in ,

MOHAMED SALAH WEKA UFALME WAKO MBELE YA IAN RUSH

Mohamed Salah thanks to Allah for every goal he scores for Liverpool.

Mwishoni mwa juma hili kutakuwepo na derby ya kirafiki, derby ambayo
mashabiki wa timu zote mbili hukaa pamoja na kushangilia pamoja bila
vurugu yoyote.

Hakuna uhasama kwenye Merseyside derby, derby ambayo mfalme wake ni
Ian Rush, magoli 25 aliyoyafunga kwenye derby hii yanamfanya kuwa
mchezaji aliyefunga magoli mengi kwenye mechi ya Liverpool na Everton.

Uimara wa miguu yake ulifanikisha kuweka rekodi hii, rekodi ambayo
hakutosheka nayo katika maisha yake ya mpira, akaamua kuwekeza juhudi
za ufungaji mpaka akaifungia Liverpool magoli 346 magoli ambayo
yalimfanya kuwa mfungaji bora wa wakati wote wa Liverpool mbele ya
Roger Hunt.

Uhai wa soka wa Roger Hunt ushafikia kikomo, hawezi tena kuifikia au
kuivunja rekodi ya Ian Rush, kinachobaki ni pengo kubwa la magoli 60,
magoli ambayo hatoweza kuyafikia tena kwa sababu kwa sasa viatu vyake
vimezeeka.

Viatu vipya ndivyo vinavyofikiriwa kufikia rekodi ya Ian Rush,
tulitamani kumuona Michel Owen akifika lakini pesa za Real Madrid
zilituharibia matamanio yetu.

Siku zilipozidi kukimbia zilifanikiwa kumfikia Fernando Torres ambaye
tulimuona anaweza akafikia rekodi ya kina Ian Rush na Roger Hunt,
lakini kama ilivyokuwa kwa Michel Owen, pesa tamu za Chelsea
zikaharibu kila kitu tulichokuwa tunakifikiria.

Tulifikiria Liverpool itakuwa timu ya kupigania makombe makubwa tena,
irudi kwenye zama zake ili wachezaji nyota waweze kubaki ndani ya timu
na kuvunja rekodi za watu wengi, lakini ilikuwa tofauti utajiri wa
makombe ya Barcelona ulimshawishi Luiz Suarez kuondoka Anfield.

Anfield ƙlikawa daraja la wachezaji nyota kupita na siyo kukaa tena.
Pesa na Makombe yakawa yanafupisha safari ya wachezaji nyota waliokuwa
wanaibuka Liverpool.

Maumivu yakawa ndani ya mashabiki wa Liverpool, hawakuwa na cha
kufanya zaidi ya kukubaliana na hali. Mwenendo wa timu yao ulikuwa
mbovu.

Hata alipoondoka Philipe Countinho watu walisonya sana, wakatukana
sana , wakachoma jezi yake lakini vyote hivo havikutosha kufuta ukweli
kuwa Philipe Countinho alikuwa ameshahama Liverpool na kuipenda jezi
ya Barcelona.

Inawezekana Mohamed Salah alitumika kama mtu wa kuwasahaulisha maumivu
ya kuondokewa na Philipe Countinho.

Magoli yake yalikuwa leso ya kufuta machozi ya mashabiki wa Liverpool,
usoni mwao wakawa na tabasamu pana lakini tabasamu hili ni la mashaka
kwa sababu hawajui kama Mohamed Salah atatumia Anfield kama daraja au
kama makazi ya muda mrefu.

Makazi ambayo yatamfanya awe mfalme mpya pale kwa sababu ana viatu
vipya vinavyoweza kufikia rekodi za kina Ian Rush na Roger Hunt.

Ian Rush
Ian Rush

Watu watakukumbuka kwa alama ambazo umeacha sehemu fulani, Ian Rush na
Roger Hunt waliwahi kuacha alama za kufunga magoli 40 ndani ya msimu
mmoja, alama ambayo Mohamed Salah anaelekea kuifikia.

Magoli 37 mpaka sasa tena katika msimu wake wa kwanza na Liverpool,
hii ni dalili tosha anaweza kufikia alama nyingi zilizowahi kuwekwa na
Ian Rush pamoja na Roger Hunt.

Kinachotia kigugumizi ni hii hali iliyopo Liverpool, wachezaji nyota
wengi huitumia Liverpool kama sehemu ya kupitia na siyo sehemu ya
kukaa.

Mohamed Salah ataweza kukaa Liverpool muda mrefu na kujiwekea ufalme
wake wa kudumu? Ana ubavu wa kuikataa Ofa za Barcelona na Real Madrid
zitakapokuja mezani kwake? Timu ambazo zinaweza kumpa uhakika wa
kushinda klabu bingwa ulaya? Timu ambazo zinaweza kusukuma mafanikio
yake binafsi kwenye tunzo mbalimbali?

Haya ni maswali magumu na mazito, maswali ambayo yanazika matamanio
yangu ya kumuona Mohamed Salah alipowahi kufikia Ian Rush na Roger
Hunt

Natamani sana Mohamed Salah aamini ninavyoamini mimi kuwa popote
unaweza ukapafanya pawe nyumbani kwako penye furaha.

Uwezo wake uliopo ndani ya miguu yake ni silaha tosha ya kuweka furaha
moyoni mwake, kitu kizuri yuko chini ya kocha mshindi Jurgen Klopp, ni
rahisi kwake kupafanya Liverpool kuwa sehemu yenye furaha na kufikia
walipowahi kufika kina Roger Hunt na Ian Rush.

Report

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya [email protected]

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote
Tanzania Sports

Insta ya Cristiano Ronaldo imenifanya nimkumbuke Ngassa na Kaseja

Tanzania Sports

MAN CITY v UNITED: DHAMIRA YA KUWEKA REKODI DHIDI YA HITAJI LA KULINDA HESHIMA