in ,

Mzozo Hispania: Soka yaahirishwa

 

 

SOKA ya Hispania imeingia katika mtanziko na sasa Shirikisho la Soka la Hispania (RFEF) limetangaza kuahirisha kwa muda usiojulikana mashindano yote kuanzia Mei 16, chanzo kikiwa mzozo wa haki za matangazo ya televisheni na haki za wachezaji.

 

RFEF na Serikali ya Hispania wanazozana juu ya jinsi fedha zitokanazo na matangazo ya mpira kwa televisheni zinavyogawanywa.

 

Ahirisho hilo litaathiri zaidi ya wachezaji 600,000 na mechi 30,000 wakati huu msimu wa ligi ukielekea ukingoni katika nchi nyingi.

Uamuzi huo unakuja wakati Ligi Kuu ikiwa imebakisha mechi tatu, huku Barcelona wakiongoza kwa tofauti ya pointi mbili mbele ya mahasimu wao, Real Madrid.

 

Serikali ya Hispania inaridhia sheria mpya inayotoa haki sawa katika kutafuta na kupata haki za televisheni kwa klabu zote, badala ya hali ilivyo sasa ambapo ni Barcelona na Real Madrid tu wenye haki ya kujadili dili za televisheni.

 

Hali hiyo inazifanya klabu hizo mbili kuchukua karibu nusu ya fedha zote za matangazo, huku klabu nyingine zote za La Liga zikigawana nusu iliyobaki.

 

Chama cha Taifa cha Soka ya Kulipwa (LFP) chenye dhamana na ligi za madaraja mawili ya juu kinaunga mkono sheria hiyo na kinachukua hatua za kisheria kuzuia kusimamishwa kwa ligi.

 

RFEF imesema ipo tayari kwa majadiliano na serikali, lakini yenyewe imekaa kimya pasipo kutoa majibu yoyote.

 

Uamuzi wa kusitishwa kwa soka ni matokeo ya ubishani juu ya nani hasa anasimamia soka ya Hispania na ni hatima ya mvutano wa muda mrefu juu ya mgawanyo wa mapato yatokanayo na matangazo ya televisheni.

 

Barca na Real hawataki kuona utaratibu huo ukibadilika, kwani unawafaidisha na ndiyo maana huweza kusajili wachezaji wa kimataifa na kuitawala soka ya nyumbani na Ulaya pia.

 

Serikali na LFP wanataka kuona mfumo wa kugawanya mapato ukiwa sawia kama ule wa Ligi Kuu ya England (EPL), ambapo mgawo ni sawa na vinginevyo hutegemea ufanisi wa timu, ubingwa, kushuka au kupanda daraja.

 

RFEF wameingilia katika kwa sababu hawakubaliani na baadhi ya maelekezo na wanahisi kwamba mamlaka yao imedharauliwa kwa sababu hawakushirikishwa vya kutosha kuamua mambo muhimu.

 

Shirikisho hilo linasema kwamba ndilo linasimamia soka, na sasa linaonesha kwa vitendo kwa kuuchukua mpira, kukataa kucheza na kusimamisha mashindano yote katika umri wowote.

 

Mzozo huu unaeweza kulinganishwa na ule ambao hutokea England mara moja moja, huku Chama cha Soka (FA) na Bodi ya Ligi Kuu kutunishiana misuli juu ya nani ni zaidi.

 

Wanaohusika katika mzozo wa Hispania ni LFP, RFEF, Chama cha Wanasoka wa Hispania (AFE) na Serikali ya Hispania.

 

AFE wanapinga uamuzi huu mpya, ambao ukitekelezwa utafaidisha klabu za madaraja mawili ya juu tu, huku ukiwaacha yatima wachezaji wengine wote wa madaraja ya chini.

 

AFE walikuwa wameandaa mgomo wikiendi hiyo hiyo ya Mei 16/17 kupinga mabadiliko haya pendekezwa.

 

RFEF kwa upande wake wanaona kwamba Serikali ya Hispania inaingilia masuala ya soka, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).

 

Iwapo FIFA itaona hivyo, ina maana Hispania itakuwa imejitumbukiza katika hatari ya kufungiwa soka, wakati huu ambapo inajiandaa kurejesha heshima yake na ni bingwa wa zamani wa dunia.

 

Rais wa RFEF, Angel Maria Villar ambaye pia ni Makamu wa Rais wa FIFA anatambulika kuwa mshirika na rafiki wa muda mrefu wa Rais wa FIFA, Sepp Blatter.

 

Hata hivyo, Villar ana ufuasi mdogo kutoka kwa umma, lakini bosi wa LFP, Javier Tebas naye hapendwi na washabiki, sababu kubwa ikiwa kukubaliana na kampuni za televisheni kuweka muda wa kuchezwa soka ambao si mwafaka kwa washabiki kufuatilia kwenye televisheni.

 

Uamuzi wa kuahirisha soka unamaanisha kwamba hata fainali ya Kombe la Mfalme, maarufu kama Copa del Rey baina ya Barcelona na Athletic Bilbao iliyopangwa kufanyika Mei 30 imesitishwa.

 

Mechi muhimu za La Liga zilizobaki ni za Mei 17 baina ya Atletico Madrid na Barcelona huku  Espanyol wakiwa wamepangwa kucheza na Real Madrid.

 

Mei 23 pia kuna mechi kati ya Barcelona na Deportivo wakati Real Madrid ilikuwa wacheze dhidi ya Getafe.

 

Kadhalika La Liga watabaki bila bingwa na mechi zilizokuwa zimalizike mapema kupisha mashindano ya Amerika Kusini zitakwama.

 

Hayo ni mashindano yanayoshirikisha baadhi ya wachezaji walio La Liga, wakiwamo Neymar, Luis Suarez na James Rodriguez.

Inatarajiwa kwamba pande husika zitakaa chini kupata suluhu ya suala hili, lakini serikali inaweza kuziba masikio, maana ilikataa hata kusikiliza hoja za Catalan (iliko Barcelona0 kutaka kujitenga na Hispania.

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Barcelona wawachapa Bayern 3-0

Ni Yanga na Azam Afrika