in , ,

Simba inacheza kibingwa

Kuna mengi yamebadilika sana tangu mwalimu Pierre Lenchantre na
Masoud Djuma walipoichukua timu. Wengi wanaweza wakaona mabadiliko ya
kimfumo peke yake kutoka timu kucheza 4-4-2 mpaka 3-5-2

Hiki ndicho kitu kinachoonekana kwa nje, lakini kwa ndani kuna vitu
vingi sana ambavyo vinaonekana na vinadhihirisha kuwa kwa sasa Simba
inacheza kibingwa.

Baada ya Simba kutolewa na Al-Masry tulitegemea timu ingepoteza
uelekeo kwa sababu ya kutoka kwenye mashindano makubwa.

Mashindano ambayo walikuwa wanayaota kila siku baada ya kukaa misimu
minne bila kucheza mashindano haya, walikuwa wameyakumbuka katika
kiwango cha hali ya juu kuanzia kwa mashabiki, viongozi mpaka
wachezaji.

Shauku ya kufika mbali ilikuwa kubwa, siku ya mechi ya Al-Masry katika
uwanja wa Taifa , Dar-es-Salaam ilijidhihirisha hilo. Mashabiki
walikuja wengi kuishabikia timu yao.

Muda mwingi walikuwa wakipiga hamasa ya kuwataka vijana wao wapigane
bila kuchoka, wachezaji walipigana, miguu yao ilikuwa na shauku ya
kuwa na mpira kila muda. Matokeo ya sare ya 2- 2 hayakuwa matokeo
yaliwakatisha tamaa.

Walipanda ndege wakiamini kabisa wanaenda kufanya vizuri nchini Misri,
nia ya kufanya vizuri ilionekana uwanjani ,matokeo ya bila kufungana
yaliwafanya watolewe kwenye michuano hii.

Michuano ambayo walikuwa na hamu nayo, kama tunavyojua kwa timu zetu
kubwa hapa nchini zinapotolewa katika mashindano ndicho huwa chanzo
cha migogoro ndani ya klabu.

Migogoro ambayo husababisha mwenendo wa timu kuwa mbovu kwenye ligi
kuu, mara hii ikawa tofauti, utulivu ulitawala ndani ya timu na
wachezaji waliandaliwa dhifa ya mchana wakapata chakula cha pamoja na
wachezaji kupongezwa kwa jitihada walizozionesha.

Hii ilionesha kuna mshikamano mkubwa ndani ya timu na klabu kwa
ujumla, hata Yanga ilipofanikiwa kufikia alama za Simba na kulingana
nao wengi walitegemea Simba itakuwa na presha kubwa kuwaona wapinzani
wao wakiwa wamewakaribia.

Yalitokea msimu uliopita wengi wakaona yanaweza kutokea tena msimu
huu, lakini ikawa tofauti presha hawakuruhusu iwe ndani yao. Akili ,
nguvu waliziweka kwenye kila mechi walizokuwa wanacheza hawakufikiria
tena kuhusu Yanga aliyekuwa karibu yake.

Alikimbia huku akijiangalia yeye ni wapi alipokuwa anaelekea
hakuruhusu kabisa kutazama alikotoka kuona ni wapi alipo mpinzani
wake.

Utulivu ukawa mkubwa ndani ya timu, hata aina ya kucheza mechi husika
kukawa kuna badilika kila baada ya mchezo.

Baada ya kufunga goli la kwanza dhidi ya Njombe Mji walianza kulinda
goli lao. Hawakuona haja ya wao kuendelea kufunguka kutafuta magoli
mengi, wameshajua kabisa kipindi hiki ligi ilipo ni kipindi ambacho
timu inahitaji ubinngwa na siyo magoli mengi.

Hiki kitu hata kwenye mechi ya leo dhidi ya Tanzania Prisons
kilionekana, baada ya kupata goli walionekana kuwa imara kulilinda
goli lao na hata walipofunga goli la pili ilitosha kuwaonesha kuwa
wameshapata alama muhimu kwa ajili ya ubingwa.

Mzunguko wa kwanza timu ilikuwa inashinda magoli mengi, kipindi hiki
timu ilikuwa lazima ifunguke kwa ajili ya kupata ushindi mnene kwa
akiba nzuri kwa tahadhari kama iliyotokea msimu jana.

Hata mzunguko huu wa pili,viungo wa kati wanaotumika ni wale ambao
wanauwezo wa kushambulia na kukaba kwa pamoja (Shomari Kapombe na
Asante Kwasi aliyetumika mechi ya leo dhidi ya Tanzania Prisons).

Hii ni kuiwezesha timu iwe na uwiano mzuri eneo la katikati mwa uwanja
(wakati wa kukaba na wakati wa kushambulia).

Hiki kilionesha kuwanufaisha Simba kwa sababu wakati timu ilipokuwa
inashambulia viungo hawa walikuwa wnahusika katika kujenga
mashambulizi,na timu ilipokuwa inashambuliwa walisimama imara kukaba
(hii inaonesha timu inacheza kwa tahadhari bila kujali wanakutana na
mpinzani wa aina gani , kila mpinzani walimheshimu) na hii ndiyo sifa
ya timu bingwa (kumheshimu kila aina ya mpinzani).

Heshima hii imeanzia kwa mashabiki wao ambao wanaonekana kuwa pamoja
na benchi la ufundi, viongozi na wachezaji.

Viongozi pia wako kwa ajili ya wachezaji muda mwingi. Mshikamano huu
ni tasafri tosha kuwa Simba inaendeshwa kibingwa.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

JANA MLIMTEGEMEA MANJI, LEO MTENGENEZENI MANJI WENU

Tanzania Sports

WENGER NI LAZIMA AENDE ILI ARSENAL WAWE WASHINDANI WA KWELI