in , , , ,

MSIMU MZURI KWA BARCA MPAKA SASA, ILA UNAWEZA KUHARIBIWA NA CHELSEA

Ni salama kusema kuwa FC Barcelona tayari wana uhakika wa makombe mawili msimu huu? Inaweza kuwa hivyo. Ndani ya dimba la Mestalla, jana waliwaondosha Valencia kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mfalme kwa mabao ya Philippe Coutinho aliyefunga bao lake la kwanza kabisa ndani ya uzi wa Blaugrana na lile la Ivan Rakitic.

Wanakwenda fainali ya tano mfululizo kupigania taji la nne mfululizo la Kombe la Mfalme kwa ushindi wa jumla wa 3-0 baada ya kuwa walishinda 1-0 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Nou Camp wiki iliyopita. Watavaana na Sevilla kwenye fainali itakayopigwa Aprili 21. Sevilla wao wamekwenda fainali kwa gharama ya Leganes waliowaondosha kwa jumla ya mabao 3-1.

Aprili mwishoni ni mbali na timu yoyote inaweza kubadilika kutoka kwenye kiwango bora mbaka kwenye kiwango duni na hata kinyume chake. Lakini kwa namna yoyote itakavyokuwa Sevilla wanahitaji kiwango kikubwa cha bahati kuweza kuwazuia Lionel Messi na wenzie wasinyanyue taji lao la nne mfululizo la Kombe la Mfalme.

Barcelona wana msimu mzuri mno mbaka sasa. Wakati Sevilla ndio pekee wenye nafasi ya kuharibu mipango ya Barcelona ya kushinda taji la Kombe la Mfalme, ni Atletico Madrid wanaoweza kupewa nafasi ya kuwapiku vinara hao kwenye ushindi wa Ligi Kuu ya Hispania msimu huu. Pengo la alama 9 ni kubwa kiasi ingawa halikatishi tamaa kiasi hicho kwa kuwa kuna raundi 16 zimesalia.

Wakati kwenye michuano ya nyumbani FC Barcelona wakionekana kuwa salama mno kipindi hiki, hali pengine ni tofauti kidogo kwenye michuano ya Ulaya. Chelsea wanaotajwa kuwa dhaifu kwenye siku za karibuni ni moja kati ya ndoto za kutisha mno kwa miamba wa Katalunya. Chelsea wanaweza kudhalilishwa na Bournemouth na Watford lakini wakaonehsa mchezo tofauti dhidi ya FC Barcelona.

Kwanini Chelsea wanaweza kuuharibu msimu wa Barcelona mapema? Ni swali gumu lenye majibu mepesi. Chelsea wanaweza kwa sababu wanaweza kufanya hivyo. Hawapo kwenye kiwango kizuri msimu huu na wameporomoka zaidi kwenye siku za karibuni lakini ifahamike kuwa morali ya mchezo watakayokuwa nayo kwenye michezo miwili dhidi ya Barcelona inaweza kuwapa faida kubwa.

Wachezaji wengi wa Chelsea wana msimu mbaya lakini wana silaha mbili za maana zinazoweza kuwafanya wazime makali ya Barcelona kwenye michezo itakayopigwa baadae mwezi huu na mwezi Machi. Eden Hazard na N’Golo Kante ndio silaha zenyewe. Ni wachezaji unaoweza kuwatumainia hata unapocheza na timu ya Lionel Messi aliye kwenye kiwango bora.

Hazard anaweza kuwaletea Barcelona madhara makubwa. Wakati ni wazi kuwa miamba hao lazima watatawala katika michezo yote miwili kwa kiasi kikubwa, lakini mipira michache itakayopata kumfikia Hazard upande wa kushoto inaweza kuwapa faida Chelsea. Barcelona wanaotumia muda mwingi kushambulia wanaweza kumuachia Hazard nafasi nzuri ya kuwasumbua walinzi wachache watakaokuwa nyuma mara kadhaa atakapopata mipira.

Jina la Hazard limo kwenye orodha ya wachezaji 6 wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwezi Januari wa Ligi Kuu ya England iliyotangazwa jana. Chelsea wanapitia kipindi kigumu, lakini sio Eden Hazard. Chelsea wanaweza kuwa hawaiogopeshi FC Barcelona lakini Hazard anaogopesha kwa kiasi fulani na anaweza kuwaharibia msimu.

N’Golo Kante anaweza kuwa sio yule wa msimu uliopita aliyewafunika zaidi ya wachezaji takribani 500 wa Ligi Kuu ya England na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa EPL. Lakini uwezo wake wa kunyang’anya mipira mguuni unaweza kuilinda vyema safu dhaifu ya ulinzi ya Chelsea hata dhidi ya timu ngumu. Anaweza kupunguza makali ya Ivan Rakitic na wenzie kwenye eneo la kiungo. Anaweza kumzuia Lionel Messi asizunguke sana na mipira.

Ni Wilfred Ndidi wa Leicester City na Idrissa Gueye wa Everton wanaomzidi Kante kwenye takwimu za kunyang’anya mipira mguuni mbaka sasa kwenye Ligi Kuu ya England. Kushindwa kwake kung’ara kwenye michezo michache iliyopita kunaweza kukudanganya kuwa hana jipya tena. Lakini Mfaransa huyu bado ni wa moto.

Itakumbukwa Chelsea walikwenda kupambana na Barcelona msimu wa 2011/12 kwenye hatua ya nusu fainali wakiwa kwenye hali kama waliyo nayo sasa. Na hawakuwa na wachezaji wa kutumainiwa kama walivyo Hazard na Kante wa sasa lakini waliwaondosha Barcelona. Michezo baina ya timu hizi ya Februari 20 na Machi 14 italeta majibu. Msimu mzuri wa Barcelona unaweza kuharibiwa mapema na Chelsea.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

YAFUATAYO NI MAKOSA YA BAKAYOKO

Tanzania Sports

SPURS ANA NAFASI YA KUSHINDA DHIDI YA ARSENAL