in , ,

HIVI SIMBA NA YANGA HAMUONI AIBU KUTUKANWA?

Mtu mzima hutukanwa kwa mafumbo, hakuna tusi la moja kwa moja linalokuja kwa mtu mzima.

Yeye fumbo ni tusi tosha kwa sababu mtu mzima ana utashi na uelewa mkubwa wa kupambanua mambo.

Yeye hutafakari kila fumbo linalokuja kwake na kulitolea maamuzi ambayo ni chanya kwake.

Tatizo huwa linakuja pale ambapo mtu mzima huyo anapotukanwa na kila mtu tena kila siku tena kwa fumbo lile lile,lakini yeye akaonesha kutojali.

Hapo lazima kwa pamoja tushangae na kujiuliza kuna nini katika akili yake.

Miaka mingi imepita, kila uchwao Simba na Yanga hupokea tusi kubwa linaloitwa kiwanja.

Kila panapokucha, mtu mpya huibuka na kuwatukana kwa fumbo lakini hakuna kitu kipya ambacho hufanyika kwa vilabu hivi kongwe.

Ni vilabu ambavyo vina umri wa babu, lakini havina maendeleo yanaosadifu umri wao.

Vina miaka mingi lakini vimekosa akili nyingi ya kujikomboa katika hali ya kujitegemea.

Tangia vianzishwe vilabu hivi vimekuwa vikiishi kwa kutegemea huruma.

Vimeshindwa kujiendesha kwa mafanikio kulingana na mtaji walio nao wa mashabiki wengi.

Vilabu hivi ni nembo ya mpira wa Tanzania, vilabu hivi vipo katika mioyo ya Watanzania wengi.

Kwa kifupi , Watanzania wengi wanavipenda vilabu hivi kwa dhati kubwa.

Lakini cha kushangaza na kusikitisha ni kwamba vilabu hivi vimeshindwa kutumia mapenzi makubwa ya mashabiki yao kujiondoa katika utegemezi.

Jana kumetoka marekebisho ya ratiba ya uwanja, ambao mechi za mwishoni mwa juma zinazowahusu hawa wazee zitachezwa katika uwanja wa Azam Complex badala ya kiwanja cha Uhuru.

Ni aibu sana kwa timu kubwa ambayo inamashabiki wengi, ina miaka mingi kwenye tasnia ya mpira kukosa sehemu yao ya kuchezea bila bugudha.

Inauma kuona Simba na Yanga kutoumizwa na kitendo hiki cha kufukuzwa fukuzwa kwenye viwanja .

Kwao wao hawajakaa na kutafakari kuwa hilo ni tusi ambalo wanatukanwa.

Masikio yao hayasikii , akili zao hazitaki kuelewa wanavyoambiwa kuwa wanatakiwa wajenge viwanja vyao ili wajitegemee wao bila bugudha.

Azam anawastili lakini ni aibu kubwa kwenda kwenye timu ambayo mnaizidi umri mkubwa lakini inawazidi maendeleo makubwa sana.

Hivi Simba na Yanga wanashindwaje angalau kutumia mtaji mkubwa wa mashabiki kujenga uwanja?

Hivi kwa mtaji huu wa mashabiki hawawezi kwenda kwenye taasisi yoyote ambayo wakaingia nayo mkataba.

Ikajenga uwanja ambao watakuwa wanalipa pole pole kwa makubaliano ya muda fulani?

Wakati wanalipa, jina la kiwanja linakuwa jina la taasisi husika ambayo imehusika kujenga ule uwanja.

Jina hilo likatumika mpaka pale ambapo deni la uwanja litakapoisha.

Hakuna mfanyabiashara ambaye atakataa kwenda kuwekeza sehemu ambayo ina mtaji mkubwa wa mashabiki.

Mashabiki ndiyo wanunuzi wa bidhaa, na mfanyabiashara yoyote yule hutafuta sehemu ambayo inawanunuzi wengi kwa ajili ya manufaa ya bidhaa yake.

Bidhaa yake inapokuwa sehemu ambayo kuna watu wengi , kuna kuwa na faida ya bidhaa yake kufika kwa watu wengi.

Lakini tunakosa watu sahihi wa kutafuta watu ambao watashirikiana kuzijenga hizi timu mbili.

Ni aibu kila siku babu kuzomewa na wajukuu zake, babu anatakiwa aheshimike na siyo kuzodolewa.

Kuna kipindi ambacho inatakiwa kifike Simba na Yanga waseme imetosha .

Imetosha kutukanwa, kuzodolewa, kudharauliwa.

Ni wakati sahihi kwao kuamka na kuanza upya, kuanza upya si dhambi.

Ni wakati sahihi wao kuviendesha Simba na Yanga kama bidhaa.

Waviendeshe hivi vilabu kibiashara ili kufikia mafanikio ambayo wanayatamani.

mail to: [email protected]

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NI MAPEMA MNO KUWAKATIA TAMAA REAL MADRID

Tanzania Sports

MAENEO MANNE YANAYOISUMBUA LIVERPOOL