DAKIKA 90 za mchezo wa fainali ya Kombe la FA England zilitosha kuamua nani mshindi, licha ya baadhi ya mashabiki waliokuwa wanatazama mchezo huo kwa njia televisheni kudhani kutokana na mwenenndo wa mchezo huo ungeweza kumaliza dakika hizo bila kupatikana mbabe, hivyo kuongezwa dakika hadi 120 ama kupigiana penalti za kuamua bingwa.
Walikuwa ni Chelsea waliotandaza soka maridadi katika kipindi cha kwanza. Chelsea walipiga pasi za rula, walionana vema kila idara. Nafasi ya kiungo ya Chelsea ilionesha matuamini ya kuibuka washindi ikichezwa na wachezai watatu, wakiongozwa na Mateo Kovacic na Jorginho.
Hata hivyo walikuwa Arsenal walioanza kufumania nyavu za Chelsea lakini bao la Pepe lilikataliwa. Arsenal walicheza fainali hiyo wakiwa kama timu ambayo imejifunza kujipenda. Yenye makali, kujipanga, kutohofia na hamu ya kuibuka mshindi ilikuwa wazi mbele yao
Dakika chache baadaye Chelsea walipachika bao la kwanza kupitia Christian Pulisic ambaye aliwatoka mabeki wa Arsenal kwa kasi kabla ya kupachika bao hilo, huku Arsenal wakionesha kutokata tamaa.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta akiwa kwenye benchi la ufundi, alirusha mikono huku na huko, akiwahimiza wachezaji kana kwamba mchungaji anahubiria waumini wake kuwa na matumaini.
Umri, ujana,ari na nguvu za Mikel Arteta viliwafanya wachezaji wa Arsenal waone wanaye mpiganaji ambaye ahanahangaika huku na huko kuhakikisha wanaibuka washindi.
Mikel Arteta si sawa na bosi wao wa zamani Arsene Wenger ambvaye alikuwa na hamasa ya kiufundi pekee, hakujishughulisha na harakati za kuelekeza na kuhamasisha akiwa kwenye ‘touchline’.
Alikuwa Pierre Emerik Aubameyang aliyesaka goli la kusawazisha kwa timu yake. nahodha huyo wa mchezo alifanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari na beki na
na nahodha wa Chelsea, Cesar Azpilicueta hivyo mwamuzi Antony Taylor kuamuru ipigwe penalti kabla ya penalti hiyo kupigwa alihakikisha kwa kutazama marudio ya faulo hiyo. Bila ajizi Auabameyang alipachika penalti hiyo maridadi na kuandika bao la kwanza kwa Arsenal.
Kuanzia hapo sura ya mchezo ilianza kubadilika. Mpangilio wa mashabulizi ya Chelsea ulianza kuyumba, huku Arsenal wakipanga mashambulizi ya kiustadi. Safu ya ushambuliaji ya Arsenal iliongozwa na Piere Emerik Aubameyang na Alexander Lacazzete.
Kilipoanza kipindi cha pili Arsenal waliendelea kupangilia vizuri mashambulizi yao. Walijiamini na kusonga mbele kwa ustadi. Ni timu ambayo ilitoka kuwatupa nje ya mashindano wababe Manchester City, na sasa walitaka kudhihirisha kuwa wanataka kuibuka mabingwa na wanao uwezo.
Dakika chache baadaye Aubameyang alipachika bao la pili na ushindi lililowahakikishia Arsenal ubingwa. Tangu hapo Chelsea haikuwa na ubora walioonesha kipindi cha kwanza. Walitawaliwa kila kona, hawakuwa na kasi tena.
NGEKEWA YA NAMBA 14
Nahodha wa Arsenal Pierre Emerick Aubameyang anavaa jezi namba 14. Ni mchezaji huyo mwenye namba 14 ndiye aliyepachika mabao mawili yaliyoipa taji Arsenal na kuwahkikishia nafasi ya kushiriki michuano ya Ulaya msimu ujao.
Ngekewa ya namba 14 ilionekna wazi mwishoni mwa mchezo huo baada ya wachezaji wote wa Arsenal kuvalishwa jezi yenye namba hiyo. Jezi za namba 14 za Arsenal ziliandikwa ‘Always Forward’ ikiwa na maana ‘tunasonga mbele’.
Pia namba 14 ni taji lao la 14 la FA tangu kuanzishwa kwa timu na michuano hiyo. Ni namba ambayo imewapa ngekewa kutoka kwa mfungaji mwenye namba 14 hadi kuhakikisha timu yake inatwaa taji la14.
MAJANGA CHELSEA
Nahodha wa Chelsea Cesar Azpilicueta alisababisha penalti ya kwanza kwa Arsenal aktika fainali ya FA. Lakini vile vile alikuwa mchezaji wa kwanza wa Chsela kutolewa uwanjani baada ya kuumia misuli ya nyuma kwenye paja la mguu wa kushoto.
Kana kwamba haitoshi, staa wao mwingine Christian Pulisic naye aliumia nyama za paja na kushindwa kuendelea na mchezo. Kiungo nyota wa timu hiyo Mateo Kovacic lailimwa kadi ya pili ya njano hivyo kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Antony Taylor.
FAINALI YA UPWEKE
Hii fainali ya kwanza kuchezwa kwenye uwanja wa Wembley bila mashabiki. Mlipuko wa ugonjwa Corona umesababisha mchezo huo kuchezwa bila mashabiki. Sababu kubwa ikiwa ni kulinda afya za mashabiki kutokana na kirusi ya ugonjwa huo kusambaa kwa njia ya hewa.
Hii ilikuwa fainali yenye ukiwa ambapo wachezaji walipachika mabao na kushangilia kwa upweke zaidi. utamu wa mabao ni amsha amsha za mashabiki, na mbwembwe zao za kushangilia. Lakini dimba la Wembley limekuwa la kwanza kuwa mwenyeji wa fainali ambayo haina mashabiki waliohudhuria uwanjani hapo. Ni ukiwa na upweke.
Comments
Loading…