*Abramovich akimkataa ataenda klabu nyingine EPL
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho amesema hana nia ya kuondoka Stamford Bridge, lakini yupo tayari kufundisha klabu nyingine kwenye Ligi Kuu ya England (EPL).
Mourinho, 52, alirejea Chelsea 2013 baada ya kuwafundisha kuanzia 2004 hadi 2007 uhusiano wake na mmiliki, Roman Abramovich kuvuruhika, akaondoka kwenda klabu za nje ya EPL.
Amesema hayo baada ya kutajwa kuwa kocha bora England kwa msimu wa 2014/15 ambapo amewapa Chelsea ubingwa, akiziacha timu nyingine kwa mbali.
“Kuna uwezekano wa mimi kufundisha klabu nyingine, ndio, lakini nawapenda Chelsea na madhali nipo kwenye mikono ya Abramovich, basi nitakuwa hapa hadi wakati huo.
“Siku Abramovich akiona kwamba sifai tena kwa Chelsea, mimi bado nitataka kufanya kazi, ikiwezekana hapa hapa England pia,” anasema Mreno huyo mwenye maneno mengi, wakati mwingine ya kuudhi makocha wenzake.
Bosi huyu wa zamani wa Porto alipoondoka, Chelsea walianza msimu wa 2007/8 kwa tabu, mwenyewe akawafundisha Inter Milan alikotwaa ubingwa wa Italia, Kombe la Ligi na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mourinho aliondoka na kujiunga na Real Madrid, nako akatwaa ubingwa wa La Liga ya Hispania na kombe jingine, akikaa kwa miaka mitatu kabla ya kurudi Chelsea 2013.
Amesisitiza kwamba hata akipewa mara mbili ya mshahara wake wa sasa na klabu yoyote, madhali Abramovich bado anamtaka Chelsea, hataondoka. Amebainisha kwamba zile zama za klabu moja kama Manchester United au Chelsea kuitawala ligi kwa muda mrefu bila ushindani hazipo tena.
Mchezaji wa Chelsea na Timu ya Taifa ya Ubelgiji, Eden Hazard amechaguliwa kuwa mchezaji bora kwa msimu huu, ambapo awali alichaguliwa pia kuwa mchezaji bora na Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA).
Wengine waliokuwa wakiwania tuzo ya mchezaji bora ni wachezaji wenzake wa Chelsea, John Terry, Cesc Fabregas na Nemanja Matic. Kadhalika walikuwamo mshambuliaji wa Manchester City, Sergio Aguero, kipa wa Manchester United, David de Gea, mpachika mabao wa Tottenham Hotspur, Harry Kanena nyota wa Arsenal, Alexis Sanchez.