in , ,

Paul Godfrey katusahaulisha Juma Abdul

Mchezaji bora wa ligi kuu ya Tanzania mara mbili mfululizo. Ukisikia hiki cheo kitu kinachokuja kwenye akili yako ni mshambuliaji.

Hawa ndiyo tumezoea kuwaona wakichukua sana hizi tunzo. Wametufanya tuone tunzo za uchezaji bora wameumbiwa wao tu.

Ni nadra sana kusikia beki amekuwa mchezaji bora wa msimu. Ni nadra sana. Hata katika tunzo za Ballon D’or huwezi kuona.

Ilitokeaga tu Fabio Cannavaro, tangu hapo hakuna hata beki mmoja ambaye amekuja kuwa mchezaji bora kwenye tunzo za ballon d’or.

Licha ya kupita vipaji Vingi sana vyenye kuvutia sana kwenye nafasi mbali mbali za beki lakini hakuna ambaye amekuja kuvunja rekodi ya Fabio Cannavaro.

Leo hii tunamshuhudia taratibu Sergio Ramos anaelekea kumaliza maisha yake ya mpira kama mchezaji lakini bila kuwa na Ballon D’or mkononi.

Hivyo ndivyo dunia ya mpira ilivyo na ukatili wa hali ya juu. Ukatili ambào anaenda kufanyiwa Sergio Ramos ndiyo huo ambao aliwahi kufanyiwa Nemanja Vidic.

Hapa nazungumzia mabeki hodari kuwahi kutokea kwenye ardhi hii (Nemanja Vidic na Sergio Ramos), ambao walishinda kila kitu kwenye ngazi ya klabu.

Ambao walikuwa wanaogopeka sana. Walikuwa wanaheshimika sana na bado wanaheshimika sana mpaka muda.

Ambao hakuna kocha ambaye angeweza kuwakataa kuwa nao kwenye timu. Lakini mwisho wa siku hawakuwahi kubeba tunzo ya Ballon D’or.

Unamkumbuka Philippe Lahm?, yule aliyewahi kuwa beki wa kulia wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani ?

Yule ambaye Pep Guardiola aliwahi kukiri kuwa hajawahi kufundisha mchezaji mwenye ubongo wenye daraja kubwa la kufikiria katika mpira kama yeye ?

Hapo ukumbuke Pep Guardiola amewahi kuwafundisha kina Lionel Messi, Xavi, Iniesta, Henry , Puyol lakini yeye anaamini hakuna mchezaji aliyewahi kuwa na akili kubwa ya mpira kama yeye.

Lakini pamoja na sifa zote alizowahi kuzipata Phillipe Lahm hakuna tunzo ya Ballon D’or iliyowahi kuja katika mikono yake.

Huyu ni beki, beki wa kulia kama ambavyo alivyo Juma Abdul. Beki bora ambaye aliwahi kushinda tunzo ya mchezaji bora wa ligi kuu mara mbili mfululizo.

Alikuwa moja ya mabeki bora sana katika kikosi cha Yanga. Ubora ambao uliusaidia sana timu na yeye kuheshimika sana.

Hadithi imekuwa tofauti sana kwa siku za hivi karibuni tangu awe majeruhi, ubora wake umepungua sana tofauti na zamani.

Leo hii miguu yake inashinda sana kwenye benchi tofauti na zamani ambavyo alikuwa añashinda ndani ya uwanja.

Kwa sasa ndani ya uwanja kuna Paul Godfrey, kinda ambaye ametoka katika timu ya vijana na Leo hii yupo katika nafasi ya Juma Abdul.

Kiwango chake kimetufanya tumsahau kabisa Juma Abdul. Hatumkumbuki tena kwa sababu ya kiwango bora cha Paul Godfrey pekeee.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Mambo muhimu kwenye mechi ya YANGA na SIMBA

Tanzania Sports

Kepa katuonesha SARRI hana SAUTI NZITO !