MASHINDANO mapya ya Kombe la Dunia ngazi ya klabu yanatarajiwa kunguruma mwezi huu wa Juni huko nchini Marekani. Timu mbalimbali zinawakilisha mabara yao. kuanzia bara la Afrika, Ulaya, Amerika kusini, Amerika kaskazini, Asia na kwingineko. Ni mashindano ambayo yanachukua nafasi ya Klabu Bingwa Dunia ambayo yalikuwa yakifanyika kila mwezi Desemba na Real Madrid ndiye kinara kwa kunyakua mara 9. Katika makala haya TANZANIASPORTS inaangazia taswira ya mashindano hayo. Ni mashindano ambayo yamefungua nafasi kwa mashabiki,makocha, viongozi na wawekezaji. Je nini umuhimu wa mashindano wa kombela dunia la klabu?
Jukwaa jipya la kibiashara na uwekezaji
Mashindano yoyote yanapofanyika, suala la biashara ni miongoni mwa mambo yanayoangaliwa. Kwenye mashindano ya Kombe la Dunia ngazi ya klabu yanatengeneza jukwaa jipya kwa wafanyabiashara ambao wanatakiwa kujitangaza na kuwekeza. Shirikisho la soka duniani FIFA pamoja na wanachama wake wanategemea kuvuna faida kwenye mashindano hayo. Nii hi njia nyingine ambayo FIFA inatengeneza pesa na kuvisaidia vilabu vyao kutangaza biashara zao zaidi. Mabilionea wanaweza kutumia jukwaa hili jipya kuwekeza pesa na hivyo kuinua hali ya ushindani miongoni mwa vilabu. Uwekezaji ukiwa mnono ndivyo ambavyo ushindani wao unakuza fahari ya mashindano hayo.
Mwanzo mpya wa soka
Kwa muda mrefu kulikuwa na mjadala juu ya kubadilisha mfumo wa fainali za Kombe la dunia kutoka miaka minne hadi miwili. Hali kadhalika mjadala huo ulikuwepo kwneye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya yaani Euro ambapo baadhi ya wadau walitamani kuona linachezwa baada ya miaka miwili kuliko minne ya sasa.
Kimsingi ulikuwa ujumbe kuwa katika ya mashindano hayo kulihitajika burudani na fursa nyingine kwa mashabiki na wawekezaji. Kwahiyo kwa upande wa EUFA wakaja na mashindano Nations League, huku FIFA ikiingiza mabadiliko kwenye mashindano yake ya klabu bingwa dunia.
Hivyo basi, kabla ya Euro kuna burudani mashabiki wanaipata kupitia Nations League, huku FIFA wakiwaburudisha kwenye kwenye mashindano ya Koombe la Dunia la klabu. Hii ina maana mjadala wa kupunguzwa miaka ya kuchezwa fainali za kombe la dunia au Euro unakufa taratibu kwani burudani zinakuwa za kutosha na kuwaridhisha wadau wa mchezo huo.
Taswira ya dunia
Kwenye fainali za Kombe la Dunia kunakuwa na wawakilishi wachache. Timu zinazofuzu ni zile ambazo zinatazamwa kama zenye viwango vya juu na vipaji bora. Lakini mashindano ya Kombe la Dunia la klabu ni ishara ya kukusanya dunia yote kuanzia ngazi ya chini zaidi. Klabu mbalimbali zinajumuika na kushindana na wenzao kutoka mabara yao. mashindnao haya yanatengeneza taswira ya dunia ya vipaji vya soka. Fikiria Seleman Mwalimu kupangwa katika mchezo mojawapo, maana yake si tu ataitangaza Wydad Casablanca bali pia nchi yake ya kuzaliwa. Kwenye mashindano haya klabu zinatumia jukwaa hili kama sehemu ya kusaka vipaji vipya pamoja na kutangaza vipaji na ufundi wao katika kandanda. Hili ni eneo ambalo wachezaji na makocha wanatakiwa kutumia kama fursa ya kuonesha maarifa waliyonayo.
Burudani zaidi
Mashabiki wa soka wanajifunza na kuburudishwa kutoka kwenye klabu zingine. Watakuwa na nafasi ya kuona raha na burudani ya mchezo wa soka badala ya kusubiri miaka minne kushuhudia fainali za Kombe la Dunia. Katika kombe la dunia mwaka huu linachezwa mwaka mmoja kabla ya fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026 huko huko Marekani na washirika wake. mashabiki wanapata nyongeza ya burudani na kushuhudia vipaji vipya kwenye soka na kupata historia zaidi kutoka Mataifa mengine.
Mtanzania kushiriki Kombe la Dunia la klabu
Pengine inaweza kuwa rekodi ya aina yake kwenye mashindano ya Kombe la Dunia ngazi ya klabu kwa mchezaji wa Tanzania kushiriki akiwa katika klabu ya nje. Seleman Mwalimu anakuwa mchezaji wa kwanza kucheza mashindano hayo ikiwa ni rekodi ya aina yake kwa mchezaji wa Kitanzania. Hakuna mchezaji wa Tanzania ambaye ameshiriki muundo huu mpya wa Kombe la Dunia la klabu. Ilikuwa rahisi kwa klabu bingwa Dunia lakini mashindano haya yanekuja kuleta chachu nyingine kwa klabu, wachezaji, viongozi, biashara na wawekezaji.
Comments
Loading…