuna kipa atamudu shughuli za washambuliaji wa Simba? Ngoja tuone msimu ujao.
Mashabiki wamechoka robo fainali
Ndiyo, furaha ya mashabiki wa Simba si tamasha tu, bali ndani ya dimba wanataka kuona timu yao ikipanda ngazi kimafanikio. Wanashinikiza mafanikio kwa kuujaza uwanja. Kwenye tamasha lao wanajaa, kwenye mechi wanajaa, kwenye shughuli za kununua jezi nako ujazo unakuwa mkubwa. Hata hivyo mashabiki nao wanaweza kuchoka, hasa pale timu yao ikiishia tena robo fainali ya mashindano ya CAF.
Simba ni taasisi kubwa barani Afrika, inatupiwa macho na wachezaji na makocha wengi wanaotamani kufundisha timu hiyo wakiwa na imani kuwa ina bahati na uwezo wa kutamba kimataifa na uwaandikia wasifu mzuri. Kwahiyo katika mashindano ya CAF lazima tukubali mashabiki wanachoka, wanataka kuona Simba ikirudi mitaa ya Msimbazi ikiwa na ubingwa wa Afrika.
Hapa tulipo Simba wanatakiwa kuhakikisha malengo yao ni kutwaa kombe, iwe African Super League (CAF Super League) au Kombe la Shirikisho. Hakuna sababu nzito ya kusema Simba hii inajipanga kufika hatua ya makundi au robo na nusu fainali. Chini ya uongozi wa Murtaza Mangungu na Afisa Mtendaji wake Imani Majura lengo liwe moja tu; kutwaa kombe lolote la CAF. Wao akili zao ziwe kutwa kombe tu bila kujali wana kikosi cha kuwafikisha wapi. Kadiri sifa zao zinavyokua ndivyo shinikizo la kutwaa kombe linavyozidi. Ilipofika Simba ni parefu sana, sasa kazi iwe kombe tu. Kocha anayepewa malengo iwe kutwaa kombe tu, asilete hadaa kuwa haijawahi kuchukua kombe la mashindano ya CAF bali afuate maagizo tu.
Comments
Loading…