Real Madrid sasa wako nyuma ya vinara wa La Liga FC Barcelona kwa alama 10 kufuatia sare ya bila kufungana waliyoipata dhidi ya Atletico Madrid ndani ya dimba la Wanda Metropolitano usiku wa Jumamosi. Mapema kabla ya mchezo huo vijana wa mwalimu Ernesto Valverde waliwaadhibu Leganes kwa kipigo cha 3-0 kwa mabao ya Luis Suarez (2) na Paulinho na kukamilisha alama 34 kwenye michezo 12.
Mabingwa watetezi wakiwa na alama 24 mbaka sasa wapo katika nafasi ya tatu mbele ya majirani zao Atletico Madrid walio kwenye nafasi ya nne wakiwa pia na alama 24. Tofauti ya mabao ndio inayozitengenisha timu hizi kutoka jiji la Madrid. Valencia wao wapo kwenye nafasi ya pili wakiwa na alama 34 baada ya kuwafunga Espanyol Jumapili ndani ya dimba la RCDE.
Alama 10 zinaonekana na nyingi mno na ni mzigo mkubwa kwa Real Madrid. Uwezekano wa kuziba pengo hilo unaonekana kuwa finyu kwa wengi ingawa bado kuna raundi 26 zimesalia kuelekea kumalizika kwa mashindano hayo Mei mwakani. Kwenye historia ya La Liga hakuna timu iliyowahi kuziba pengo la alama 10 na kutwaa taji la ligi hiyo.
Pengo kubwa zaidi la alama ambalo timu iliwahi kuliziba na kufanikiwa kutwaa taji la La Liga ni pengo la alama 9. Ni Barcelona chini ya mwalimu Louis van Gaal waliofanikiwa kuziba pengo la idadi hiyo ya alama na kutwaa taji kwenye msimu wa 1998/99. Historia inatoa picha kuwa Real Madrid walio nyuma kwa alama 10 hawana nafasi ya kuwapiku Barcelona kwenye mbio za La Liga msimu huu.
Pia kwa mujibu wa takwimu za Ligi Kuu ya Hispania, FC Barcelona ndio timu bora zaidi kwenye mashambulizi ikiwa imefunga mabao 33 mbaka sasa ambayo ni mengi kuliko timu yoyote. Na pia ndio timu imara zaidi kwenye ulinzi ikiwa imeruhusu mabao 4 pekee ambayo ni machache zaidi kuliko timu nyingine yoyote. Real Madrid wana kibarua cha kuwafukuza Lionel Messi na wenzie ambao wako imara mno msimu huu.
Real Madrid wao wamefunga mabao 22 pekee kwenye michezo 12 waliyocheza huku nyota wa timu hiyo Cristiano Ronaldo akiwa na bao moja tu mbaka sasa kwenye michezo nane ya La Liga aliyoichezea timu hiyo. Wamefungwa pia mabao 9 mbaka sasa idadi ambayo ni zaidi ya mara mbili ya mabao ambayo vinara wa ligi FC Barcelona wameruhusu mbaka sasa. Mabingwa hawa watetezi wanaonekana kuwa dhaifu mno msimu huu na wanao mlima mrefu wa kupanda.
Hata hivyo mwalimu Zinedine Zidane ana maoni tofauti. Ana matumaini makubwa kuwa FC Barcelona watateleza mara kadhaa mbeleni na kuwapa wao nafasi ya kuwapiku. Anasema kuwa ingawa ni kweli pengo la alama 10 ni kubwa lakini ni mapema mno kwa timu yake kukata tamaa na kwamba watapigana mbaka mwisho wa safari.
Pengine kwa upande mwingine historia inampa nafasi Zinedine Zidane kuwa na matumaini ya kuwakamata Barcelona. Kwenye msimu wa 2013/14 FC Barcelona chini ya mwalimu Gerardo Martino walianza kwa kushinda michezo 11 kati ya 12 ya mwanzo na kutoa sare mchezo mmoja pekee. Hali ndiyo ilivyo na kwenye msimu wao huu mbaka sasa. Lakini taji la La Liga kwenye msimu huo wa 2013-14 lilikwenda kwa Atletico Madrid. Hili linafundisha kuwa Real Madrid hawana sababu ya kukata tamaa mapema.
mail to: [email protected]