in

Simba bingwa katika fainali ya kikatili

Yanga Vs Simba

MABINGWA wa Ligi kuu Tanzania Bara, Simba wamefanikiwa kutwaa Kombe la Shirikisho baada ya kuwachapa watani wao wa jadi Yanga kwa bao 1-0 lililofungwa na kiungo mkabaji Taddeo Lwanga kwenye uwanja wa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma. Bao hilo lilipatikana baada ya kona nzuri iliyochongwa na Luis Miquissone katika kipindi cha pili cha mchezo huo na kuwa la kwanza kwa nyota huyo raia wa Uganda kuipa ubingwa Simba.

Fainali hiyo ilitawaliwa na rafu nyingi, ambapo Yanga walicheza faulo 22 wakati Simba walifanya madhambi mara 17. Katika mchezo huo uliojaa presha kubwa, mwamuzi Ahmed Aragija aliwanyima penalti Simba baada ya nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto kumchezea madhambi winga wa Simba, Luis Miquissone katika eneo la hatari.

Licha ya kuanza mchezo kwa presha kubwa, lakini mwamuzi wa mchezo huo taratibu alifanikiwa kutuliza akili yake na kuziamua vizuri timu hizo. Aragija ambaye alilaumiwa katika mchezo wa nusu fainali uliyochezwa mjini Songea ambapo aliruhusu Simba kupiga mpira wa faulo uliopigwa haraka na Bernard Morrison kabla ya wachezaji wa Azam hawajajipanga na Miquissone kutumbiza wavuni.

Hata hivyo uzoefu unaonesha uamuzi wake ulikuwa sahihi kwa sababu matukio ya namna hiyo yametokea katika nchi mbalimbali bartani Ulaya husuani kwa mshambuliaji wa zamani wa Arsenal Thiery Henry na beki wa Real Madrid Nacho Hernandez waliopachika mabao kwa staili hiyo, huku Azam wakilaumiwa kwa kushindwa kudhibiti mbinu za Simba kwa kuzuia mpigaji wa faulo hiyo wakati wakijiandaa kujipanga.

Kwa ushindi wa kombe la Shirikisho, Simba wamechukua mataji mawili msimu huu baada ya kutangulia kuchukua Ligi Kuu Tanzania bara, ambalo walikuwa wanalitetea.

Yanga ilicheza kwa sehemu kubwa ya mchezo huo baada ya kiungo wake mkabaji Tonombe Mukoko kutolewa nje kwa kadi nyekundu kipindi cha kwanza kwa kosa la kumpiga kiwiko nahodha wa Simba, John Bocco.

Ukatili mwingine katika mchezo wa fainali ya Azam Federation ni kushuhudia klabu ya Yanga ikimaliza msimu wa nne pasipo kuchukua taji la Ligi Kuu

Ushindani wa mechi hiyo na kumkosa Mukoko ulikuwa ukatili ambao Yanga walitakiwa kumudu kukabiliana na kasi ya Simba ambao hawakuwa wakicheza soka lao lililozoeleka na walikuwa wanapiga pasi ndefu ndani ya eneo la 18 ili washambuliaji  wao John Bocco na Chris Mugalu wagombanie na mabeki wa Yanga.

Kushindwa kwa timu hizo kucheza soka safi kulichangiwa na ubovu wa uwanja (pitch) ambapo zote hazikuwa na uwezo wa kupiga pasi 5 mfululizo. Uwezo wa wachezaji kumiliki mpira ulikuwa hafifu kwa sababu uwanja ulishindwa kuwapa kile walichokitaka hivyo kushindwa kukata kiu ya mashabiki wengi waliojazana uwanjani hapo.

Uwanja wa Ziwa Tanganyika umetajwa kuwa mbovu kuliko yote msimu huu kutokana na wachezaji kushindwa kuonesha ubora wao sababu ya ubovu wa uwanja.

Uwanja huo ulichaguliwa mwanzoni mwa msimu huu kutumika katika mchezo wa fainali ya kombe la Azam Federarion Cup, baada ya michezo ya nusu fainali kuchezwa katika viwanja vya CCM Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma, na li Hassan Mwinyi mkoani Tabora.

Tanzaniasports imezungumza na wadau mbalimbali wa soka ambao wamekiri kuwa mchezo wa fainali ulipaswa kuchezwa kwenye uwanja wenye hadhi ya kuoneshwa kimataifa kuliko wa Ziwa Tanganyika ambao uko chini ya viwango.

“Ilikuwa mechi mbovu kabisa tumenyimwa ladha kabumbu. Uwanja unahatarisha usalama wa wachezaji. Timu hazikucheza kupiga pasi 10 mfululizo. Ni aibu kumiliki uwanja wa namna hiyo na fedheha mno kwa sababu mechi hizi zinaangaliwa na mamilioni ya washabiki duniani” amesema mmoja wa viongozi wa chama tawala kwa sharti la kutotajw ajina.

“Mashabiki wa Kigoma wamepelekewa fainali, ni jambo zuri, lakini wanahitaji kushinikiza wawe na uwanja wenye viwango. Licha ya uwekezaji kwenye mashindano haya, inabidi mabadiliko yafanyike. Robo fainali na nusu fainali zifanyike viwanja vizuri, hata Lake Tanganyika ukitengenezwa, ila mchezo wa fainali unatakiwa kuchezwa kwenye uwanja wenye hadhi bila kujali ni Yanga,Simba,Azam au Mtibwa.”

Ukatili mwingine katika mchezo wa fainali ya Azam Federation ni kushuhudia klabu ya Yanga ikimaliza msimu wa nne pasipo kuchukua taji la Ligi Kuu, pamoja na kulikosa kombe la shirikisho yote mbele ya watani wake wa jadi. Kwa miaka minne hiyo Yanga wamefanikiwa kutwaa kombe la Mapinduzi lililofanyika visiwani Zanzibar kwa kuwafunga Simba kwa mikwaju ya penalti .

KITUKO NA HISIA ZA MASHABIKI

Tanzania Sports
Yanga na Simba

Katikati ya Manispaa ya Morogoro nikiwa na nimeambatana na askari wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania tulishuhudia zogo na nyimbo mbalimbali barabarani ambapo mashabiki wa Simba walikuwa wanashangilia ushindi wa timu yao.

Askari huyo akiwa amevalia sare za kazi aliamuru tusimame ili kuhakikisha hali ya usalama. Kitu ambacho mimi na askari huyo hatukujua ni mashabiki hao kumbeba shabiki wa Yanga kwenye mkokoteni na kuendesha huku na huko wakikimbia na kuimba nyimbo za kujisigu na ushindi wa Simba.

Askari huyo alilazimika kuachana na wasiwasi wake baada ya kugundua kuwa mashabiki walikuwa wameamua wenyewe na ilikuwa furaha yao ya ushindi kwa Simba pamoja na kumtania shabiki wa Yanga aliyeridhia kupakizwa ndani ya Mkokoteni huku kavalia jezi ya timu yake na barakoa mdomoni. Ilisisimua mno.

Report

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Giorginio Chiellini

Kompyuta zinawabeba wachezaji ‘wahuni’ na wazee

Tanzania Sports

Using trained Gymnasts to entertain politicians won’t win Tanzania Olympic Glory