*Chelsea watwaa Kombe la Europa jioni
*Benfica wazungusha lakini si kufunga
Rafa Benitez amefunika ulimwengu wa soka tena, wiki hii kwa kutwaa Kombe la Europa akiwa na Chelsea, na ni tuzo kubwa kwake anapomaliza ukocha wake wa muda wa klabu hiyo.
Benitez aliyetamba Uingereza akiwa na Liverpool kwa mafanikio kabla ya kufifia na kuondoka, amekuwa hapendwi na washabiki wa Chelsea ambao wamekuwa wakimzomea na kumshikia mabango, lakini amekuwa daima akisema yeye anajikita kufundisha na kuwinda makombe.
Baada ya kutwaa makombe kadhaa na timu mbalimbali, wakati muda wake ukiyoyoma Chelsea, ambapo kocha mpya ataanza baada ya ligi kuu kumalizika, Benitez Jumatano hii amecheka na Kombe la Europa, baada ya Chelsea kuwafunga Benfica kutoka Ureno 2-1 katika fainali iliyopigwa nchini Amsterdam, Uholanzi.
Vijana wa Benfica, hata hivyo, waliwapelekesha Chelsea muda mwingi wa mchezo kwa kukitawala kiungo, kupiga chenga za maudhi na kuwafanya uchochoro hata mabeki hodari kama Ashley Cole na viungo Ramires na Lampard, lakini daima walikuwa wakipatwa kigugumizi cha miguu kwenye kutumbukiza mpira wavuni.
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, walishakosa mabao karibu matatu ya wazi kwa walivyoliendea lango la Chelsea taratibu na ama kuishia kunyang’anywa mpira hatia za mwisho au mashuti yao kuwa fyongo au kuwagonga Chelsea. Waliwatia tumbo joto hasa Chelsea, waliohitaji msasa wa kitaalamu kutoka kwa Benitez wakati wa mapumziko.
Hata hivyo, Fernando Torres aliyefufuliwa na Mhispania mwenzake, Benitez, alipachika bao zuri la kwanza baada ya kufanya kazi ya ziada kuwatoka mabeki, kumzunguka kipa na kuweka mpira kimiani. Hata hivyo, bao hilo lilirudishwa kwa mkwaju wa penati, baada ya Cesar Azpilicueta kuzuia mpira kwa wazi na makusudi katika eneo la penati.
Beki Branislav Ivanovic alionesha umuhimu wake tena Jumatano hii kwa kupachika bao kwa kichwa katika dakika za majeruhi, baada ya kona ambayo kama wachezaji wa Benfica wangekuwa makini kufagia mipira, wala haingepigwa. Wachezaji hao walikuwa macho na akina Torres na wengine, wakamwacha Ivanovic kujitwisha taratibu kichwa na kutikisa nyavu.
Chelsea walikuwa na bahati katika usiku huo, kwani Benfica walikuwa bora zaidi kwa wastani, na walikuwa na kila sababu ya kulia kwa kulala nyasini wakijutia nafasi walizopoteza, kwani ni mwaka wa 51 wanakosa kombe, ambapo kwa mwaka wa saba mfululizo wanashindwa kunyakua kombe kwenye fainali.
Benitez sasa ataondoka kwa amani, mbwembwe na tambo baada ya mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Everton Jumapili, bila kujali kama watashinda au la, kwani amewapa kombe na kuweka rekodi nyingine kubwa, baada ya mtangulizi wake, Roberto Di Matteo kutwaa Kombe la Mabingwa Ulaya msimu uliopita, lakini Chelsea wakaweka rekodi mbaya ya kuwa bingwa mtetezi wa kwanza kutolewa hatua ya makundi.
Baada ya gwaride la ubingwa wa England la Manchester United, lile la Manchester City kuota mbawa baada ya kufungwa na Wigan, Chelsea watakaporejea London kutoka Amsterdam wanatarajiwa kuwaonesha washabiki wao linavyofanana kombe hilo.
Comments
Loading…