in , ,

Pazia la Ligi Kuu England lafunguliwa-Naziangalia timu zote za EPL

 Na: Israel Saria
MIAMBA 20 ya soka inaanza kupimana nguvu kwenye Ligi Kuu ya England (EPL), katika msimu mpya wa 2012/13.
Huu ni mwanzo wa miezi mingine tisa ya misukosuko, utata, timu kutamba na nyingine kunyong’onyea, ilimradi tu ni mikikimikiki ya ligi.
Tunao mabingwa wapya, Manchester City waliowapoka kombe majirani wenzao – Manchester United.
Je, msimu huu wataweza kuhimili vishindo na kulinda heshima ya Etihad? Wataweza kukabiliana na wapinzani wao wakubwa – United?
Chelsea, Tottenham na Liverpool zinaingia dimbani baada ya kupata makocha wapya wa kudumu, hivyo wakilenga kuimarisha vikosi vyao.
Je, Arsene Wenger wa Arsenal atairejesha klabu kwenye mbio za kuwania taji? Timu mpya zilizopanda daraja za Southampton, Reading na West Ham hazitapenda kuona zikiadhiriwa na kurejeshwa ligi ya chini.
Nahodha wa Arsenal aliyehamia Man Utd
Lakini pia klabu zinazojitutumia za Norwich, Swansea na West Brom nazo zina makocha wapya.
Kipenga kimeshapulizwa, pazia linashushwa na wanaume wanaanza kuchuana kuwania pointi tatu muhimu kwa kila mechi.
Arsenal
Washika Bunduki hawa wa London wanaingia wakiwa bila nahodha wa wa msimu uliopita, Robin van Persie. Kahamia Manchester United kwa dau la Pauni milioni 24.
Hata hivyo wanazo bunduki mpya katika Santi Cazorla, Olivier Giroud na Lukas Podolski.
Bado kiungo wa kimataifa, Jack Wilshere anauguza goti lake, na huenda akarejea uwanjani Oktoba hii. Walimaliza msimu uliopita wakiwa nafasi ya tatu.
Aston Villa
Timu ya Aston Villa haikufanya vyema msimu uliopita, kwa sababu ilimaliza ya 16.
Utendaji wao mbovu ndio ulisababisha wakamfukuza kocha wao, Alex McLeish baada ya kunusurika kushuka daraja. Walijadiliana na mwanasoka mkongwe Ole Gunnar Solskjaer kuwa kocha, lakini wakaishia kumteua Paul Lambert wa Norwich kuwa bosi mpya.
Lambert anasema Stiliyan Petrov ataendelea kuwa nahodha, licha ya kutokuwa kikosini kwa vile anasumbuliwa na mkanda wa jeshi. Mwenyewe anasema anakaribia kupona.
Katika siku 14 za Novemba, watakuwa na wakati mgumu kwani watakabiliana na Manchester United, Manchester City na Arsenal. Mechi ya kwanza ni dhidi ya Norwich, timu ya zamani ya kocha huyo.
Washabiki wanaamini kwamba uwapo wa Lambert utarejesha ile chachu ya ushindi iliyokosekana miongoni mwa wachezaji kwa muda mrefu.
Chelsea
Chelsea hawakuwa wazuri kwenye ligi, lakini walifanikiwa kutwaa Kombe la FA na kutamba Ulaya kwa kutawazwa mabingwa wa Ulaya. Walimaliza ligi wakiwa nafasi ya sita.
Wamemtangaza Roberto Di Matteo kuwa kocha mkuu wa kudumu. Bado kuna tetesi kwamba Pep Guardiola aliyeng’atuka Barcelona ataingia Chelsea baada ya mwaka mmoja hivi. Matteo anasema hakiogopi kivuli chake.
Chelsea wamesajili wachezaji wapya, Eden Hazard, Oscar, Marko Marin na Thorgan Hazard. Lakini pia wameondokewa na nyota wao, Didier Drogba aliyekwenda Shanghai Shenhua ya China.
Wanaanza ligi huku kepteni wao, John Terry aliyesafishwa na mahakama kwa ubaguzi wa rangi dhidi ya Anton Ferdinand wa Queen Park Rangers (QPR) kufunguliwa mashitaka mapya na Chama cha Soka (FA).
Wanaanza mechi ya kwanza ugenini dhidi ya Wigan, kisha Reading na Newcastle nyumbani halafu QPR ugenini na Stoke nyumbani.
 
Everton
Everton ya kocha David Moyes haipo vibaya kwa sababu licha ya kumaliza nafasi ya saba, kwenye Kombe la FA ilifika nusu fainali.
Ina vifaa vipya kama Steven Pienaar kutoka Tottenham na Steven Naismith wa Rangers. Wana wachezaji waliozoeana, hivyo inaelekea watafanya vizuri.
Fulham
Hii ni timu ambayo husumbua vigogo, haitabiriki, lakini kwa ujumla haina matokeo mazuri sana. Ilimaliza ligi katika nafasi ya tisa na sasa kuna kila dalili ya kuwakosa wachezaji wao mahiri Clint Dempsey na Moussa Dembele.
Kuondoka kwa nahodha wao muhimu, Danny Murphy kunaacha pengo kubwa kwenye kiungo.
Kocha Martn Jol atakuwa na kibarua dhidi ya
Chelsea, Tottenham na Newcastle mwishoni mwa Novemba na mwanzoni mwa Desemba, hivyo anatakiwa kugangamala.
Liverpool
Anfield ina wimbo mpya wa kutaka kuijenga timu upya, kuirejesha enzi za zamani ilipokuwa ikitawala mpira vyema kwa pasi za uhakika na mashambulizi makali.
Baada ya kumwondosha mkongwe wa Anfield, Kenny Dalglish, nafasi yake amepewa Brendan Rodgers kutoka Swansea, ili alete mfumo wa timu ile Anfield.
Katika kuhakikisha anajenga soka anayoipenda, Rodgers amemchukua Joe Allen kutoka timu yake ya zamani ya Swansea kwa Pauni milioni 15 na mchezaji mahiri, Fabio Borini wa Roma kwa Pauni milioni 11. Andy Carroll, pamoja na kuwa timu ya taifa ya England, ameoneshwa pa kutokea, kwamba hawezi kwenda na mfumo unaotakiwa na wamiliki wa Kimarekani.
Manchester City
Wamwaga fedha hawa wa Manchester ndio mabingwa wa England, lakini msimu huu hawajaonesha makeke kwenye usajili.
Mchezaji mpya aliyetajwa kabla ya kuanza ligi ni Jack Rodwell kutoka Everton.
Wanacho kikosi chenye wachezaji wazuri, wanaoelewana na baadhi wameongeza mikataba ya muda mrefu, kama alivyofanya kocha Roberto Mancini.
Manchester United
Hawa walivuliwa ubingwa msimu uliopita, na sasa wanataka kurejesha heshima, pengine ndiyo maana wamemsajili nahodha wa zamani wa Arsenal, Robin van Persie.
Kocha Alex Ferguson anasema Van Persie akiungana na Wayne Rooney, upachikaji mabao utakuwa si wa kawaida, hivyo kuwa rahisi kutwaa vikombe.
Wachezaji wengine wapya ni Shinji Kagawa na Nick Powell.
 
Newcastle United
Hii ni timu iliyoanza kuchanua katika mzunguko wa pili wa EPL, na laiti ingezinduka mapema ingemaliza ligi katika nafasi nzuri zaidi.
Hata hivyo haikuwa pabaya, kwani ilikuwa nafasi ya tano.
Vijana hao wa Alan Pardew watatakiwa waanze kwa nguvu, na watashukuru iwapo tegemeo lao kubwa, Msenegali Papiss Cisse, atarejea cheche zake za mwishoni mwa msimu uliopita wa.
Wanaanza ligi huku wachezaji wote muhimu wakiwapo, na pia atakuwa na wale aliowakosa msimu uliopita, mlinzi Steven Taylor na winga Mfaransa, Sylvain Marveaux.
 
Norwich City
Norcwich City ilimaliza msimu uliopita wa ligi ikiwa nafasi ya 12. Imepoteza kocha wake, Paul Lambert aliyenyakuliwa na Aston Villa na kumteuat Chris Hughton wa mahasimu wa mjini kwao, Birmingham.
QPR
Queen Park Rangers au kama ilivyozoelekea, QPR, ni timu iliyosumbua vigogo karibu na mwisho wa msimu uliopita, hadi ikasalimika kushuka daraja.
Hadi mechi ya mwisho dhidi ya Manchester City, haikuwa na uhakika wa kubaki, na ilitangulia mara mbili kuifunga City, kabla matajiri hao hawajachomoa na kutwaa ubingwa.
Chini ya kocha Mark Hughes aliyepata kuchezea Man United, QPR ilimaliza ya 17 na msimu huu wanaanza na wachezaji wapya, Samba Diakite aliyekuwa Nancy, Park Ji-sung kutoka Manchester United na Junior Hoilett wa Blackburn.
Kiungo wake muhimu, Joey Barton amefungiwa mechi 12 na FA na klabu imemvua unahodha baada ya fujo alizofanya dhidi ya Man City katika mechi ya mwisho ya msimu.
Reading
Reading ni timu mpya kwenye ligi hii, japokuwa ilishapata kucheza EPL miaka iliyopita. Ilishika nafasi ya kwanza katika kufuzu kucheza EPL.
Msimu uliopita ilishindwa kwa ncha ya sindano kuingia, baada ya kushindwa kwenye mechi muhimu.
Klabu hii imenunuliwa na bilionea wa Kirusi, Anton Zingarevich na huenda akaipa msuli wa kifedha kuchanja mbuga inavyotakiwa.
Southampton
Hawa ni wageni wengine kwenye EPL na walishika nafasi ya pili kwenye harakati za kufuzu.
Hawa wanaanza kampeni yao kwa kucheza na mabingwa watetezi, Manchester City uwanja wa Etihad kabla ya kuwakaribisha Wigan na Manchester United.
Stoke City
Hii ni timu nyingine iliyokuwa eneo lisilo zuri sana msimu uliopita katika EPL, kwani ilimaliza ikiwa ya 14.
Sherehe za Krismasi zinaweza kuwa tamu au chungu kwao, kwani watakabiliana na Tottenham, Liverpool, Manchester City na Chelsea katika wiki tatu zinazoizunguka sikukuu hiyo.
 
Sunderland
Sunderland walimaliza msimu uliopita wakishika nafasi ya 13 pia, hivyo kocha Martin O’Neill ana kazi ya kurejesha makali ya zamani, ili awe na kikosi cha ushindani zaidi.
Udhaifu mkubwa unaonekana kwenye washambuliaji zaidi, na hata kwenye usajili wa majira ya kiangazi, hakuna mchezaji anayeweza kusemwa ni nyota aliyesajiliwa.
Katika mechi zao 13 za mwisho walishinda mbili tu. Walimtimua kocha waliyekuwa naye, Steve Bruce, na sasa wamejenga imani kwa O’Neil licha ya matokeo hayo.
Swansea
Swansea ni kama yatima, kwa sababu baba aliyewalea wakiwa daraja la chini, akawapandisha daraja na kuwafanya waendeleze soka ya kuvutia amewahama.
Brendan Rodgers aliitika mwito wa Liverpool, licha ya kuwa awali alitajwa angejiunga Tottenham na kusema hangaliaondoka Swansea.
Walimaliza ligi na Rodgers wakiwa nafasi ya 11 katika msimu wa kwanza tu EPL, ufanisi ambao ni mzuri.
Timu sasa inanolewa na kiungo wa zamani wa
Real Madrid na Barcelona, Michael Laudrup. Ni kusubiri tu kuona tija yake, kwa vile ndio msimu wa kwanza.
Tottenham Hotspur
Klabu inayong’ara katika jiji la London ilimtimua kocha iliyokaa naye kwa miaka minne, Harry Redknapp, baada ya kukosa nafasi ligi za Ulaya.
Ilitangaza ilitaka kijana mwenye hamasa, naye akatokea kuwa kocha wa zamani wa Chelsea, Andre Villas-Boas ambaye ameanza makeke, ikiwa ni pamoja na kutangazia vita Chelsea iliyomtimua mapema.
Tottenham ilimaliza ligi ikiwa ya nne, lakini Chelsea ikainyang’anya nafasi yake ya ushiriki Ulaya baada ya kutwaa kombe la Ulaya.
Wachezaji wapya klabuni hapo msimu huu ni Jan Vertonghen, Gylfi Sigurdsson na wengine majadiliano yanaendelea.
Luka Modric amekuwa kama Van Persie, akilazimisha kuondoka wakati klabu bado inamtaka, hisia ake zote zikiwa Real Madrid.
Gareth Bale amepona baada ya kuwa majeruhi, lakini nahodha Scott Parker hatacheza mwanzoni mwa msimu, kwani ni majeruhi.
West Brom
West Bromwich Albion ni timu iliyomaliza msimu uliopita ikiwa nafasi ya 10.
Imemwajiri kocha msaidizi wa zamani wa Liverpool na Chelsea, Steve Clarke kuwa kocha mkuu. Hiyo ilikuwa baada ya Roy Hodgson kuteuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya England.
Clarke ana kibarua kigumu na tata, maana anaanza na timu aliyoikimbia mara ya mwisho – Liverpool. Washabiki wanatarajia kumaliza katika nafasi 10 za juu.
West Ham
West Ham United ni wageni wengine kwenye EPL, japo nao wanafanya marejeo, kwa sababu walichacheza humu. Waliingia katika dirisha la pili la mechi za mtoano.
Ni timu inayoingia na kocha mwenye jina kubwa – Sam Allardyce na klabu inasema imeingia kwneye kipindi muhimu, japokuwa chaweza kuwa kigumu.
Wanaanza kucheza na timu sita zilizomaliza nje ya nane bora, hivyo huenda ikawapa morali wachezaji iwapo wataweza kuanza kwa ushindi.
Wigan
Wigan ilimaliza msimu uliopita katika nafasi ya 15 na inajiwinda kwa msimu mpya bila mabadiliko makubwa sana
Wigana wana mchezo wa kuvutia, na huenda kocha
Mhispania, Roberto Martinez akawaimarisha vijana wake ili washinde mechi zaidi na kutafuta fahari ya vikombe.
Martinez alisafiri hadi Marekani kusailiwa na wakuu wa Liverpool, lakini ghafla akaachwa hewani na Rodgers kuchukuliwa.
Bila shaka atataka kuwaonesha Liverpool Novemba 17 kwamba wakuu wao hawajui kufanya usaili.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Robin Van Persie atua Manchester United

Pazia la Ligi Kuu England lafunguliwa