in , ,

NI WAKATI WA SAMATA NA ULIMWENGU

Akiwa katika timu ya Taifa

 

Mbwana Samata juzi aliifungia TP Mazembe mabao matatu kwenye mchezo wa Kundi A wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Moghreb Tetouan. TP Mazembe walipata ushindi mnono wa 5-1 na kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Hii ni mara ya tatu kikosi cha TP Mazembe kutoka jiji la Lubumbashi nchini Congo DRC kinakwenda kucheza nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kikiwa na nyota wawili kutoka Tanzania, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu.

Mara ya kwanza ilikuwa ni kwenye michuano ya 2012 ambapo Mazembe iliingia nusu fainali na kutolewa na Esperance ST ya Tunisia. Bao pekee la Mohamed Ben Mansour kwenye mchezo wa pili wa nusu fainali jijini Tunis liliwanyima Samata na Ulimwengu nafasi ya kutinga fainali ya michuano hiyo

Mara ya pili ilikuwa ni mwaka jana 2014 ambapo Mazembe ilienguliwa kwenye hatua za nusu fainali na ES Setif ya Algeria ambayo ikaenda kutwaa taji la michuano hiyo kwenye mchezo wa fainali dhidi ya AS Vita Club ambayo pia ni ya Congo DRC.

Mwaka 2009 na 2010 TP Mazembe ilitwaa ubingwa wa Afrika mara mbili mfululizo. Samata na Ulimwengu walikuwa bado hawajajiunga na timu hii na wala hakukuwa na mchezaji yeyote wa Tanzania ndani ya kikosi cha Mazembe. Mwaka 2010 timu hiyo ilitinga mbaka fainali ya michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia.

Kwa vyovyote vile Samata na Ulimwengu wanatamani kuyafikia mafanikio haya wakiwa na TP Mazembe. Wameshashinda taji la Ligi Kuu ya nchini Congo DRC mara nne mfululizo wakiichechezea timu hiyo. Hivyo hakuna mafanikio zaidi wanayoyatamani kwenye soka la ndani la Congo DRC.

Wanachokitamani kwa sasa nyota hao wawili kutoka Tanzania ni kuyafikia mafanikio kama waliyofikia Tresor Mputu na Dioko Kaluyituka. Mputu na Kaluyituka walikuwa  nyota tegemeo wa kikosi cha Mazembe kilichotwaa mataji ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika 2009 na 2010.

TP Mazembe wanao uwezo wa kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka huu. Pengine uwepo wa Samata ndilo tumaini kubwa la TP Mazembe  kwenye hatua ya nusu fainali ambayo Mazembe watacheza dhidi ya El Merreikh ya Sudan tarehe 25 mwezi huu na tarehe 02 mwezi ujao.

Natumaini safari hii Samata na Ulimwengu hawataishia nusu fainali. Wataiwezesha Mazembe kutinga fainali na kutwaa ubingwa dhidi ya USM Alger ya Algeria au Al-Hilal ya Sudan mwezi Novemba mwaka huu. Kiwango cha Samata na wachezaji wengine wa TP Mazembe vinatosha kutimiza utabiri huu.

Wakishatwaa ubingwa huu wa bara la Afrika watakuwa wamekata tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia itakayofanyika nchini Japan kuanzia tarehe 10 mbaka 20 mwezi Disemba mwaka huu.

Samata na Ulimwengu wakiwa na kikosi cha TP Mazembe natumaini watavuka hatua za robo fainali kama walivyofanya wakina Tresor Mputu mwaka 2010 ambao walifanikiwa kutinga mbaka fainali waliyopoteza dhidi ya Inter Milan.

Mabingwa wa Ulaya FC Barcelona na mabingwa wa Amerika ya Kusini River Plate ya Argentina tayari zipo kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano ya Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA. Ikiwa Samata na Ulimwengu watafanikiwa kuiwezesha Mazembe kufika hatua hii watakutana na moja ya klabu hizo. Naamini ni wakati wao kuyafikia mafanikio hayo.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

MATOKEO LIGI YA MABINGWA ULAYA

Tanzania Sports

ARSENAL YAZAMISHWA UGENINI (CL)