in

Nyota wanaotamba soko la uhamisho kwa sasa….

*Mawakala, klabu zapigana vikumbo kuwasajili
*Ligi Kuu Uingereza yaongoza kwa kuwanyakua

DIRISHA la usajili la majira ya kiangazi lingali wazi kabisa, likiacha wadau kufurahi au kuudhika na wanaopita hapo kubadili timu.
Klabu kadhaa zimepeleka wachezaji wao maeneo ya mbali na makazi yao kwa ajili ya mechi za kujipima nguvu, nyingi zikivuka bahari kwenda mabara tofauti.

Kuna usajili uliokamilika, unaoendelea huku klabu nyingine, mawakala na wachezaji wakiendelea kushikana mashati au kushawishi wachezaji kubaki au kuondoka waliko ili kujiunga nao kabla dirisha halijafungwa mwishoni mwa Agosti.
Tuanzae na Clint Dempsey. Mmarekani huyu mwenye umri wa miaka 29 anayechezea Fulham ni mmoja wa washambuliaji ghali.
Anaweza kuhama maana mkataba wake unakatika, na atafanya hivyo ikiwa dau la klabu yake litafikiwa. Liverpool inamtaka, na inafikiria kuwapa Fulham kitita cha fedha pamoja na mchezaji wake Charlie Adam juu.
Arsenal inadaiwa kukikinaishwa na mchezaji wake Mdenishi, Nicklas Bendtner anayetafuta jinsi ya kupata makazi nje ya London. Alikuwa Sunderland kwa mkopo, lakini kwenye mashindano yaliyoisha ya Uefa 2012 aliwika vyema. Anahusishwa na kuhamia AC Milan ya Italia au Galatasaray ya Uturuki. Arsenal wangependa kumuuza mapema iwezekanavyo ili kupunguza mzigo wa mishahara na kupata fedha kununua mchezaji wamtakaye.
Newcastle United inaendelea kutafuta nyongeza ya mabeki au viungo wakabaji, na mmoja anayetupiwa macho ni beki wa kushoto, Aly Cissokho wa Olympique Lyon ya Ufaransa.
Tottenham Hotspur (Spurs) ya Andres Villas-Boas imetua hapo hapo Lyon, ikimtaka golikipa wake Hugo Lloris ambaye pia ni nahodha wa timu ya taifa ya Ufaransa.
Ana umri wa miaka 25 na ni mlinda mlango mahiri mwenye nyota itakayozidi kung’aa. Kwa muda sasa Spurs hawana suluhisho la kudumu langoni mwao, pengine Lloris ataziba.
Chelsea wanaonekana kumnyatia mshambuliaji nyota wa FC Porto, Hulk, lakini Andre Villas-Boas naye ameingiza mikono yake hapo, haijulikani nani atampata, kama yupo.
Wakati Daniel Agger akionekana yu kamili kutetea jahazi la Liverpool ya Brendan Rodgers inayojengwa upya, hakuna uhakika wake kubaki hapo Merseyside, kwani wababe wa dunia – Barcelona wanamtaka. Liverpool wataacha kushawishika na kitita cha Wahispania hao?
Simulizi ndefu ya nahodha mshambuliaji wa Arsenal, Robin van Persie haitaki kumalizika, nap engine mwisho utakuwa mtamu zaidi, maana vigogo vinne vinampigania – Arsenal alipo, Manchester City, Manchester United na Juventus wanaotaka kumwondosha kabisa Uingereza.
Kizungumkuti kingine ni Luka Modrick wa Spurs anayesakwa na mwenyewe akitaka kuondoka, na hadi katikati ya wiki alishapigwa faini mara mbili na klabu yake kwa kutofanya mazoezi na wenzake. Ndoto ya kuchezea Real Madrid inamrudia usiku na mchana na pengine si kosa lake.
Real wanakataa kuwalipa Spurs dau zima wanalotaka, lakini uzuri ni kwamba kuna zaidi ya mwezi kumaliza mambo hayo. Lakini roho ya mtu itahemea juu juu muda wote huo si atashindwa hata kucheza muda ukiwadia?
Washika Bunduki wa London wanahusishwa na kumtaka nyota wa kimataifa wa Hispania na Athletic Bilbao, Fernando Llorente Torres kwa ajili ya kuwa ngao ikiwa van Persie atayeyuka.
Kinda wa Wigan, Victor Moses ni moja ya vipaji vinavyoibukia kwenye timu iliyonusurika kushuka daraja msimu uliopita na ametupiwa macho sana.
Chelsea waliodhamiria kubaki matawi ya juu wanamuwinda na wametenga Pauni milioni saba, licha ya Wigan au wana Latics kuaminiwa kufikiria dau la Pauni milioni 10.
Kwenye kioo wanakuja tena Tottenham, pengine kwa sababu ya uwapo wa AVB – wanamtaka mchezaji mahiri wa Malaga, Santi Cazorla; na huyu anasemwa atakuwa mbadala wa kwanza wa Luka Modric iwapo ataondoka.
Mchezaji huyu ndiye amekuwa chachu ya timu hiyo kuingia kwenye nne bora nchini Hispania.
Barcelona wanapiga baragumu sokoni wakitafuta pa kumuuza kiungo wao, Ibrahim Afellay aliyechoshwa na maisha ya Camp Nou.
Wanasema mitaani kwamba mchezaji huyo angependa acheze London kwa kujiunga na The Gunners au Italia kwa kujiunga na Inter Milan. Ama klabu za Spurs, Liverpool na AC Milan zinadaiwa kumtamani mchezaji huyo.
Majaliwa ya Andy Carroll wa Liverpool na timu ya taifa ya England hayajajulikana, lakini wadau vijiweni wanasema dau la Pauni milioni 35 alilonunuliwa nalo miezi 18 iliyopita ni kubwa mno, kwani si mzuri kihivyo. Zipo klabu nyingi zilizo radhi kutoa Pauni milioni 15 msimu huu wa kiangazi zimchukue.
Kocha Rodgers yu tayari kwa mazungumzo ili kijana huyo mwenye umri wa miaka 23 aondoke Merseyside asikopendwa, licha ya kuchipua mwishoni mwa msimu wa 2011/12 hadi akaitwa timu ya taifa.
Mwingine anayetarajiwa kuondoka hapo ni Martin Skrtel, mlinzi wa kati kutoka Slovakia, aliyekuwa mmoja wa wachezaji wazuri zaidi England msimu uliopita. Anadaiwa atajiunga Manchester United au hata kwenda ng’ambo.
Kiungo wa Uruguay, Gaston Ramirez anatajwa kujiunga na Liverpool. Lakini huyu ni tegemeo la timu yake ya Bologna iliyo Serie A nchini Italia. Wengine wanasema atakwenda Juventus.
Mabingwa wa Ulaya, Chelsea, wameshakubaliana dili na Internacional kwa ajili ya uhamisho wa mchezaji machachari wa Brazil, Oscar. Hiyo itakuwa rasmi baada ya Olimpiki iliyozinduliwa jana, kwani Oscar yupo hapa London na wana Samba.
Mwanandinga wa kimataifa wa Hispania anayekipiga Athletic Bilbao, Javi Martinez (23) anadaiwa kuwa ndiye kiungo mkabaji ghali zaidi kwenye soka sasa. Ni kwa sababu hiyo, Bayern Munich, Barcelona na Manchester City  zinamuwania.
Hata hivyo, Kocha wa Bayern, Jupp Heynckes anaona kwamba bei yake ni kubwa mno, hoja inayofanana na ya Barcelona, hivyo City yenye tabia ya kumwaga mapesa ikibaki yenyewe kumdaka.
Nyota wa kimataifa wa Canada na timu ya Blackburn Rovers, Junior Hoilett ni mmoja wa wachezaji wanaofuatiliwa zaidi, ambapo baada ya timu yake kushuka daraja anaangalia jinsi ya kurejea ligi kuu.
Hoilett alikuwa kwenye mazungumzo ya mwisho ya kujiunga Queen Park Rangers (QPR).
Borussia Dortmund imekuwa katika jitihada za kuzuia klabu kumtwaa mshambuliaji wao machachari kutoka Poland, Robert Lewandowski.
Hata hivyo, kwa hali ilivyo, kuzuia huko kuna ukomo, kwani mchezaji mwenyewe ameshatamka anataka kuhama ili acheze kwenye Ligi Kuu ya Uingereza
Mwingine aliyegonganisha vichwa kwenye michuano iliyomalizika hivi karibuni ya UEFA ni mchezaji wa kimataifa wa Urusi na klabu ya CSKA Moscow, Alan Dzagoev.
Tetesi zisizokoseka kwenye soka kila wakati, zinamhusisha na kuhamia Arsenal, kwenda kuchukua nafasi ya Mrusi mwenzake, Andrey Arshavin anayetafuta pa kutokea London msimu huu wa kiangazi.
Mikasa huwa haiishi, na kwa Arsenal huu ni mwingine, kwani Liverpool na Chelsea zimesema zinamtaka winga wa kimataifa wa England, Theo Walcott.
Mchezaji huyo anayetarajiwa kujadili mkataba wake na Arsenal, anaonekana kushawishiwa, kama si kushinikizwa kuondoka klabu hiyo ya kaskazini mwa London ili akacheze ipasavyo.
Brazil inaongoza kwa wachezaji wake kumulikwa na rada msimu huu. Mshambuliaji Leandro Damiao wa
Internacional na Timu ya Taifa ya Brazil anahusishwa na AC Milan au Spurs.
Hata hivyo, hakuna kitakachoamuliwa hadi michezo ya Olimpiki, anayoshiriki, imalizike.
Kiu ya Newcastle kuongeza wachezaji wenye vipaji kwenye kundi lake msimu huu ni kali, ikidaiwa wanamuwania nyota wa kimataifa wa Ufaransa na Lille OSC, Mathieu Debuchy.
Mbrazili mwingine anayedaiwa kuwa safarini kuingia Ligi Kuu ya England ni mwanandinga wa Sao Paulo, Lucas Moura.
Wakati Kocha Mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amekiri kumtaka, klabu za Real Madrid na Chelsea nazo zinaning’iniza noti hewani kumvutia kwao.
United wanajua kwamba eneo la kiungo ndilo linatakiwa kuwa kipaumbele kwao kwenye dirisha hili kubwa la usajili, ndiyo maana hawatumii vibaya uwazi wake.
Zipo habari kwamba wanataka kumsajili nyota wa FC Porto ya Ureno, Joao Moutinho, na hakika usajili huu utakuwa mkubwa, iwapo Mashetani Wekundu hawa wataufanikisha.
Hawa ndio wanasoka walio sokoni, ambao kwa kiasi kikubwa ama wapo Ligi Kuu ya England au wanawaniwa na klabu zake, na zuri kutokana na haya ni kwamba ligi kuu msimu ujao itanoga, mtoto hatatumwa dukani.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Nyota wanaotamba soko la uhamisho

The Summer Olympic games are now hours away