Msimu mpya wa 2021/2022 wa Ligi Kuu Hispania maarufu kama La Liga ni mbichi mno. Timu zimecheza mechi chache hadi sasa. Real Madrid wameanza msimu huu wakiwa na kocha mpya, Carlo Ancelotti ambaye amechukua nafasi ya Zinedine Zidane. Mara baada ya kumalizika msimu uliopita Zidane alitangaza kujiuzulu.
Zinedine Zidane alijifunza ukocha chini ya Carlo Ancelotti. Mtaliano huyo alikuwa mtu anayependwa na Zidane. Makocha hawa wawili wana mambo yanayofanana mno katika utendaji wao wa kazi, lakini Ancelotti ameonesha tofauti kidogo tangu kuanza msimu huu na Real Madrid imekuwa timu ya tofauti pia.
Ni dhahiri Ancelotti ameongeza sababu nyingine inayomtofautisha na mwanafunzi wake. Hilo ni jambo la tofauti kuliko ilivyozoeleka huko nyuma kuwa watu hawa wanafanana mno katika utendaji wa kazi ingawa walitofautiana namna ya kuendesha mambo katika nyakati mbalimbali zikiwemo ngumu.
Hizi ndizo sababu tano zinazowatofautisha makocha hawa wawili wanaopendana na kupeana maarifa nyakati za nyuma.
KUMWAINI VINICIUS JUNIOR
Winga huyo raia wa Brazil hakuwa mchezaji wa kutumainiwa katika kikosi cha kwanza, ingawaje mara kadhaa alipewa nafasi hiyo lakini ni mchezaji aliyekosa kuaminiwa na Zidane. Lakini sasa chini ya Carlo Ancelotti hali ni tofauti kwani Vinicius amekuwa mchezaji wa tofauti katika kikosi cha Ancelotti.
Wakati nyota huyo mwenye umri wa miaka 21 akiwa likizo katika majira ya joto, Ancelotti alimpigia simu na kumfahaisha kuwa anakwenda kuwa mchezaji muhimu katika kikosi chake, na haijalishi kama Kylian Mbappe angekuja au la.
Vinicius sasa amelipa kwa imani aliyopewa na kocha huyo. Kwa sasa anaonekana anajiamini zaidi na kuwa mchezaji aliyekamilika na kuungwa mkono na makocha wake huku timu ikicheza kumzunguka yeye. lakini chini ya Zidane mchezaji huyo hakupewa majukumu makubwa na hata siku aliyopewa bado yalikuwa ya imani ya chini mno.
Wachezaji tofauti hupokea hamasa na ufundi kwa njia tofauti. Inaonekana sasa Carletto anafahamu namna ya kupata ubora wa Vinicius ambaye ameanza kuonekana kama nyota mpya klabuni hapo.
ZIDANE ALIJENGA ULINZI MKUBWA
Katika msimu wa mwisho wa Zidane, licha ya kumaliza mikono mitupu lakini kulikuwa na matokeo mazuri katika kikosi. Tangu mwezi Februari hadi Mei mwaka huu Real Madrid ilifungwa mchezo mmoja tu katika uwanja wa Stamford Bridge, sababu kubwa ilikuwa ni ulinzi mkubwa uliosukwa na kocha huyo licha ya kukumbana na majeruhi kadhaa yaliyoharibu mipango yake.
Ancelotti na Zidane wote wanapenda kuona timu zao zikishambulia wakati wote, lakini Mtaliano huyo ameongeza mambo mengine kwa kuhakikisha Real Madrid inakuwa imara katika safu ya ulinzi ndio maana amesisitiza umakini,ubora na uamuzi sahihi katika ukabaji.
Chini ya Zidane, Real Madrid haikuwa na ubora katika mipango ya kushambuliaji, lakini ilifungwa mabao machache. Ancelotti sasa anatumia mbinu za kudhibiti wapinzani kuanzia safu ya ulinzi, lakini amewapa maarifa washambuliaji na viungo wake uwezo wa kuwa hatari wakati wowote eneo la adui.
CARLETTO KUMREJESHA PINTUS
Zidane alikuwa kocha wa kwanza kumwajiri Antonio Pintus kuwa kocha wa viungo lakini uhusiano wao uliharibika kipindi alipojiuzulu mara baada ya kutwaa taji la Uefa Mei 2018. Baada ya mambo kuharibika na makocha wawili kufukuzwa, ilibidi Perez amrudishe Zidane. Naye Zidane aliporejea kwa mara ya pili Pintus aliondoka klabuni hapo.
Sasa Ancelotti amemrejesha Antonio Pintus katika nafasi yake na matokeo yameonekana hadi sasa. Real Madrid wana nguvu zaidi msimu huu, lakini pia matarajio ni kuona kiwango cha wachezaji kupata majeraha kinapunguzwa.
WACHEZAI CHIPUKIZI KUPEWA NAFASI KULIKO WAKONGWE
Mfaransa huyo alikuwa na maamuzi yaliyowaachia njia panda mabosi wake kuhusiana na matumizi ya wachezaji chipukizi, na hilo lilichangia mgongano wa sera baina ya pande hizo mbili. Zidane alipendelea kuwapanga wachezaji watiifu kwake ambao walionekana wakongwe hali ambayo iliwanyima nafasi chipukizi.
Ancelotti ameifanya timu hiyo iunganike zaidi kwani wachezaji chipukizi na wakongwe wote wanapewa nafasi sawa katika mechi. Na zaidi wachezaji chipukizi wamehakikishiwa nafasi ya kucheza katika mechi.
Kocha huyo amethibitisha kuwa Vini Jr na Fede Valverde watakuwa na majukumu makubwa msimu huu. Majukumu hayo pia yatamhusu nyota mpya aliyewasili msimu huu Eduardo Camavinga ambao wanatakiwa kuimarisha uwezo wa eneo la kiung.
Uamuzi wa Ancelotti kumtumia beki wa kushoto Miguel Gutierrez katika kikosi cha kwanza mbele ya Marcelo ni ushahidi wa tofauti ya makocha hao. pia Ancelotti amebainisha Eden Hazard sio mchezaji ambaye hagusiki tena, hivyo anatakiwa kuongeza kiwango ili ampatie nafasi kikosi cha kwanza.
SAKATA LA GARETH BALE
Zidane aliporejea kwa mara ya pili kuifundisha Real Madrid hakuficha kuwa hakumhitaji Gareth Bale katika kikosi chake. alifanya kila njia kuhakikisha staa huyo anaondoka klabuni hapo.
Ancelotti amempokea Bale msimu huu na amemuonesha kuwa yuko tayari kumpa nafasi ya kucheza kama wachezaji wengine, jambo ambalo awali halikuwepo kwa nyota huyo kutoka Wales. Kitu kinachomnyima nafasi kwa sasa ni majeraha aliyopata, lakini kocha yuko tayari kumpanga katika mechi.
Comments
Loading…