in ,

SIMBA v. YANGA: TUSUBIRI DAKIKA TISINI

*VPL*

 

Wikiendi hii Ligi Kuu Tanzania Bara inaingia kwenye mzunguko wa nne. Jumla ya michezo nane itapigwa katika siku za Jumamosi na Jumapili. Hata hivyo macho na masikio ya mashabiki wa soka Tanzania yapo kwenye mchezo mmoja tu. Huo ni mchezo  wa watani wa jadi, Simba na Yanga utakaopigwa kwenye dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam kesho Jumamosi.

Timu zote hizi mbili zimeshinda michezo yao mitatu ya kwanza. Yanga ambao wanaongoza ligi kwa tofauti ya mabao waliwafunga Coastal Union, Tanzania Prisons halafu JKT Ruvu huku Simba wakipata ushindi dhidi ya African Sports, Mgambo JKT na kisha Kagera Sugar.

Nafikiri kuwa na matokeo ya asilimia mia moja ya michezo mitatu ya awali kunaipa kila timu kati ya hizi mbili hali ya kujiamini kwa kiasi fulani. Hata hivyo pengine Yanga ambao ni mabingwa watetezi wa ligi hii wapo kwenye presha kutokana na ukweli kuwa wamekuwa wakipata matokeo mabaya dhidi ya Simba kwa muda wa miaka miwili sasa kwenye ligi hii.

Kikosi cha timu ya Yanga.
Kikosi cha timu ya Yanga.

Mara ya mwisho Yanga walipowafunga Simba ilikuwa ni Mei 2013.  Yanga walishinda mchezo huo kwa mabao mawili kwa sifuri ambapo Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza ndio waliopeleka kilio hicho Msimbazi.

Hilo linawafanya Yanga kuwa na woga na hofu kuelekea mchezo wa kesho ingawa wanaonekana kuwa na kikosi imara zaidi ya kile cha Simba kwa sasa. Kwenye misimu miwili iliyopita Yanga pia walikuwa imara zaidi ya Simba lakini hawakuweza kuwafunga Simba kwenye michezo yote minne ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Nahodha wa Yanga Nadir Haroub amedai kuchoshwa na uonevu ambao wamekuwa wakikutana nao dhidi ya Simba. “Mimi na wachezaji wenzangu tupo vizuri kuikabili Simba, matokeo mabaya kwenye mechi yao sasa basi tumechoka, watatujua siku hiyo,” alisema nahodha huyo akiongea na HabariLeo.

Pengine kuchoshwa na matokeo mabaya wanapokutana na Simba kunaweza kuwapa morali wachezaji wa Yanga katika kukabiliana na Simba hapo kesho. Mbaka sasa mabingwa hao watetezi wameshafunga jumla ya mabao 9 kwenye michezo mitatu huku wakiruhusu bao moja tu. Amis Tambwe na Donald Ngoma ndio vinara wa mabao kwenye timu hiyo kila mmoja akiwa amepachika matatu.

Simba wao wanonekana kuwa katika hali ya kujiamini zaidi kuelekea mchezo wa kesho. Pengine ni kwa sababu ya matokeo ya michezo ambayo wamecheza na Yanga hivi karibuni. Bila shaka matokeo mazuri ambayo wameyapata kwenye michezo mitatu ya awali nayo ni sababu ya kijiamini kwao.

Kikosi cha timu ya Simba.
Kikosi cha timu ya Simba.

Wekundu hao wa Msimbazi wana alama tisa sawa na Yanga huku wakiwa na magoli sita ya kufunga na wameruhusu bao moja. Hamis Kiiza ambaye Mei 2013 akiwa Yanga aliwafunga bao Wekundu hawa kwenye mchezo wa mwisho walipofungwa na Yanga ndiye kinara wao wa mabao kwa sasa. Ameweka wavuni mabao matano kati ya sita ambayo Simba wamefunga. Huenda hapo kesho ataiangamiza timu yake ya zamani.

Kocha mkuu wa Simba Dylan Kerr ametamba kuwa anawafahamu vizuri Yanga hivyo haoni sababu ya kushindwa kuwafunga hapo kesho. “Nataka kuwafunga Yanga Jumamosi, sioni sababu kwanini tushindwe kuwafunga. Nina wachezaji wazuri na wote wako na afya njema kimwili na kiakili, hivyo sina wasiwasi”, aliimbia Mwanaspoti.

Yameshasemwa mengi na kila timu imeshajiandaa kukabiliana na nyingine hapo kesho. Dylan Kerr amesema kuwa tusubiri tuone timu gani ni bora zaidi hapo kesho. Naungana naye kwa kusema tusubiri dakika tisini.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Waingereza wanavyojenga soka ya Ufaransa

Tanzania Sports

KASHFA YA JINAI FIFA: