Yanga imetolewa kwenye hatua ya robo fainali ya klabu bingwa ya afrika na klabu ya Mamelodi Sundowns. Imetolewa katika hatua ya mikwaju penati baada ya kumaliza dakika zote 180 bila ya kufungana na hivyo kupelekea kwenda kwenye hatua ya matuta. Hakika kila mchezaji wa Yanga anastahili pongezi kwa matokeo na hatua ambayo klabu hiyo imefikia. Katika mechi zote mbili za robo fainali ambazo klabu ya Yanga ilicheza dhidi ya klabu ya Mamelodi Sundowns hamna mchezaji ambaye alingara sana kwenye mechi hizo Zaidi ya Djigui Diarra. Golikipa ambaye aliondoa mashuti mengi ya wachezaji wa klabu ya Mamelodi na hivyo kufanya wachezaji hao washindwe kupata matokeo ya kupata goli ndani ya dakika 180 za uwanjani mpaka walipoenda kwenye hatua ya penati.

Diarra kabla ya kusajiliwa na wababe hao wa mitaa ya Jangwani Kariakoo alikuwa anachezea klabu ya Stade Malien ya huko nchini kwao Mali ambako alichezea kwa miaka kadhaa. Kipa huyo kwa sasa ana umri wa miaka 29 na mara nyingi kwa magolikipa wa kigeni kipindi wakiwa na umri huo huwa wanapenda kutafuta changamoto mpya na tetesi zinasema kwamba kuna vilabu kadhaa vya kimataifa ambavyo vinahitaji saini yake ili akachezee vilabu hivyo kwa misimu ijayo.

Ni kipa ambaye ni mzoefu na ana rekodi nzuri hata kwenye Nyanja za kimataifa kwani mwaka 2015 alisaidia taifa lake kushika nafasi ya tatu kwenye mashindano ya kombe la dunia la wachezaji wenye chini ya umri wa miaka 20. Yeye ndiye aliyekuwa golikipa nambari moja na kwenye robo fainali alichomoa michomo ya penati na hivyo kusaidia taifa lake kusonga mbele hadi kwenye hatua inayofuata ya nusu fainali.

Mwaka huu kwenye mashindano ya AFCON aling’ara na alionyesha uwezo wa hali ya juu kwenye nafasi yake kama kipa wa timu ya taifa la Mali. Katika timu ya wakubwa ya taifa la Mali alianza kuchezea mnamo mwaka 2016 kwenye hatua ya mechi za kutafuta nafasi ya kwenda kucheza AFCON na amekuwa msaada mkubwa kwa taifa hilo. Ana mataji 7 ya ligi ambapo 5 aliyapatia kwao Mali na 2 ameyapatia nchini Tanzania akiwa na uzi wa Yanga. Amechezea timu ya taifa jumla ya mechi 58. Ameisaidia klabu yake ya Yanga kushika nafasi ya 2 kwenye mashindano ya shirikisho barani Afrika msimu uliopita.

Kwa umahiri wake na uhodari wake ni wazi kwamba vilabu vingi vikubwa vitahitajia huduma yake na kwa hivyo thamani yake sokoni itaongezeka na vilabu vyenye pesa vitampandia dau ambalo litakuwa sio rahisi kwake kulikataa. Yatarajiwa kwamba ofa za vilabu hivyo vikubwa itakuwa ni yenye kutamanisha na kushawishi kuliko mkataba ambao atakuwa nao kwenye klabu hiyo ya Jangwani.

Amecheza mechi nyingi sana katika klabu ya Yanga bila ya kuruhusu magoli na amekuwa nguzo muhimu sana kwao katika makombe ambayo wameyabeba katika kipindi cha hivi karibuni. Ana sifa ya uongozi pindi awapo uwanjani mara kwa mara utamwona anatoa maelekezo kwa wachezaji wenzake juu ya namna ya kuzitumia fursa vizuri pindi wawapo uwanjani na hata kutoa maelekezo juu ya ni namna gani bora kurekebisha makosa ambayo wanakuwa wameyafanya kipindi wanapokuwa uwanjani. Kama akikaa mitaa ya Jangwani mda mrefu basi atakuja kuwa ni miongoni mwa magwiji wa kikosi hicho.

Mambo muhimu ambayo Yanga wanatakiwa kumfanyia kwa sasa kumbakisha ni pamoja na kuhakikisha mkataba wake unaboreshwa kwa kuboreshwa stahiki zake na pia kuangalia namna gani bora ya kumhudumia vizuri ili aweze kuendelea kubaki katika kikosi hicho. Kisaikolojia mchezaji hushawishika kuendelea kubaki katika klabu husika sio kwa sababu tu ya maslahi ya mashahara peke yake bali klabu inatakiwa iangalie namna gani bora ya kumhudumia kisaikolojia ili wamfanye aendelee kuwa bado sehemu yao na kujituma kwa wingi.

Mifano ipo mingi ya wachezaji walioacha kucheza klabu licha ya kwamba walikuwa wanapokea mishahara mikubwa lakini wakaacha vilabu hivyo mfano aliyekuwa mshambuliaji wa Brazil na klabua ya Inter Miami Adriano ambaye aliacha kucheza soka katika klabu yake ya Inter Milan na kisha kwenda kwao Brazil na kuishi mtaani. Mchezaji huyo alikuwa ameingia katika msongo wa mawazo na klabu hiyo ilikosa namna ya kumhudumia na kumsaidia mchezaji wao na akajikuta anaacha mshahara mzuri uliokuwa na marupurupu kibao na kurudi mtaani kwao huko Brazil.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0
Tanzania Sports

WATOTO WA KARIAKOO KATIKA KLABU BINGWA AFRIKA

Tanzania Sports

MASHUJAA WAMEENDELEZA USHUJAA WAO KWA SIMBA