Mourinho amshusha daktari
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho amemtoa kafara daktari wa timu hiyo, Eva Carneiro, akidai kwamba alichangia kwenda kwao sare 2-2 na Swansea wikiendi iliyopita, ambapo amemwondosha kwenye benchi lake.
Japokuwa Mourinho alionesha wazi kukasirishwa na hatua ya Carneiro kwenda kumtibu Eden Hazard kwa kitambo wakati Chelsea wakiwa tayari wamempoteza kwa kadi nyekundu kipa wa Thibaut Courtois, ukweli ni kwamba daktari huyo aliitwa uwanjani na mwamuzi Michael Oliver.
Mourinho amemshusha cheo daktari huyo mwenye mvuto miongoni mwa washabiki wa Chelsea lakini sasa Mourinho ameamua kumvua kazi zake za kuwatibu wachezaji wa kikosi cha kwanza kwenye mechi. Carneiro aliitwa uwanjani mara mbili na mwamuzi Jumamosi hii.
Jumanne hii, mwanamama huyo ameelezwa kwamba hatakaa tena kwenye benchi la matabibu wa timu hiyo. Hazard alianguka baada ya kukabiliana na mchezaji wa Swansea, Gylfi Sigurdsson.
Picha ya video inaonesha wazi mwamuzi akiwaita mara mbili matabibu hao na laiti Carneiro angetumia kama utetezi huenda angerejeshewa majukumu yake.
Kimsingi, kwa kuzingatia mwongozo wa Baraza la Matabibu (GMC), Carneiro au daktari mwingine yeyote hawezi kukataa kuingia uwanjani kumtibu mchezaji, bila kujali kwamba kocha mkuu wa timu hataki mchezaji agangwe.
Madaktari, chini ya mwongozo huo, wanatakiwa kuchukua hatua haraka iwapo wanaona kwamba wateja wao wapo hatarini kiafya na ikiwa utu au utulivu wake unaelekea kuathiriwa, bila kujali matakwa tofauti ya waajiri wao.
GMC imepata kutoa adhabu kwa madaktari walioshindwa kuchukua hatua katika kiwango kinachotakiwa, ambapo kuna kashfa iliyojulikana kama ‘Bloodgate’ ya 2009, ambapo daktari wa klabu ya Harlequins, Wendy Chapman alisimamishwa kazi kwa kushindwa kuchukua hatua stahiki kwa mchezaji.
Mourinho, katika mechi ya Jumamosi, alimkasirikia Carneiro akidai kwamba alikuwa na uhakika Hazard hakuhitaji kugangwa na kwamba ilikuwa lazima daktari huyo azingatie ukweli kwamba walikuwa pungufu ya mtu mmoja tayari na kwamba kitendo chake kilisababisha Swansea wakasawazisha bao.
“Nina uhakika Eden hakuhitaji tiba pale, hakuwa ameumia. Lazima daktari auelewe mchezo na kuchukua hatua kwa kuzingatia hali ilivyo,” akasema Mourinho ambaye sasa ameamua mwanamama huyo hatakuwa daktari wa mechi, hatasafiri na timu wala kufanya nao kazi wakati wa mazoezi kiwanjani Cobham.
Jumapili hii Chelsea watasafiri kukabiliana na Manchester City uwanjani Etihad. Ni matakwa kwa kila klabu kuhakikisha wana daktari wa timu ya kwanza na mtaalamu mwandamizi wa viungo na wa utimamu wa mwili.
Mourinho anadai kwamba daktari wake huyo hakuonesha ukomavu, uzoefu wala kujituma haraka, na kwa hali hiyo atapewa majukumu mengine tofauti na aliyokuwa nayo. Caneiro alijiunga na Chelsea tangu 2009 na Jumatatu hii aliwashukuru watu kwa kumuunga mkono kwenye kazi yake.