Hatimaye βwataalamuβ wa Ligi ya Europa β Sevilla wamenyuanyua kombe la ligi hiyo kwa mara ya sita, wakiwakata kilimilimi Inter Milan wa mwalimu Antonio Conte.
Walichukua ubingwa huo wa ligi ndogo ya Ulaya baada ya ushindi wa 3-2 kwenye mechi iliyokuwa ya kuvutia mno.
Mshambuliaji wa Sevilla, Luuk de Jong, akasema kwamba mafankio hayo yamewafika kutokana na kuishi na kucheza pamoja kama familia moja. Conte alikuwa amesema awali kwamba timu yake ilikuwa na tamaa sana ya kutwaa kikombe hicho, lakini bahati haikuwa ya Internazionale.
Mchezaji huyo wa zamani wa Newcastle wa Uingereza na Borussia MΓΆnchengladbach wa Ujerumani, amekuwa shujaa, kwani ndiye aliyefunga bao la ushindi dhidi ya Manchester United na kuwatupa nje ya mashindano wakati wa nusu fainali. Safari hii alifunga mabao mawili kwenye ushindi wa mechi iliyochezwa Cologne, Ujerumani
βImekuwa raha kubwa sana; tumekuwa na mechi ngumu kwa kweli wakati wote wa michuano hii, lakini tukacheza vizuri sana kama timu. Ungeweza kuona wazi wakati wote kwamba kwa hakika tulikuwa kama timu.
βTulifanya kazi pamoja na haikujalisha tulikuwa tunakabiliana na nani kwenye mechi zile, haikujalisha nani alishuka uwanjani, kila mmoja anafanya kazi kwa ajili ya kuunga mkono mwenzake na ilionekana wazi pia hata kwenye hatua hii ya mwisho katika gemu ya fainali.
βIlikuwa ngumu. Tulianza vyema lakini kukiwa hakuna jitihada kubwa wala chochote wakafunga bao kwa sababu ya penati. Lakini nilikuja kuweza kufunga mabao mawili kwa kichwa. Kwa hakika nina hisia ya aina yake na kwa bahati mwishoni tukashinda mechi,β anasema mchezaji huyo akiwa na kombe lao.
Conte akasema kwamba wiki ijayo wataamua juu ya hatima yake, akisema hana uhakika iwapo atakuwa kocha wa Inter msimu ujao na kwamba Inter watapanga mambo ya baadaye wakiwa naye au pasipo yeye. Akipita mbele ya kombe, Conte ambaye ni kocha wa zamani wa Chelsea, alivua medali ya ushindi wa pili, akidhihirisha kwamba hakufurahia matoke ohayo.
De Jong aliyefunga mabao manane tu msimu wote kabla ya fainali hiyo, aliingia akitokea benchi dhidi ya United, akawapa Sevilla ushindi, ndipo akajumuishwa kwenye kikosi cha kuanza dhidi ya Inter, akijengewa imani na kocha Julen Lopetegui, imani iliyolipa vyema.
De Jong alisawazisha bao la kwanza la Romelu Lukaku alilofunga kwa penati ya dakika ya tano tu, akipiga kichwa kana kwamba anapiga mbizi, kisha akafunga kwa mpira mkali wa kichwa kufuatia mpira wa adhabu ndogo wa Ever Banega na kufanya waongoze 2-1. Diego Godin alisawazisha, lakini likawa bao la kujifunga la Lukaku lililowapa Sevilla ubingwa.
Akieleza jinsi alivyopewa Habari kwamba angecheza mechi hiyo kwa kuanzia kikosi cha awali, De Jong anasema: βAliniambia (Lopetegui). Lakini mie nikamwambia β kama nilivyomwambia kwa mechi zile nyingine β kwamba nipo tayari wakati wote anaponihitaji, na leo (jana), kwa hakika mambo yakawa mazuri hasa kwangu na kwa klabu.
βNadhani huu ni utaaalamu wangu. Bao la kwanza kutokana na majalo ya Jesus Navas lilikuwa kamilifu, nililenga posti ya karibu, na kweli mpira ukazama ndani, kisha likaja lile la pili, majalo nzuri mno ya Banega na mipira hii ya vichwa kwa kweli ni mizuri ukiweza kuitumbukiza kwenye posti ya mbeli, ukazama ndani kikamilifu.β
Lopetegui alifukuzwa kazi ya ukocha wa Timu ya Taifa ya Hispania β La Furia Roja β kabla tu ya fainali za Kombe la Dunia, baada ya kutangaza kujiunga na Real Madrid ambako pia alifukuzwa baadaye kutokana na ufanisi mdogo wa timu, akachukuliwa na Sevilla.
Anaeleza kufurahishwa na kuwaongoza Sevilla kuchukua kombe hilo, likiwa ni la kwanza tangu ashike hatamu hapo Sevilla. βNi jambo la aina yake kutwaa kombe, na kwangu nasema hii ni kwa ajili ya klabu, kwa ajili ya washabiki, maalumu sana. Tunafurahi sana kwa sababu tumepambana vikali hasa katika emchi ngumu lakini tukamalizia kwa raha.β
Akizungumzia mchango wa De Jong, kocha huyu anasema kwamba huyo ni mchezaji mzuri sana na kwamba alikuwa akisubiri wakati kama huo na akawasili na kufanya yake kwa muda mwafaka.
Comments
Loading…