Mmoja ni Afisa Mhamasishaji wa klabu na mwingine ni Afisa Habari wa klabu. Vyeo vyote viwili lazima viwe chini ya idara ya habari ya klabu ya Yanga, kwa maana hiyo yoyote ambaye atasema chochote sehemu yoyote ile lazima idara ya habari ya Yanga iwe imedhibitisha jambo hilo.
Tuachane na hilo kwanza, tuanzie hapa ili upate picha nzuri. Kumbukumbu zako naomba uzirudishe mpaka kipindi kile cha mwenyekiti wa Yanga, Bwana Yusuph Manji. Uongozi ambao ulikuwa na mafanikio makubwa sana ndani na nje ya uwanja.
Ndiyo uongozi ambao ulifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuiwezesha Yanga kushinda ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania bara mara ya tatu mfululizo. Yanga hakuwa na mpinzani kwa kipindi kile kwenye ligi yetu hii, hata wale Simba walikuwa wanaiogopa Yanga.
Ndiyo uongozi ambao ulifanikisha Yanga kufika hatua ya robo fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika mara mbili, ndiyo timu ambayo iliibana Al Ahly kule Misri. Ilikuwa timu ambayo imekamilika kwa kiasi kikubwa.
Timu ambayo ilikuwa chini ya nahodha mahiri kuwahi kutokea nchini, Nadir Haroub Cannavaro, katikati ya uwanja kulikuwa m nywele ndefu kutoka Zimbambwe za Kamusoko na miguu iliyojaa ufundi kutoka Rwanda ya Haruna Niyonzima kule mbele Kulikuwa na utatu mtakatifu wa Simon Msuva, Donald Ngoma na Obrey Chirwa.
Kikosi hiki kilikuwa kinampa kiburi kila mwana Yanga na kwa kipindi kile idara ya habari ya Yanga ilikuwa na mtu anayeitwa Jerry Muro. Mtu ambaye aliwatesa kwa kiasi kikubwa sana Simba kwa wakati huo, aliongea kila alipojisikia kuongea kwa sababu timu yake ilikuwa inafanya vyema.
Aliwaita Simba ni watu wa mchangani, hawakubisha walikaa kimya, hata wakati ambao aliposema Yanga ni wa kimataifa, watu wa kupanda ndege kila mara, Simba hawakuwa na la kusema kwa sababu huu ndiyo ukweli ambao kwa wakati huo ulikuwa wazi.
Kuna kipindi aliyekuwa mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji aliondoka kwenye nafasi yake ya uenyeketi. Viongozi wengi wakaondoka pia baada ya Yusuph Manji kuondoka, hata Jerry Muro hakuona umuhimu wa kuendelea kuwa msemaji wa timu kipindi ambacho Yusuph Manji hayupo kwenye uongozi.
Yanga ikatetereka sana, ile nafasi ya usemaji wa klabu ikachukuliwa na Dismass Ten, yeye alianza kuleta utamaduni ambao ulikuwa haujazoeleka. Hakuwa na uwezo wa kuongea sana kama Jerry Muro, ila alikuwa na uwezo wa kubuni na kufanya kwa vitendo kuliko kuongea.
Alihakikisha kurasa za Miranda ya kijamii ya Yanga iko inafanya kazi , akaja na wazo na jarida , akatengeneza ofisi maalumu ya kufanyia mikutano na waandishi wa habari. Aliongeza vitu vingi sana ambavyo awali havikuwepo kwenye idara ya habari ya Yanga.
Kwa bahati mbaya mashabiki wa Yanga hawakuhitahi hivyo vitu, wao walihitaji mdomo wake. Waliamini mdomo wake ulikuwa na nafasi kubwa sana kuliko vitu ambavyo alikuwa anavifanya na kwa bahati mbaya Dismass Ten hakuwa na uwezo wa kuongea kama ambavyo mashabiki wa Yanga walivyokuwa wanataka aongee.
Ukawa mwanzo wa mashabiki wa Yanga kuonekana wapweke mbele ya Haji Manara, shinikizo la mashabiki kutaka msemaji ambaye atapambana na Haji Manara lilianzia hapa. Na huu ndiyo ukawa mwanzo wa Hassan Bumbuli na Antonio Nugaz kuwa kwenye idara ya habari ya Yanga.
Antonio Nugaz aliletwa kwa ajili ya kupambana na Haji Manara mdomoni kwa sababu huo uwezo anao , aliletwa kwa ajili ya kuondoa upweke kwa mashabiki wa Yanga na kuwafanya wahamasike zaidi ili waje angalau kwa wingi kwenye viwanja kuishuhudia timu yao.
Turudi kwenye hoja yetu ya kwanza ambayo nilianza nayo kwenye makala hii , Antonio Nugaz na Hassan Bumbuli wanafanya kazi katika ofisi moja (idara ya habari ya Yanga) chochote kile ambacho watatakiwa kuongea sehemu yoyote lazima kiwe kimedhibitishwa na idara hii ya habari.
Siyo kudhibitishwa tu, lazima waseme kitu ambacho kinafanana kwa sababu kinatoka sehemu moja. Juzi baada ya Yanga kuachana na aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Yanga, kulikuwa na taarifa mbili tofauti kutoka kwa hawa watu wawili.
Hassan Bumbuli alisema kamati tendaji ya klabu ya Yanga imeachana na katibu mkuu kwa makubaliano ambayo yalikuwa na faida kwa pande zote mbili. Lakini Hassan Bumbuli alisema kuwa kamati tendaji ya klabu ya Yanga hawajatoa sababu ya kwanini Yanga imeamua kuachana na katibu huyo.
Antonio Nugaz alipohojiwa alisema kamati tendaji imetoa sababu ya kwanini Yanga wameachana na katibu mkuu wao, yeye alisema katibu mkuu huyo alikuwa haendani na kasi ya Yanga, kuelekea kwenye mabadiliko ya uendeshaji wa klabu Yanga walihitaji katibu mwenye kasi.
Watu wawili ambao wanafanya kazi katika ofisi moja wametoa majibu mawili tofauti kwenye swali lile lile. Hii yote inaonesha hakuna mawasiliano kati yao kipindi ambacho kama kuna taarifa inatakiwa kutoka kwa walaj, hapa wanaonesha kiwango hafifu cha ueledi.
Comments
Loading…