Cristiano Ronaldo amerudi kwenye kiwango chake baada ya kufunga bao muhimu na kumtengea Marcelo kufunga la pili katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) baina ya Real Madrid na Schalke.
Wadau walikuwa wakihoji utimamu wa Ronaldo na kiwango chake cha soka kabla ya mechi hiyo, lakini ameonesha bado yumo.
Kocha wake, Carlo Ancelotti alimsifu akisema nyota wake huyo huishi kwa mabao.
Real sasa wameshinda mechi 10 mfululizo za UCL huku Ronaldo akifikisha mabao 58 kwenye mechi 58. Alikuwa amecheza mechi tatu bila kufunga bao.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Gelsenkirchen, Ronaldo alifunga vyema baada ya kumiminiwa majalo na Dani Carvajal, akatengeneza la pili baada ya Schalke kukosa bao kwa shuti la Felix Platte kugonga mwamba.
Schalke wanaofundishwa na mchezaji na kocha wa zamani wa Chelsea, Roberto Di Matteo walimpoteza mchezaji wao hatari, Klaas-Jan Huntelaar aliyeumia kabla ya mapumziko, na kuwa pigo kubwa kwao.
Katika mechi nyingine, FC Basel na FC Porto wamekwenda sare ya 1-1.
Comments
Loading…