in , ,

MOURINHO ANAMTAZAMA SANCHEZ SISI TUNAMWANGALIA

Hapana shaka mwaka huu ulianza na mshindo mkuu, mshindo ambao ulitokea
katika jiji la Manchester na kusambaa duniani.

Kila sehemu duniani ƙkote watu wengi walikamatwa hisia zao kutokana na
usajili wa Alexis Sanchez.

Hiki ni kitu cha kawaida sana kwa klabu kubwa kama Manchester United,
klabu ambayo inajua kucheza na akili za watu ili wanufaike na biashara
yao ya mpira

Kwao wao mpira ni biashara kuanzia nje ya uwanja mpaka ndani ya
uwanja, ndiyo maana unaweza ukawaona hawachukui makombe makubwa kama
kombe la ligi kuu ya England lakini kwenye suala la utajiri ndiyo
klabu tajiri duniani.

Inajua namna ya kufanya biashara ndani pamoja na nje ya uwanja.

Pesa zao kwa Paul Pogba zilirudi kabla hata ya Paul Pogba kukanyaga
nyasi za Old Traford .

Walitengeneza mazingira ya kuuza jezi kabla zake kwa manufaa ya klabu
, na mazingira haya yalianza kutengenezwa kwa kulifanya jambo la Pogba
kuwa kubwa , kila mtu aliongelee watu watamani kuwa na jezi namba 6.

Pesa ikaingia kwenye akaunti zao, maisha yakaendelea mpaka yakafika
siku ambayo Alexis Sanchez alitakiwa kwenda Manchester United kutoka
Arsenal.

Hakuna hela waliyotoa kumnunua Alexis Sanchez zaidi ya kubadilishana
wachezaji, lakini kwao wao halikuwa jambo dogo.

Haikuwafanya wao wasiwe na uchungu kisa hawajatoa hela ya kumnunua.
Wakatengeneza mazingira mazuri, mazingira ambayo yatamvutia kila mmoja
na awe na shauku na Alexis Sanchez.

Mazingira haya yalimfanya Alexis Sanchez azaliwe upya na kuonekana
kuwa mkubwa zaidi ya yoyote kwenye ligi ya England.

Lilikuwa jambo la kushangaza kipindi Alexis Sanchez anaenda Manchester
United kukutana na shabiki wa Manchester United akimpandisha Alexis
Sanchez kwenye daraja la kina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo hii ni
kwa sababu ya mazingira yaliyotengenezwa na kitengo cha biashara ya
Manchester United.

Mazingira ambayo yaliongeza matamanio kwa mashabiki, wakajivunia kuwa
na Alexis Sanchez na kumuona moja ya nyota mkubwa kwenye sayari hii.

Jezi namba saba (7) aliyokabidhiwa ndiyo ikawa msumari wa mwisho
kwenye mioyo ya mashabiki wa Manchester United , matamanio ya kununua
jezi yake ikawa kubwa.

Mauzo ya jezi yake yalienda kwa kasi kubwa, Manchester United ikawa
imeshafanya biashara kubwa nje ya uwanja, macho na masikio ya wengi
wakawa wanasubiri namna ambavyo Alexis Sanchez atafanya vizuri ndani
ya uwanja.

Matamanio yalikuwa makubwa sana, kiasi kwamba kila shabiki alitamani
kila mpira uwe unamfikia Alexis Sanchez ili afanye mambo makubwa.

Mambo ambayo yalikuwa yanachagizwa kutokana na usajili wake kuwa na
nguvu pia na jezi yake namba saba ambayo iliwahi kuvaliwa na watu
wazito ambao walifanya mambo makubwa katika timu ya Manchester United

Miamba kama Brayn Robson “Captain Marvel”, Eric Cantona, David Beckham
na Cristiano Ronaldo waliwahi kufanya vitu vitakatifu wakiwa ndani ya
joho lenye namba 7.

Tangu 2009 , Cristiano Ronaldo alipovua Joho hilo, kila aliyekuwa
anajaribu kulivaa lilikuwa linampwaya.
Wengi walisubiri ni nani atakayeweza kulivaa joho hili aonekane
limemtosha ipasavyo, Alexis Sanchez alibeba matumaini mengi kwenye
hili.

Matumaini ambayo mpaka sasa yanaishi kwa sababu haimanishi
ameshashindwa kufanya vizuri na jezi hii, lakini matumaini ya
mashabiki yamepungua.

Mechi 9 akiwa na goli moja pamoja na pasi tatu za mwisho za magoli ni
jambo ambalo linaonesha mwanzo usio wa kishindo kwake.

Wakati mashabiki wanatamani kishindo ƙkikubwa kutoka kwa Alexis
Sanchez, Jose Mourinho anatamani kuona kishindo ƙkikubwa kutoka kwenye
timu yake.

Jose Mourinho anataka timu yote kwa ujumla ifanye vizuri, hata kama
mchezaji mmoja asipofunga cha muhimu kwake ni kuona mchango wa
mchezaji huo umesaidia kushinda mechi husika

Ndipo hapo matamanio ya kocha na mashabiki yanapotofautiana. Kocha
matamanio yake yanaongozwa na msukumo uliopo ndani yake, wakati
mashabiki matamino yao huongozwa na namna ambavyo wanataniwa na
wapinzani wao

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

KAZI KUBWA IKO KWA MOURINHO KULIKO KLOPP

Mkapa Stadium

TUNASHINDWA KUUFANYA UWANJA WA TAIFA KAMA SEHEMU YA UTALII?