in , , ,

Simba vs Kagera, Vurugu mtindo mmoja…..

Changamoto kwa Rais Mpya wa TFF

Goli la kusawazisha la penalti katika dakika ya mwisho la Kagera Sugar dhidi ya Simba jana lilizua kizaazaa kutoka kwa mashabiki waliodaiwa kuwa wa miamba hao wa soka nchini walioanza kung’oa viti na kurusha vitu mbalimbali uwanjani na kuwalazimisha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwasambaratisha katika mechi iliyoisha kwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Simba waliongoza kwa goli la kipindi cha kwanza lililofungwa na mshambuliaji Amisi Tambwe na lilidumu hadi katika dakika za lalasalama.

Wakati Simba wakiamini mechi ingelimalizika matokeo yakiwa 1-0, kiungo George Kavilla wa Kagera alipenyeza pasi ndefu kwa Daudi Jumanne aliyekuwa katikati ya mabeki wa Simba ndani ya boksi na beki wa kati Mganda Joseph Owino alimdondosha Jumanne aliyekuwa anataka kufumua shuti kufunga katika dakika ya tatu kati ya nne zilizoongezwa za majeruhi.

Kutokana na faulo hiyo, refa Mohamed Theofile kutoka Morogoro aliamuru ‘tuta’ lililofungwa na beki wa zamani wa Simba, Salum Kanoni.

Baada ya goli hilo kufungwa, washabiki wa Simba walianza kung’oa viti vya Uwanja wa Taifa kwenye Jukwaa la Simba lililopo Kaskazini mwa uwanja huo wenye uwezo wa kuketisha watazamaji 57,558, hali iliyowalazimu polisi kufyatua mabomu ya machozi na kuufanya uwanja huo kugeuka kuwa wa vita.

Wachezaji wa Simba wakauweka mpira katikati ya uwanja kwa ajili kabla ya refa kupuliza kipenga cha mwisho.

Huku vurugu zikiendelea majukwaani, nahodha wa Simba, Nassor Masoud ‘Chollo’ aliondolewa na polisi wakati akijaribu kumfuata mwamuzi baada ya kipenga cha mwisho.
Mashabiki kadhaa waliwekwa chini ya ulinzi katika kudhibiti vurugu hizo.

Basi la timu ya Simba kwa mara ya pili ndani ya wiki moja lililazimika kusindikizwa na magari ‘Defender’ tatu za polisi na gari la maji ya kuwasha ili kuwalinda wachezaji dhidi ya mashabiki wao wenye hasira.

Mama aitwaye Fii Kambi, shabiki wa Simba kutoka Tawi la Mpira Pesa aliyekuwa kwenye Jukwaa la Simba, alianguka na kuzirai baada ya mabomu kuanza kupigwa. Alilazwa kwenye chumba cha matibabu cha Uwanja wa Taifa kabla ya gari la wagonjwa la hospitali ya Muhimbili kumchukua kumpeleka hospitalini.

Kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni ‘King’ alisema alitarajia vurugu hizo zingetokea kutoka na uamuzi wa marefa ambao haukumvutia.

“Sijafurahishwa na maamuzi ya marefa wa leo (jana) ambao mimi nawaita (akatukana). Na nilijua mwisho wa mchezo kutatokea vurugu,” alisema kocha huyo ambaye msimu uliopita alikuwa akiwafundisha mahasimu wake wa jana, Kagera Sugar.

Kocha wa Kagera Sugar, Jackson Mayanja aliwasifu wachezaji wake baada ya sare hiyo. “Wachezaji wamefanya kazi nzuri hasa kipindi cha pili. Waamuzi wamefanya kazi yao vizuri. Mabadiliko ya wachezaji wawili (Adam Kingwande na Juma Mpola) yametusaidia sana,” alisema. Simba haikufanya mabadiliko ya kikosi kilichoanza jana.

Mechi ya jana ilikuwa ya kwanza kwa kipa Mganda Abel Dhaira kuanzia benchini Simba tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Agosti 24.

Ukiwaondoa beki Martin Muganyizi na kiungo Zuberi Dabi, kikosi cha Kagera kilichoanza katika mechi yao ya ligi hiyo dhidi ya Yanga mjini Bukoba Oktoba 12, ndicho kilichoanza katika mechi ya jana. Nafasi za wawili hao katika mechi hiyo waliyolala 2-1 dhidi ya Yanga zilichukuliwa na Geofrey Wambura na Suleiman Kibuta.

Kagera Sugar walianza kwa kasi mpira wakipiga pasi zao fupi fupi na kuwachanganya wachezaji wa Simba ambao walikuwa wakilazimika kucheza rafu kuwapunguza kasi wageni wao.

Hadi dakika ya nane, kikosi cha ‘Wanamsimbazi’ kilikuwa kimecheza rafu 5-0 huku kiungo ‘fundi’ Hamis Ndemla akilimwa kadi ya njano na refa Theofile baada ya kumkwatua George Kavilla wa Kagera katikati ya uwanja katika dakika ya saba.

Tambwe aliifungia Simba goli la kuongoza katika dakika ya tatu kati ya tano zilizoongezwa za majeruhi za kipindi cha kwanza baada ya kumlamba chenga beki kisiki Ernest Mwalupani na kipa mtokeabenchi Hannington Kalyesubula na kufunga akiitendea haki pasi ndefu iliyopenyezwa na beki wa pembeni Issa Rashidi ‘Baba Ubaya’.

Goli hilo lililodumu hadi mapumziko lilimfanya Tambwe afikishe magoli tisa katika mechi 10 alizoitumikia Simba msimu huu.

Hakucheza mechi ya ufunguzi walioshikwa kwa sare ya 2-2 dhidi ya wageni wa ligi kuu Rhino Rangers mjini Tabora baada ya kukosa hati ya uhamisho wa kimataifa (ITC), kabla ya kuja kukosa mechi iliyopita waliyolala 2-1 dhidi ya Azam FC kutokana na majeraha.

William Lucian aliinyima timu yake ya Simba goli la wazi akipaisha ndani ya sita mpira uliotemwa na kipa Kalyesubula kufuatia shuti kali la nahodha wa Nassoro Masoud ‘Chollo’ katika dakika ya 34.

Kipa Antony alilazimika kutolewa baada ya kugongana na mshambuliaji Betram Mwombeki wa Simba katika dakika ya nane tu ya mechi hiyo. Alitibiwa na kuendelea na mchezo lakini kadri muda ulivyokuwa unasonga maumivu yakawa makali zaidi kwenye mkono wake wa kulia, akatoka.

Dakika ya 62 Themi Felix aliachia kombora kali, mpira ukagonga mwamba wa goli kisha ukadondoka chini kabla ya kurudi katikati ya uwanja katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na mashabiki wachache.

Simba inaendelea kubaki katika nafasi ya nne ya msimamo ikiwa na pointi 21 baada ya mechi 12, nyuma ya vinara Azam na Mbeya City wenye pointi 23, huku Yanga ikiwa katika nafasi ya tatu kwa pointi 22 baada ya mechi 11.

Vikosi vilikuwa; Simba: Abuu Hashimu, Nassoro Masoud ‘Chollo’, Issa Rashid, Joseph Owino, Hassan Khatib, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Said Ndemla, Betram Mwombeki, Amisi Tambwe na William Lucian

Kagera Sugar: Agaton Antony/ Hannington Kalyesubula, Salum Kanoni, Martin Muganyizi, Ernest Mwalupani, Malegezi Mwangwa, Zuberi Dabi/ Juma Mpola (dk.46), Benjamin Asukule/ Adam Kingwande (dk. 46), George Kavilla, Themi Felix, Daudi Jumanne na Paul Ngwai

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Man City, Spurs zasonga mbele

LEADERSHIP COURSE COMES TO A CLOSE IN TANGA