in , ,

Namkumbuka “MAFISANGO” Kila nikimuona “CHAMA”.

Niliwahi kumshuhudia Patrick Mafisango, macho yangu hayakujutia hata mara moja kila taswira yake ilipokuwa inapenyeza kwenye mboni ya jicho langu.

Mboni ya jicho langu ilibarikiwa sana na burudani ambayo ilikuwa inatoka katika miguu ya Patrick Mafisango. Ilikiwa burudani haswaa!, alikuwa anastahili kuitwa fundi.

Aliweza kutengeneza kila aina ya kifaa au nyumba. Yani kwake yeye kila ukimletea kifaa chochote kile alikuwa na uwezo mkubwa wa kukitengeneza tena katika ubora wa hali ya juu.

Hata majengo yaliyochakaa aliyewaze kuyarekebisha ipasavyo, na alijua kwa ufasaha ni aina gani ya rangi ilikuwa sahihi kwa ajili ya kung’arisha jengo husika.

Aling’arisha jengo , na kila jengo alilokuwa analing’arisha lilikuwa linatamanika katika kila jicho lililokuwa linamtazama. Hapo ndipo ukawa mwanzo kwake yeye wa kujipatia mashabiki wengi.

Alipendwa mno!, alikubalika sana! na akaaminika kupita kiasi!, kiasi kwamba nafasi yake ile aliyokuwa anacheza ilikuwa haiwezi kukamilika bila yeye kuwepo.

Yeye ndiye aliyeleta ukamilifu wa neno “KIUNGO WA KATI” alijua haswaa kuiunganisha timu , alijua kuichezesha timu. Alifanya kile alichokuwa anakiona yeye ni bora ndani ya uwanja.

Alifanya Simba iwe inatawala sana mchezo ndani ya dakika 90 kwa sababu tu yeye alikuwa mmiliki halali wa eneo la kiungo cha kati. Alihakikisha amejimilikisha haswaa, hatimiliki aliichukua na kuimbatia.

Hakuna aliyeweza kuja kwake ili ampore hatimiliki ile, alihakikisha kila silaha ambayo alikuwa nayo inatumika ipasavyo kuhakikisha anailinda hiyo hatimiliki.

Alikuwa na nguvu!, akabarikiwa chenga maridhawa, akawekewa uwezo wa kupiga pasi za mwisho, Mungu akamuongezea uwezo wa kupiga mashuti , vyote hivo akaona havitoshi akampa na uwezo wa kufunga.

Hapo ndipo mahaba yetu kwake yalipozidi, tukajikuta tunampenda kupitiliza , MUNGU alipoona mapenzi yetu kwa Patrick Mafisango yamezidi aliamua kumpenda zaidi yeye.

Akatuondolea kipenzi chetu katika mikono yetu, tukawa wapweke sana, tena upweke ambao ulikuwa umetawaliwa na mvua kubwa ya machozi.

Macho yetu yaligeuka kuwa bomba la kutiririsha machozi bila kuchoka. Hata mashavu yetu yalilowana sana!, kwa kifupi tulilia sana baada ya kuondokewa na Patrick Mafisango.

Tungepata wapi mtu mwingine ambaye angekuwa mwenyekiti wa kamati ya burudani kwenye ligi yetu ?, tulikata tamaa na tukaona kuwa hatutopata tena burudani maridhawa kwenye ligi yetu!.

Miaka mingi sana imepita, Leo hii ligi yetu ina mtu ambaye anastahili kabisa kuwa mwenyekiti wa kamati ya burudani kwenye ligi yetu.

Mtu ambaye ana sifa nyingi zinazoendana na sifa alizokuwa nazo Patrick Mafisango!, ni mtu ambaye ana uwezo mkubwa wa kupiga pasi, kupiga mashuti, kuichezesha timu ipasavyo.

Kwa kifupi ni mtu ambaye ana uwezo wa kuvishwa lile taji ambalo aliliacha Patrick Mafisango, taji la mwenyekiti wa burudani. Ukimtazama Chama unaona faida ya wewe kuchagua mchezo wa mpira kama mchezo wako pendwa.

Anakufanya ujivunie kwanini unapenda mpira wa miguu na anakupa sababu ya kwanini uliamua kuchagua kufuatilia mpira wa miguu.

Ni darasa tosha kwa wachezaji wetu wa ndani na ni darasa kubwa kwa kamati zetu za usajili, zinatakiwa zijifunze kutuletea wachezaji wa kulipwa na siyo wachezaji wa nje!.

Tumekuwa tuna mazoea ya kusajili mchezaji tu kisa katoka nje ya nchi lakini cha ajabu mchezaji huyo hukuta ana kiwango ambacho ni kidogo ukilinganisha na kiwango cha wachezaji wetu.

Tunahitaji mchezaji wa kulipwa!, mchezaji ambaye atakuwa darasa la kujifunzia kwa wachezaji wetu. Kwangu Mimi kwa Chama ni darasa tosha kwa wachezaji wetu.

Darasa ambalo wachezaji wetu wanatakiwa kwenda na kalamu pamoja na karatasi kisha waanze kupata elimu kubwa kutoka kwa Chama. Elimu hii ilienda na Mafisango lakini taratibu namuona Chama akiirudisha.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Simba yenye NDEMLA ni hatari zaidi kuliko Simba yenye MKUDE

Tanzania Sports

Arsenal: Mwamko wao si wa uongo