BODI ya Wakurugenzi ya Chelsea ikiongozwa na mmiliki, Roman Abramovich
wamekuwa katika majadiliano juu ya hatima ya kocha wao, Jose Mourinho.
Taarifa zinasema kwamba kichapo cha 2-1 kutoka kwa Leicester Jumatatu
hii kimemfanya mmiliki kufikiria upya iwapo kuna haja ya Mourinho
kubaki klabuni hapo, au amwondoshe na sasa amekuwa akitafuta mawazo
juu ya kipi cha kufanya.
Abramovich amekuwa muda wote akidaiwa kueleza kwamba anamuunga mkono
kocha huyo aliyerejea kwa awamu ya pili na kuwapa Chelsea ubingwa
msimu uliopita. Sasa na pointi 15 wakiwa katika nafasi ya 16 kwenye
msimamo wa ligi baada ya kupoteza mechi tisa kati ya 16 walizocheza.
Hakuna uhakika iwapo Mourinho atakuwa kocha wa Chelsea Jumamosi hii
watakapovaana na Sunderland na baada ya hapo watacheza na Watford
kabla ya kuwakabili Manchester United. Chelsea wapo pointi 20 nyuma ya
vinara wa ligi – Leicester na pointi 14 nyuma ya kuweza kufuzu kwa
Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mourinho alitangulia kusema kwamba hawataweza kutetea ubingwa wao,
lakini kisha akasema itakuwa ngumu kushika nafasi nne za juu lakini
sasa lugha inayozungumzwa Stamford Bridge ni kipi cha kufanya kuwazuia
wasishuke daraja.
Hata hivyo, Mourinho na msaidizi wake, Rui Faria waliongoza mazoezi ya
Chelsea Jumatano alasiri akitafuta kuwarejeshea makali nyota wake
tayari kupambana na ‘vibonde wenzao’ Sunderland wikiendi hii.
Baadhi ya yanayojadiliwa, inaaminika ni iwapo kuna haja ya kuachana na
Mourinho anayesifika kwa mbinu mpya anazoweza kuja nazo lakini pia
kuzingatia jinsi wamekuwa wakididimia bila mabadiliko yoyote klabuni .
Inadaiwa pia kwamba baadhi ya wachezaji wanamlaumu kwa kauli yake ya
Jumatatu kwamba kuna usaliti wa kazi yake kutoka kwa wachezaji, huku
wachezaji wenyewe kwa wenyewe pia wakitupiana maneno kwa kushindwa
kuonesha kiwango.
Ikiwa wataachana na Mourinho, Chelsea, na kwa usahihi zaidi,
Abramovich, atatakiwa kumlipa Mourinho fidia kubwa, kwani ni majuzi tu
amesaini mkataba wa miaka minne na analipwa mshahara wa pauni 250,000
kwa wiki.
Zipo taarifa kwamba wamekuwa wakifikiria kumchukua Guus Hiddink kama
kocha wa mpito kama ilivyokuwa zama za Rafa Benitez ili mwisho wa
msimu waangalie iwapo watampata Pep Guardiola anayedaiwa kwamba
ataondoka Bayern Munich.
Makocha wengine wanaofikiriwa ni wao wa zamani, Carlo Ancelotti
aliyepata kufukuzwa hapo na Real Madrid na sasa hana kazi wakati
mwingine anayefikiriwa ni yule wa Atletico Madrid, Diego Simeone
lakini kwa sasa si rahisi kumpata.
Wazo jingine ni kumpatia Mourinho fedha kununua wachezaji wapya
dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa hivi karibuni. Kocha huyo
anadaiwa kuwaambia nyota wake kwamba alitakiwa kuuza baadhi yao
kiangazi kilichopita.