in , ,

Mgogoro wa Fifa: Blatter akomaa

*Platini amzodoa akimtaka ang’oke

Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter amekataa katakata kuachia ngazi, anaendelea kuongoza vikao na atasimama kutetea kiti chake Ijumaa hii.

Baada ya kashfa ya kihistoria kuikumba Fifa kwa wajumbe wake saba kukamatwa jijini Zurich kwa ajili ya kufunguliwa mashitaka ya jinai kuhusiana na rushwa na utakatishaji fedha, baadhi ya watu maarufu walitaka kuona Blatter akiondoka.

Wakati baadhi walitaka uchaguzi uahirishwe, Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini alitoa mwito kwa Blatter kuachia ngazi na kuachana na mpango wake wa kuwania uongozi kwani ‘ananuka’ akiwa mkuu wa shirikisho husika.

Platini amesema aliamua kumwambia ukweli na kwa uwazi Blatter kwamba anatakiwa kuondoka Fifa, kwa vile yeye Blatter husema ni mjomba wake, hivyo asipomwambia hakuna atakayefanya hivyo.

“Tumekuwa marafiki wakubwa sana na Blatter – siku zote amekuwa akisema yeye ni mjomba kwangu hivyo nisipomwambia ukweli hakuna atakayefanya hivyo. Anasema kwamba ingekuwa ni siku au wiki kadhaa zilizopita huenda ingewezekana kung’oka lakini kwa sasa anasema tumechelewa mno.

“Namwona (Blatter) kuwa ni rafiki aliye kwenye tatizo na ni jukumu langu kulweleza hilo. Natumaini kwamba rafiki zangu nao siku moja wataniambia; ‘Michel, wakati wako wa kuondoka umewadia’ na natumaini kwamba nitafuata ushauri wao. Ikiwa Blatter anababi kuwa rais, Uefa tutakutana Berlin kujadili hatima ya uhusiano wetu na Fifa. Je, Uefa inaweza kujitoa Fifa? Bila shaka,” anasema Platini.

Blatter (79) anayetafuta muhula wa tano hakuonekana kuguswa na mambo yanayoendelea, bali alikuwa mwenyekiti wa vikao kadhaa vya maofisa wa juu wa Fifa, akisema kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa.

Alikutana na Platini faragha baada ya kutakiwa kuachia ngazi na haijulikani ni kipi walijadili na Ijumaa hii kivumbi kitakuwa kwenye sanduku la kura baina yake na Mwana wa Mfalme wa Oman, Ali bin al-Hussein.

Wakati watu wenye ushawishi mkubwa wakitaka kura isogezwe mbele, kuna baadhi wanataka iendelee kama kawaida, wakiona kwamba tukio la kudakwa maofisa wa Fifa ni pigo la nguvu dhidi ya Blatter na hivyo uchaguzi huu ni fursa muhimu ya kumng’oa.

Uefa ilikuwa inafikiria kugomea uchaguzi huo kutokana na makandokando yanayotokea lakini Alhamisi hii imeamua kwamba itashiriki na kumuunga mkono Prince Ali. Kwa upande wake, Shirikisho la Soka la Afrika (Caf) limeamua kuendelea kumuunga mkono Blatter.

Licha ya matatizo yake, shirikisho jingine, lile la Asia nalo limeamua kumuunga mkono rais huyo mkongwe, japokuwa mmoja wa wanachama wake, Shirikisho la Soka la Australia limesema kwamba litampigia kura Prince Ali.

Fifa inayokabiliwa na tuhuma nyingi za kashfa, ikiwa ni pamoja na utoaji na upokeaji wa milungula wa maofisa wake, Jumatano hii ilitumbukia kwenye kashfa ya kina zaidi baada ya maofisa wa Marekani kuwashitaki maofisa 14, wakiwamo saba wa Fifa wakihusishwa na biashara chafu ya fedha na rushwa.

Maofisa hao wa Fifa walikamatwa alfajiri ya Jumatano kwenye hoteli waliyofikia jijini Zurich, ikiwa ni kwa maombi ya Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) ambalo limekuwa likiwachunguza maofisa wa Fifa kwa miaka mitatu iliyopita. Uswisi imesonga mbele na kuanza uchunguzi wake huru juu ya jinsi maombi na utoaji wa nafasi za uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2018 na 2022 vilivyofanyika.

Walionaswa na kufunguliwa mashitaka ni – Rafael Esquivel, Nicolas Leoz, Jeffrey Webb, Jack Warner, Eduardo Li, Eugenio Figueredo na Jose Maria Marin. Wanaelezwa kuhusika na pauni milioni 97 (shilingi za Tanzania karibu 198,850,000,000) isivyo halali.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Sevilla mabingwa Europa

Alexis Sanchez chaguo la washabiki