Sevilla wamekuwa klabu ya kwanza kutwaa ubingwa wa Ligi ya Europa mara nne katika historia ya soka.
Wahispania hao walitwaa kombe baada ya kwuazidi nguvu Dnipro kwa mabao 3-2 kwenye mechi waliyotawala kwa asilimia 62.
Carlos Bacca wa Sevilla alifunga mabao mawili na kufikisha jumla ya mabao saba kwenye michuano hiyo na sasa Sevilla wamefuzu moja kwa moja kwa hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) mfumo unaoanza rasmi wakati huu.
Ilikuwa mechi kali na ya kuvutia jijini Warsaw, Poland Jumatano hii ambapo Wahispania walianza kufungwa kwa bao la Nikola Kalinic aliyewapa wananchi wa Ukraine matumaini kwamba timu yao ingeweza kutwaa ubingwa huo.
Hata hivyo, Sevilla ambao tangu awali walionesha dhamira ya kuchukulia kwa umakini mkubwa mashindano haya, walijibu mapigo kwa mabao mawili ya haraka, moja liitiwa kimiani na Grzegorz Krychowiak kabla ya Bacca kumzunguka kipa na kucheka na nyavu.
Bao la pili la Waukraine lilifungwa kwa mpira wa adhabu ndogo na Ruslan Rotan kwa umahiri mkubwa dakika moja kabla ya mapumziko. Bacca aliwahakikishia ubingwa Sevilla alipofunga dakika ya 73 na jitihada za wapinzani kwa muda uliobaki hazikufua dafu.
Kocha wa Sevilla, Unai Emery alisema walikuwa na kazi ngumu kufika hatua hiyo, ikiwa ni pamoja na changamoto nyingi walizofanikiwa kuzivuka ili kupata tuzo hii muhimu. Alisema mechi ya mwisho ilikuwa ngumu sana.