in ,

HONGERENI TFF, AZAM FC MMEWAACHIA MTIHANI WA KUFANYA

Jana TFF walifanya marekebisho ya ratiba kwa mara ya kwanza tangia
msimu huu uanze.

Marekebisho ambayo yamekuja na jambo ambalo lilikuwa kilio cha watu
wengi kwa muda mrefu.

Muda mrefu Azam Fc walikuwa wanalilia mechi zao kati ya Yanga na Simba
zichezwe katika uwanja wa Azam Complex badala la uwanja wa Taifa.

Kulikuwa na kila sababu kwa mechi hizi za Azam FC dhidi ya Yanga na
Simba zichezwe katika uwanja huu wa Azam Complex kwa sababu ni uwanja
ambao ulikuwa umekidhi vigezo vyote.

Vigezo ambavyo viliipa nguvu CAF kuwaruhusu Azam FC kutumia uwanja
wake katika mechi zote za mashindano ya kimataifa ( kombe la
shirikisho barani Afrika na Kombe la klabu bingwa barani Afrika) ,
mashindano ambayo Azam Fc ilikuwa inapata nafasi ya kushiriki.

Kitendawili kilikuwa kimebaki kwa TFF pekee kuruhusu mechi hizi za
Azam FC dhidi ya Yanga na Simba zichezwe.

Uongozi wa Karia umekuja kutegua kitendawili hiki kwa kuwaruhusu Azam
Fc kutumia uwanja wake wa nyumbani katika mechi dhidi ya Yanga na
Simba.

Ni furaha kwa Azam FC kwa sababu kwa muda mrefu wamekuwa wakicheza
ugenini dhidi ya hizi timu mbili.

Haki yao ya kucheza michezo 15 katika uwanja wa nyumbani haikuwepo .

Kwa msimu walikuwa wanacheza mechi 13 katika uwanja wa nyumbani na
mechi 17 kwenye viwanja vya ugenini.

Haikuwa haki kwao na TFF ilishiriki kwa kiasi kikubwa kuwadhulumu Azam
FC haki yao muhimu.

Kilio chao kilikuwa kwenye maji ilihali wao walikuwa samaki, TFF
walifananisha machozi yao kama maji.

Ilikuwa ngumu kwao kutambua kilio chao na kuwasaidia Azam FC katika hilo.

Wadau wengi walipaza sauti lakini sauti yao haikusikia na hakuna
aliyejitokeza kuja kusikiliza sauti za wadau mbalimbali wa mpira wa
miguu hapa Tanzania.

Nifuraha kubwa kwa TFF kuwaruhusu Azam Fc kutumia uwanja wao.

Furaha hii ije na funzo kwa Azam FC. Wasikae muda mrefu wakifurahia
hili jambo bila kujibu maswali yaliyopo kwenye mtihani huu.

Ni wakati mzuri kwa sasa Azam FC ku “Ubrand” uwanja wao Azam Complex
kwa kutumia hizi mechi mbili.

Kwa Yanga na Simba kwenda kucheza Azam Complex kuna ipa nafasi kubwa
kwao kuutangaza uwanja huu na ujulikane kwa watu wengi na mwisho wa
siku wauendeshe kibiashara.

Yanga na Simba zina mashabiki wengi sana hapa nchini Tanzania. Hasa
hasa katika jiji la Dar es Salaam ambapo uwanja wa Azam Complex upo.

Uwanja wa Azam Complex una uwezo wa kubeba mashabiki elfu tano.

Idadi ambayo ni ndogo sana na haitowanufaisha kwa kiasi kikubwa
kibiashara kwa upande wa kiingilio.

Hivo swali la jinsi ya wao kunufaika kwenye kiingilio linatakiwa
lijibiwe kwa jibu la kuongeza idadi ya mashabiki pale.

Hii ni fursa kwao kupanua jukwaa ili waweze kuingiza angalau mashabiki
elfu kumi ili waweze kunufaika zaidi na kiingilio.

Utaratibu mzuri ukiwekwa nina imani kubwa kwao wanaweza kuwekeza hapa
na kunufaika zaidi kwenye hili suala na kikawa chanzo kikubwa kwao cha
kuingiza kipato cha timu husika.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

NDEMLA FUTA VUMBI KWENYE KIOO

Tanzania Sports

NI WAKATI WA TIMU ZA ENGLAND KUTAWALA UEFA?