in ,

NDEMLA FUTA VUMBI KWENYE KIOO

Kuna nafasi moja tu ya kuishi ambayo kila mwanadamu hupewa na mwenyezi Mungu.

Nafasi ambayo unatakiwa uitumie kuionesha ulimwengu sababu ambayo
ilimfanya Mungu akuumbe.

Na hii ndiyo zawadi kubwa ambayo kila mwanadamu kapewa katika nafasi
iliyo sawa na mwenzake, ƙlakini tofauti huja kwenye matumizi ya nafasi
hii.

Matumizi ya nafasi ya uhai ndiyo huleta utofaufi wa mafanikio kati ya
mtu na mtu ingawa kwa pamoja wana nafasi sawa ya kuishi.

Hapo ndipo maamuzi sahihi ndiyo uhusika katika kutafuta nafasi katika
maisha yako.

Ndipo hapo unapopata sababu ya kwanini Van Persie aliamua kutoka
Arsenal na kwenda Manchester United.

Nafasi ya kupata kombe la ligi kuu ya England ilikuwa wazi kwenye timu
ya Manchester United kuliko Arsenal.

Kuna uwezekano mkubwa Van Persie asingepata kombe la ligi kuu ya
England kama angeendelea kuwa Arsenal.

Kuna uwezekano mkubwa Samatta asingefanikiwa kucheza Europa League
kama angeendelea kubweteka na pesa za Moses pale TP Mazembe.

Alichokifanya ni kutafuta nafasi ili afike mbali.

Na hiki ndicho ambacho kila mtu hutakiwa kukifanya.

Kuwa na kipaji katika maisha yako siyo mwisho wa mafanikio yako.

Unafanyeje kuking’arisha kipaji chako ?

Uko sehemu sahihi ambayo kipaji chako kitang’aa na kukupa mafanikio
makubwa katika maisha yako ?

Uko na watu sahihi ambao watakusimamia kipaji chako kifike mbali ?

Nani mshauri wako? , marafiki zako wakoje? Wanakushauri kipi ?

Msimamizi wa kipaji chako ana akili na kiu ya wewe kufika katika
matarajio yako makubwa ?

Timu yako imebeba nafasi gani katika kufikia sehemu ambayo ni kubwa?

Una nafasi kubwa kwenye timu yako ? Nafasi ambayo itakipa nafasi kubwa
kipaji chako kung’ara zaidi ?

Haya ni maswali mengi ambayo unatakiwa ukae na kujiuliza mara mbili
mbili wakati unaangalia taswira ya kipaji chako.

Tatizo wengi wetu huangalia taswira ya vipaji vyetu kwenye kioo
ambacho kina vumbi, kitu ambacho husababisha tujionee tumefubaa ili
hali tunang’aa.

Macho yangu yanaonesha Ndemla ni mung’aavu lakini napata shida
kutambua anavyojiona yeye pindi anapojiangalia kwenye kioo .

Naamini kioo anachotumia kujiangalia kina vumbi sana ndiyo maana
namuomba afute vumbi lililopo kwenye kioo chake aone taswira halisi ya
kipaji chake.

Najua pale Simba kuna Niyonzima katika nafasi yake, najua Mzamiru pia
anashiriki kwa kiasi kikubwa kumfanya asipate nafasi katika kikosi cha
Simba.

Huu ni ugumu ambao unaonekana kwa macho tu, lakini juhudi zake
zitaondoa ugumu huu.

Ni muhimu kwake kupigana kwa nguvu na maarifa makubwa kupata nafasi
katika kikosi cha Simba ili afike mbali anapopatarajia.

Ligi yetu ina mechi chache tu, mechi 30 na mechi za kombe la
shirikisho na kombe la TFF , mechi ambazo huna dhamana ya kuzimaliza
zote kwa sababu ni mechi za mtoano ambazo unaweza kutolewa wakati
wowote.

Simba ina dhamana ya kucheza mechi 33, mechi mbili za mtoano za kombe
la shirikisho barani Africa, mechi moja ya mtoano ya kombe la TFF na
mechi 30 za ƙligi kuu.

Kwa idadi hii chache za mechi hazimpi nafasi kocha kubadilisha kikosi
ila kinampa nafasi kocha kuamini kikosi ambacho atatembea nacho katika
mechi hizi chache.

Kwa hiyo mchezaji akiwa siyo chagua la kwanza kwa kocha inabidi yeye
apigane pindi anapopata hata nafasi ya dakika 5 ili amshawishi kocha
amweke katika chaguo la kwanza.

Ndicho hicho ambacho Ndemla anatakiwa kukifanya.

Ni jambo lililowazi kuwa Ndemla siyo chaguo la kwanza la kocha Omong,
lakini nafasi anayo ya kumshawishi Omong .

Kila sekunde kwake anatakiwa aithamini ipasavyo akiwa uwanjani.

Atimize majukumu yake mara mbili ya wale wanaoanza hata kama atapata muda mfupi.

Kukata tamaa kusiwepo katika maisha yake kwa sababu anakipaji kikubwa
ambacho kinaweza kumfikisha juu anapopatamania.

Ndiyo maana narudia kusema kuna haja ya kufuta vumbi kioo
anachojitazamia aone uzuri wake katika taswira nzuri afu apiganie
kuuweka uzuri wake katika sehemu kubwa.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

HAPPY ‘Anniversary’ MESUT OZIL

Tanzania Sports

HONGERENI TFF, AZAM FC MMEWAACHIA MTIHANI WA KUFANYA