Jana michuano mipya ya Simba Super Cup ilimalizika katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam. Michuano ambayo ilishuhudia Simba SC wakiwa mabingwa wa kwanza wa michuano hiyo.
Pamoja na zawadi ya bingwa wa michuano hiyo pia kulikuwepo na zawadi mbalimbali kwa wachezaji ambao walifanikiwa kufanya vizuri kwenye michuano hiyo iliyoshirikisha timu tatu ambazo ni Simba SC, Al Hilal na TP Mazembe.
Zawadi zilizotolewa kwa ajili ya wachezaji waliofanya vizuri kwenye michuano hiyo asilimia 100 ya zawadi zote zimeenda kwa wachezaji wa Simba SC, hii inaonesha namna ambavyo Simba SC ilikuwa imara kwenye michuano hii.
Mchezaji bora wa michuano hii ni Lary Bwalya kiungo mchezaji wa klabu ya Simba SC. Mfungaji bora wa michuano hii ni Bernard Morrison ambaye amefunga magoli mawili (2) kwenye michuano hii, mlinda mlango bora wa michuano hii ni Beno Kakolanya ambaye ni mlinda mlango wa Simba SC.
Michuano imeshamalizika tayari lakini hoja kubwa ambayo inazungumzwa kwa sasa ni kama Simba SC kaingiza faida au hasara kwenye michuano hii? Hoja ya mjadala huu inajikita kwenye mapato ambayo Simba Sc kayapata kwenye michuano hii.
Mimi sitaki kujikita huko kwa sababu wigo wa faida ya michuano hii ni mpana sana na tunatakiwa kuutazama kwa upana kabla hatujaja na kauli au hitimisho la Simba SC kupata hasara kwenye michuano hii.
Ndani ya wiki moja iliyopita Simba SC imekuwa na mikutano na waandishi wa habari mitano, kwa kifupi ndani ya siku saba, Simba SC imefanya mikutano mitano na waandishi wa habari.
Hii faida yake ni ipi? Simba SC wameripotiwa mara nyingi ndani ya wiki moja iliyopita. Kuripotiwa mara nyingi na vyombo mbalimbali vya habari kunatoa nafasi kubwa kwa jina la Simba SC kuongelewa sana, kusikika sana kwenye masikio ya watu wengi.
Chapa ya Simba SC ndani ya wiki moja iliyopita imezungumzwa sana kwa mazuri yanayotokana na mashindano haya. Chapa inapokuwa inazungumzwa sana kwa mazuri inakuwa imara sana.
Ndani ya wiki moja ya mashindano haya sura ya chapa ya Simba SC imekuwa imara sana kutokana na kuzungumziwa na kuripotiwa mara nyingi sana tena kwa mazuri.
Hiyo ndiyo ilikuwa faida ya kwanza waliyopata Simba SC. Sura ya chapa yao imekuwa nzuri ni rahisi kwa mdhamini kuja kuwekeza pesa kwa Simba SC kwa sababu ya wao kujitengenezea mazingira ya kuonekana ni chapa imara ambayo inaweza kuwa biashara kubwa au nembo ya kutangaza biashara ya mtu yoyote.
Faida ya pili ambayo Simba SC imepata kutokana na michuano hii ni kuwapa nafasi kubwa wadhamini wao kujitangaza, kuonekana na kuongeza mauzo kwenye michuano hii.
Kama ambavyo nimetoka kusema huko juu, Simba SC walikuwa na mikutano mitano na waandishi wa habari ndani ya wiki moja. Mikutano hii ilikuwa na bango ambalo lilikuwa lina nembo ya wadhamini wa Simba SC.
Nembo ambayo imewafanya wadhamini wa Simba SC kuonekana mara nyingi sana. Kuonekana kwao mara nyingi kutawapa nafasi ya kuongeza mauzo kutokana na michuano hii.
Hii inaweza kuvutia wadhamini wengine walionje ya Simba SC kutamani kuingia kuwekeza ndani ya Simba SC kwa kuamini kuwa watapata nafasi ya kuonekana na kuongeza mauzo kutokana na ubunifu wa Simba SC.
Simba SC imewaalika wageni ambao ni wakubwa barani Afrika. TP Mazembe na Al Hilal ni timu kubwa barani Afrika. Hii imeongeza mahusiano mazuri na uaminifu kwa watu wengine.
Simba Sc imejiongezea mahusiano mazuri na vilabu hivi, pia imejiongezea nafasi ya kupata kuaminika kwa vilabu vingine. Kwa Simba SC itakuwa rahisi kuzialika timu zingine kwa sasa kwa sababu hizo timu zitaona kuwa Simba SC walifanikiwa kuwaalika watu wakubwa na wakafanikiwa , hii ni faida nyingine waliyopata Simba SC.
Simba SC inashiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika wakiwa katika hatua ya makundi. Kuwapata TP Mazembe na Al Hilal na kucheza nao ni nafasi kubwa ya wao kupata faida kubwa kiufundi. Kwa hiyo Simba Sc wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kiufundi kwenye timu yao kupitia michuano hii.
Michuano hii ilikuwa na faida kubwa nyingi kuliko hasara chache ambazo wengi wanazitama sana. Simba Sc wamefanikiwa kushirikiana na chapa kubwa (mwanamuziki) Zuchu ambaye na yeye atakuwa amewaongezea mashabiki Simba SC kupitia michuano hii.
Comments
Loading…