in , ,

SAJILI 10 BORA MPAKA SASA KWA YANGA, SIMBA NA AZAM.

10: RAZACK ABALORA.

Ungewaambia kipi mashabiki wa Azam wakuelewe kuhusu kuondokewa na kipa
wao bora, ambaye alijimirikisha lango la timu hiyo na kuwa kama sehemu
anayolala na kuamkia pale.

Hakukuwa na mtu yoyote ambaye angeweza kuja kumpora namba Aishi Manula
kipindi kile yupo Azam fc.

Alikuwa bora , na alijihakikishia namba mpaka timu ya taifa kwa sababu
ya ubora wake aliouonesha akiwa Azam Fc.

Kipa bora mara mbili mfululizo wa ligi kuu Tanzania bara ambaye ni Tanzania one.

Kuondoka kwake kulikuwa pigo kubwa sana kwa Azam fc, na wengi
hawakuona kwa haraka haraka ni nani ambaye angeweza kuja kuziba pengo
lake.

Lakini Razack Abalora amefanikiwa kwa kiasi kikubwa Azam fc wamsahau
Aishi Manula, hakuna makosa ambayo anayafanya na kulazimika Azam fc
wamkumbuke Aishi Manula.

9: BUSWITA

Usajili wake ulikuwa na mizengwe mingi sana, mizengwe ambayo
ilipelekea afungiwe mwaka mmoja kutocheza mpira na shirikisho la soka
Tanzania ( TFF).

TFF, ilimfungulia tena, ndipo kocha Lwandamina alipoamua kuanza
kumtumia kama ORTHODOX player.

Yani akawa anacheza akiingia katikati ya uwanja na karibu ya eneo la
kumi nane la mpinzani akitokea pembeni mwa uwanja.

Hachezi kama mshambuliaji halisi wa pembeni.

Hii imeisaidia sana Yanga kwani ,Buswita amefanikiwa kuleta uwiano
mzuri wa eneo la katikati mwa uwanja, hivo timu kuifanya iwe imara
zaidi katika eneo la katikati mwa uwanja. Amekuwa akiingia katikati ya
uwanja akitokea pembeni, hivo kuongeza idadi ya wachezaji eneo la
katikati kuwa watatu ( Tshishimbi, Raphael Daudi pamoja na yeye).

8: MBARAKA YUSUPH.

Msimu uliopita alifanikiwa vizuri sana akiwa na Kagera Sugar.

Kama ilivyokuwa kwa Buswita , huyu naye usajili wake wa kwenda Azam fc
haukuwa wa amani, hali iliyopelekea Azam fc na Kagera Sugar kukaa
chini na kutumia busara iliyomfanya Mbaraka achezee Azam fc.

Baada ya kuondoka John Bocco ambaye alikuwa mhimili wa Azam Fc kwa
miaka mingi, maswali mengi yalikuwa ni nani ambaye atakuja kuziba
pengo la John Bocco.

Pamoja na kwamba Mbaraka hafungi magoli mengi, ila anafunga magoli
muhimu ambayo yanaisaidia timu kupata alama ambazo mpaka sasa
zimewaweka nafasi za juu ambapo wanalingana alama na kinara wa ligi
kuu, ila tofaufi ya magoli ndiyo inawaweka chini ya kinara wa ligi
kuu.

7: BRUCE KANGWA

Eneo jingine ambalo Azam Fc lilikuwa linawaumiza kichwa, ni eneo la
beki wa kushoto.

Gadiel Michel aliondoka, kijana ambaye alidhibitisha ubora wake katika
jezi ya Azam FC lakini Yanga wakamchukua.

Lilionekana litakuja kuwa pengo kubwa sana, lakini imekuwa tofauti
sana baada ya Bruce Kangwa kuingizwa kwenye timu.

Amekuwa mzuri sana kwenye kukaba, pia amefanikiwa kuleta uwiano mzuri
wa kukaba na kushambulia kwenye timu katika upande wa kushoto wa Azam
FC.

6: GADIEL MICHEL.

Hapana shaka msimu uliopita kati ya eneo ambalo lilikuwa linavujisha
mashambulizi katika upande wa Yanga ni eneo la kushoto ambalo alikuwa
anacheza Haji Mwinyi.

Haji Mwishi ni beki ambaye uzuri wake utauona wakati timu ikiwa na
mpira, anashambulia vizuri sana. Lakini timu ikiwa haina mpira, ikiwa
inashambuliwa ni vigumu kuona umuhimu mkubwa wa Haji Mwinyi. Hivo
alikuwa mzuri zaidi katika jukumu la kushambulia.

Gadiel, amekuja kuleta uwiano mzuri katika eneo la kushoto mwa uwanja
ambapo timu inaposhambulia na yeye anashambulia vizuri, na timu
inaposhambuliwa yeye pia anahusika vizuri sana kwenye kukaba.

5: ERASTO NYONI.

Mpaka sasa ni top assist, akiwa amepiga pasi 6 za mwisho za magoli.

Amecheza nafasi mbili mpaka sasa, yani beki wa kushoto na beki wa
kulia, na nafasi zote amecheza katika kiwango kikubwa.

Amekuwa msaada mkubwa sana kwa Simba kipindi ambacho Mohamed Hussein
alipokuwa kwenye majeraha , yeye alisimama vizuri sana eneo la
Mohamedi Hussein.

Ndiyo mchezaji wa pili, nyuma ya Emmanuel Okwi aliyehusika moja kwa
moja kwenye magoli mengi ya Simba .

4: PAPY TSHISHIMBI.

Eneo ambalo lilikuwa ni eneo bovu kwa misimu kadhaa katika timu ya
Yanga. Ni eneo la kiungo wa kuzuia. Msimu jana walilazimika kumleta
Zullu lakini hakukidhi mahitaji ya timu.

Msimu huu wamemleta Tshishimbi, ambaye kwa kiasi kikubwa amefanikiwa
kukidhi mahitaji ya timu katika eneo la katikati.

Anauwezo mzuri wa kuzuia, pia anauwezo mkubwa wa kuanzisha
mashambulizi ya timu akitokea eneo la katikati mwa uwanja.

Ni moja ya mihimili mikubwa kwa sasa katika klabu ya Yanga.

3: AISHI MANULA.

Huyu analeta tafasri sahihi ya kipa ni mtu muhimu sana wa kuiweka hai
timu kwenye mchezo kwa dakika nyingi.

Amekuwa akiokoa michomo mingi ambayo huiweka Simba kwenye mchezo kwa muda mrefu.

Amekuwa akisimama imara pindi ambapo timu inapozidiwa na kuweza kuiokoa timu .

2: AJIB

Mpaka sasa amefunga nusu ya magoli ya Yanga, na kizuri zaidi amefunga
magoli ambayo ni muhimu kweye timu.

Mfano , mara nyingi Yanga imekuwa ikiibuka na ushindi wa goli 1-0 , na
katika ushindi huo Ajib amekuwa msaada kufunga goli ambalo linaipa
alama tatu muhimu timu yake.

1: OKWI

Alibezwa sana wakati anakuja, hoja kubwa ni kuwa amezeeka. Na hawezi
kuendana na kasi ya sasa ya mpira.

Kuna vitu vimepungua kwa Okwi, kama kasi yake uwanjani lakini kuna
kitu kimoja amekiboresha , nacho ni utulivu mkubwa wa kufunga .

Kasi yake imepungua kwa kiasi kikubwa, lakini uwezo wake wa kufunga
umeongezeka maradufu.

Mpaka sasa anaongoza magoli akiwa na goli 8.

Msimu jana Simba ilikuwa nafasi ya pili kwa kuzidiwa magoli tu baada
ya kulingana alama na Yanga.

Uwepo wa Okwi umepunguza uhaba wa magoli uliokuwepo msimu jana.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MANULA ALIWAWEKA HAI SIMBA, HUKU YANGA WAKIKOSA UMAKINI

Tanzania Sports

REFA ALIIVUNJA NGUVU ARSENAL, MOURINHO ALIJIMALIZA MWENYEWE.