Ingawa Yanga ni klabu iliyotwaa mataji ya Ligi Kuu mengi zaidi kuliko zingine nchini Tanzania, lakini Simba ndio yenye mafanikio zaidi kwenye soka la Kimataifa. Yanga wamelitwaa taji la Ligi Kuu mara 27.
Hata hivyo kwenye michuano ya kimataifa jina la klabu ya Simba linachomoza zaidi kuliko Yanga. Hiyo ni miongoni mwa sababu ambazo zinaifanya timu hiyo kwa sasa kuwa katikati ya vigogo wa soka barani Afrika ambao wanatarajiwa kushiriki African Super League.
Wakati mwaka 2021 unaeleke ukingoni ni wakati ambao bila shaka yoyote Shirikisho la Soka Afrika lipo kwenye hatua za mwisho za kutengeneza utaratibu wa kuendesha mashindano ya Africa Super League. Swali je timu zipi zinaweza kushiriki African Super League?
TANZANIASPORTS katika uchambuzi huu inaangazia sifa mbalimbali za timu ambazo zinatarajiwa kushiriki mashindano hayo. Kati ya timu 20 zinazotakiwa kushiriki mashindano hayo, tayari timu 15 zinajulikana, miongoni mwao ni Simba ikichomoza kutoka ukanda wa Afrika masshariki.
AL AHLY (Misri)
Mabingwa wasioshindika barani Afrika kwa muda mrefu na ndio klabu ya karne katika bara hilo kwa mujibu wa shiikisho la CAF. Hakuna wasiwasi wowote kwa timu hii kuwa nambari moja katika soka barani Afrika kwa sababu mafanikio yake yanajieleza bayana.
Baada ya kufungwa katika fainali mbili za Ligi ya Mabingwa mwaka 2017 na 2018, walifanikiwa kurekebisha makosa yao na kuwa timu kabambe Afrika. Na sasa wamefanikiwa kutwaa mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika mfululizo. Ni miongoni mwa alama ya soka la kiarabu barani Afrika.
ESPERANCE (Tunisia)
Ukizungumzia soka la Afrika na mafanikio yake ngazi ya klabu bila shaka hii ni klabu mojawpao itakayokuwa kwenye orodha yako. Mafanikio yao makubwa ni baada ya kutwaa mataji mawili mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2018 na 2019. Hii nayo ni timu inayotarajiwa kushiriki African Super League. Bila shaka yoyote watatoa ushindani mkali kwenye michuano hiyo kama ilivyo ada kwao.
WYDAD CASABLANCA (Morocco)
Watanzania wengi wanaifuatilia klabu hii. Sababu moja kubwa ni kuwepo kwa nyota wao Simon Msuva ambaye amewahi kutamba katika klabu ya Yanga miaka ya nyuma. Msuva anakipiga katika klabu yenye ushindani mkali kwemye Ligi Kuu Morocco.
Klabu hii ilitwaa taji la Ligi ya Mabingwa baran Afrika mwaka 2017, na mwaka 2019 ilifika fainali ya Ligi hiyo lakini ikachapwa Esperance ya Tunisia. Kuanzishwa kwa African Super League kutashuhudiwa tena umahiri na ushindani wao wanaotoa kila mara ikiwemo msimu uliopita ambako walitolewa katika hatua ya nusu fainali na Kaizer Chiefs.
RAJA CASABLANCA (Morocco)
Ni miamba mingine kutoka nchini Morocco ikiwa na sifa za kipekee katika mashindano ya soka barani Afrika. Miamba imerudi Ligi ya Mabingwa baada ya kupoteana kwa miaka 15 bila kushiriki mashindano makubwa Afrika. Na sasa Raja Casablanca wanarejesha makali yao.
Ndani ya miaka minne wameshinda mataji mawili ya Kombe la Shirikisho CAF kwa kuwachapa wababe wa Algeria, JS Kabylie, na ilitwaa Super cup mwaka 2019.
Je ikiwa watashiriki African Super League kutarejesha mafanikio yao kwenye soka kama kipindi cha mwaka 1997 na 2004?
SC ZAMALEK (Misri)
Wababe wa soka Afrika, hilo halina mashaka kabisa, lakini Zamalek haijashinda taji laLigi ya Mabingwa Afrika tangu wachukue lile la mwaka 2002. Hata hivyo mwaka 2009 walishinda Kombe la Shirikisho, na baadaye wakafanikiwa kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa. Na sasa wanaweza kung’arisha nyota yao kwenye African Super League.
MAMELODI SUNDOWNS (Afrika kusini)
Hii ni miamba ya soka kusini mwa bara la Afrika na mshindani mahiri katika bara zima. Mamelodi wanatamba kwenye Ligi Kuu Afrika kusini lakini ipo dhana kwamba timu hii bado inatafuta ubabe wa soka katika mashindano ya Afrika kwa ujumla tangu kuondokewa na kocha wao Pitso Mosimane.
Msimu uliopita 2020/2021 walitolewa katika hatua ya nusu fainali na waliokuja kuwa mabingwa Al Ahly. Mamelodi Sundowns wamewahi kutwaa taji la Ligi ya mabingwa Afrika mwaka 2016. Michuano ya African Super League itakuwa sehemu yao ya kutangaza umwamba katika kandanda.
TP MAZEMBE (DRC)
Washindi waliotoweka ghafla kwenye anga za soka la Afrika. Kwa mujibu wa shirikisho la Soka Afrika, CAF linasema TP Mazembe ni klabu iliyocheza fainali 10 za CAF katika kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi 2018.
Tangu walipopata mafanikio hayo wakiwa na nyota wao Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu raia wa Tanzania hawajawahi kurudia tena kilele cha mafanikio hayo, lakini wamebaki kuwa klabu tishio katika soka la Afrika.
RS BERKANE (Algeria)
Nyota mpya, klabu mpya inayong’ara katika soka barani Afrika kwa sasa. RS Berkane msimu uliopita walitwaa Kombe la Shirikisho wakiwa wamenufaishwa na uwekezaji na usajili mzuri klabuni hapo. Ujio kocha Florent Ibenge kutoka klabu ya AS Vita ya DRC kumeongeza uimara na ushindani. Ni timu ya kuchungwa endapo itashiriki kwenye
African Super League.
HOROYA (Guinea)
Huenda ikawa timu inayoshangaza kutajwa kwenye mashindano ya African Super League. Horoya hawajawahi kufika fainali yoyote ya mashindano ya CAF tangu walipofanya hivyo mwaka 1978. Miamba hiyo kutona Guinea walitolewa kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.
ETOILE DU SAHEL (Tunisia)
Miamba ya soka ya Tunisia ambayo haina taji lolote la Afrika tangu walipotwaa Ligi ya Mabingwa mwaka 2007, lakini walitwaa pia Kombe la Shirikisho mwaka 2015. Ni klabu inayojumuishwa kwenye mashindano ya African Super League.
PYRAMIDS (Misri)
Ikiwa imeanzishwa miaka michache iliyopita na kupata uwekezaji mkubwa, Pyramids wameonesha kuwa wanaweza kumsajili mchezaji kwa gharaa yoyote na kuwa tishio katika soka barani Afrika. Mwaka 2020 walifungwa katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho CAF.
JS KAYBLIE (Algeria)
Walifungwa kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita, lakini kizazi cha dhahabu cha klabu hiyo kimeendelea kutoa matumaini kuwa kinaweza kufanya mambo makubwa zaidi kwani kushiriki kwao fainali tatu mfululizo kwa misimu mitatu kumewapa uzoefu zaidi. hawa ni mabingwa Afrika mwaka 1981 na 1990.
AS VITA (DRC)
Washindi wa pili wa Ligi ya mabingwa Afrika mwaka 2014 na Kombe la shirikisho mwaka 2018. Hata hivyo msimu huu AS Vita wamempoteza kocha wao Florent Ibenge ambaye amehamia RS Berkane.
KAIZER CHIFES (Afrika kusini)
Walifungwa katika mchezo wa fainali msimu uliopita na Al Ahly. Ni mongoni mwa timu ambazo zinaweza kushiriki michuano ya African Super League lakini walikuwa na hali mbaya Ligi Kuu Afrika kusini.
SIMBA (Tanzania)
Katika ukanda wa Afrika mashariki Simba ndio wababe ambao wametajwa kuwa na sifa za kushiriki African Super League. Ni timu ambayo kwa miaka minne imewakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
Comments
Loading…