Tuanze pale tulipo ishia, huu ndio msemo unaosambaa katika mitandao ya kijamii ya wapenda soka wa Tanzania Bara kwa kipindi hiki ambacho ligi inatarajiwa kurejea kuanzia Juni mosi katika kituo cha mkoa wa Dar es Salaam pekee.
Kurejea kwa ligi kunaweza kuwa na maana kubwa sana hasa kwa wale waliokuwa na mazonge juu ya kukabidhi ubingwa, Simba ambayo inaongoza ligi hiyo kwa zaidi ya alama 17 kwa anayefuatia Azam FC.
Mjadala ulikuwa je apewe Simba ambaye ina alama nyingi au ifutwe ili ianze upya, msuguano ulikuwa mkubwa sana na hatimaye jibu likapatikana ligi irejee na bingwa apatikane kama kanuni inavyosema kuwa aliyekuwa na alama nyingi mwisho wa msimu ndio atakuwa bingwa.
Tujikumbushe kabla hatujaenda mbali zaidi kuangalia wachezaji waliosaidia sana timu zilizo katika tatu bora.
Simba SC inaongoza katika msimamo ikiwa na alama 71 imecheza michezo 28 huku ikiwa na magoli 63 ya kufunga wakati ikiruhusu kutikiswa nyavu zao mara 15.
Katika michezo hiyo Simba imepoteza 3 imetoa sare 2 na imeshinda michezo 23.
‘Wanarambaramba’ Azam FC ambao wapo nafasi ya pili wamekusanya alama 54 kwa michezo 28, imefungwa magoli 20 na imefunga magoli 37, imepoteza michezo sita na imetoa sare 6 huku imeshinda michezo 16.
Yanga ambayo ina alama 51 ipo nafasi ya tatu, kwa michezo 27, imefunga magoli 31 na kufungwa 20 huku imeshinda michezo 14,sare 9 na imepoteza michezo 4.
Hiki sasa kikosi bora cha miamba hiyo mitatu ambayo kwa sasa ndio yenye nguvu zaidi katika ligi kuu ya Tanzania bara.
Katika kikosi hiki Aishi Manula wa Simba anaingia katika kikosi kama goli kipa namba moja kwani amefanya vizuri kwa dakika 1890 amepata ‘clean sheets’ 14 , japo Mnata wa Yanga naye amefanya vizuri ila bado Manula amefanya vizuri zaidi.
Upande wa kulia anasimama Juma Abdul kutoka Yanga, inatakiwa uwe na roho ngumu kidogo kumuacha nje Shomary Kapombe ambaye msimu wake wa mwisho pale Azam alifunga magoli 7 huku akisaidia mengine 6, msimu huu alianza kukaa nje kwa majeraha lakini kila anapopata nafasi anafanya vizuri. Juma Abdul amesadia kupatikana kwa magoli 4 dhidi ya mawili ya Kapombe hii ndio sababu tu ya kumuweka benchi.
Beki ya kushoto anasimama Mohamed Hussein beki wa Simba, wengi walijua kuwa ujio wa Gadiel Michael ungeathiri nafasi yake bado amecheza vizuri katika kiwango cha hali ya juu.
Yakubu Mohamed anasimama namba nne, beki kitasa wa Azam FC amefanya makubwa mno, anapocheza kila mmoja anaweza kuona ukubwa wake na nguvu anazozitumia huku akili zikiwa nyingi, amefanya vizuri msimu huu licha ya kutoka katika majeraha.
Namba tano anasimama Lamine Moro, hapa unaweza ukahoji juu ya Erasto Nyoni na Pascal Wawa, kilichompa nafasi ya kuanza katika kikosi hiki alicheza mechi nyingi kuliko hao wenzake.
Namba sita anasimama Jonas Mkude wa Simba, huyu bwana amejihakikishia nafasi ya kudumu ndani ya timu hiyo aliyekuwa anamsumbua na afikirie mara mbili alikuwa James Kotei lakini sasa hakuna wa kumuweka benchi labda awe majeruhi, aliisaidia Simba kufika hapo ilipo.
Upande wa kulia kwa maana namba saba anasimama Mzimbabwe Never Tigere wa Azam FC huyu ni kiungo ila mfumo wetu utamfanya acheze zaidi kwa kuchezesha wachezaji watatu mbele, ameweza kusaidia timu yake hasa katika mechi za mwisho na nathubutu kusema kuwa ameisaida timu yake kufika hapo.
Namba nane anacheza Papy Tshishimbi wa Yanga, huyu mtu ana mapafu ya mbwa anaweza kuzunguka kila sehemu ya uwanja huenda ndio kiungo bora hadi kusimama kwa ligi, nimemsogeza mbele atakuwa anasaidiana na Mkude.
Mnyarwanda Meddie Kagere atasimama katika safu ya ushambuliaji, yeye ndiye kachangia magoli mengi Simba kwani amefunga magoli 19 na ametoa pasi za msaada 6 hivyo magoli 25 ya timu hiyo katika magoli 63 ya Simba.
Dimba la mbele anasimama Salum Aboubary wa Azam nyota ambaye wakati mwingine anaamua matokeo ya ‘Wanarambaramba’ amekuwa akifanya vizuri akifunga na kutoa pasi za mwisho.
Bernard Morrison wa Yanga anakaa upande wa kushoto huyu muuaji wa Simba katika mchezo wao wa mwisho amecheza vizuri amefunga magoli 3 na kutoa msaada magoli matatu ameonesha kiwango kikubwa ambacho hakijawahi kuonekana kwa kipindi kidogo katika soka la Tanzania.
Kocha wa timu hii ni Sven Vandenbroeck wa Simba akisaidiana na Luc Eymael wa Yanga
Yaani iko hivi:-
1.Aishi Manula, 2.Juma Abdul, 3.Mohamed Hussein, 4.Yakubu Mohamed, 5.Lamine Moro, 6.Jonas Mkude, 7.Never Tigere, 8. Pappy Tshishimbi, 9.Meddie Kagere, 10.Salum Aboubakari na 11.Benard Morrison.
Comments
Loading…