Chelsea imefungua ukurasa mpya kwa kumwajiri Rafael Benitez kuwa kocha wa muda hadi mwisho wa msimu huu.
Huyu anaendeleza orodha ndefu ya makocha waliowafundisha mabingwa wa sasa wa Ulaya wanaojaribu kutetea kombe hilo.
Mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich alikuwa na nia ya kumfukuza kazi Roberto Di Matteo tangu miezi sita iliyopita.
Alishindwa kwa sababu ya kombe lenyewe, lakini sasa amepata kisingizio, baada ya Chelseakushinda mechi tatu kati ya nane.
Benitez amepata kuwa kocha wa Liverpool, lakini kwa muda hakuwa na kazi.
Abramovich aliwasiliana na Mhispania huyo kabla ya mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya Jumanne wiki hii, ambapo Chelsea walichapwa mabao 3-0 na Juventus ya Italia.
Chelsea inakaribia kuwa na wastani wa kocha mmoja kila mwaka tangu Abramovich alipoinunua klabu 2003.
Di Matteo amefukuzwa saa chache baada ya kurejea na wachezaji kutoka Italia, ambako katika kujibu maswali alikiri kwamba kama kuna wa kuwajibishwa kwa matokeo ni yeye.
Upo uwezekano sasa, kwamba kipindi cha mpito cha Benitez hapo Stamford Bridge kitatoa fursa kwa aliyekuwa kocha wa Barcelona, Pep Guardiola kujiunga Chelsea akimaliza likizo yake.
Benitez mwenye umri wa miaka 52 anakuwa kocha wa tisa.
Wapo wanaoshangaa kipi kilichomkwamisha Abramovich kuchagua kocha mwingine badala ya Di Matteo alipomfukuza Andre Villas-Boas.
Ilidhaniwa kwamba kocha anayefaa Chelsea ni anayeweza kuleta ubingwa wa Ulaya kama Di Matteo, ambaye bado kombe alilotwaa lipo kwenye makabati ya klabu.
Lakini Abramovich amekuwa mtu wa kushitukiza, asiyetabirika na anayechukua hatua kupitia watendaji wake, mwenyewe akikaa mbali kana kwamba hahusiki.
Baada ya kikao kirefu, mtandao wa Chelsea uliweka wazi habari kwamba Di Matteo anaondoka kwa sababu matokeo na mwenendo wa timu si mzuri, hivyo mabadiliko lazima.
Kama ilivyokuwa kwa makocha wengine, Chelsea wameonesha kuwa ‘wakarimu’, kwa kusema daima Di Matteo anakaribishwa Stamford Bridge na ajisikie nyumbani.
Wachambuzi mbalimbali wa soka, wakiwamo Roy Keane na Gareth Neville, usiku wa Jumanne walitoa wazo kwamba kocha huyo apewe muda zaidi, walau hadi Januari aoneshe mafanikio.
Ikiwa aliondokana na Jose Mourinho kwa sare tu na timu ‘ya kawaida’, akamfuta kazi Felipe Scolari na Avram Grant haingekuwa shida kwake kumtimua Di Matteo.
Rekodi inaonesha kwamba Abramovich, akicheza nyuma ya pazia alimfukuza kazi hata aliyefanya vyema klabuni hapo, Carlo Ancelotti, japokuwa baadaye alirudi kumtafuta na kumkosa, lakini pia aliondokana na Claudio Ranieri.
Panga la safari hii limemwangukia aliyeiletea klabu kombe la Ulaya mara ya kwanza katika historia, ambapo Kocha wa Newcastle, Alan Pardew anasema Di Matteo atapata timu nyingine ‘hata kesho’.
Upo uwezekano, hata hivyo, kwamba kufukuzwa kazi kwa Mtaliano Di Matteo kunatokana na ama kushindwa kuwamudu wacheaji au wachezaji kumkataa.
Pamekuwapo taarifa za ugomvi kwenye vyumba vya kubadilisha nguo, ikiwa ni pamoja na kubwatukiana walipofungwa mabao 2-1 na West Bromwich Albion katika ligi kuu.
Mmoja wa wachezaji, David Luiz, alikiri kutokea sokomoko, na kusema walikuwa wakijiuliza kilichotokea, kwa sababu Chelsea ni timu kubwa isiyotakiwa kushindwa.
John Obi Mikel anasema siku zilizopita walikuwa wakishirikiana vyema kushambulia na kujihami, lakini hapa mwisho kujihami kumeachiwa baadhi ya watu, hali iliyowagharimu.
Benitez anaanza kwa mtihani mgumu wikiendi hii, kwani Chelsea wanawakaribisha Mabingwa wa Engald na wanaoongoza ligi, Manchester City katika mchezo wa ligi.
Taarifa ya Chelsea inasema mmiliki wake (Abramovich) na bodi wanaamini kwamba Benitez ni kocha mwenye uzoefu mkubwa.
Kwamba uwezo wake katika kusimamia soka ni wa juu na ujio wake unaweza mara moja kusaidia klabu kufikia malengo.
Mhispania huyo hana kazi tangu Desemba 2010 alipofukuzwa na Inter Milan ya Italia, aliyoitumikia kwa miezi sita tu. Anakutana na wachezaji kwenye viwanja vya mazoezi vya Cobhan.
Benitez alijiunga na Liverpool akitoka Valencia mwaka 2004.
Aliiwezesha Liverpool kutwaa Kombe la Mabingwa wa Ulaya mwaka 2005 na kuifikisha fainali mwaka 2007, kabla ya kuondoka Anfield kwa hiari mwaka 2010.
Comments
Loading…