Kombe la dunia la mwaka 2014 ilionekana ni timu bora, timu ambayo ilifanikiwa kufika katika hatua ya fainali na ikafungwa goli moja na Ujerumani katika mchezo wa Fainali.
Wanaenda Russia, ila safari hii kuna ugumu katika njia zao kwa sababu kuanzia katika mechi za kufuzu wameonekana kama timu ambayo haina ushindani mkubwa kama wa mwaka 2014 nchini Brazil. Je wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri kama walivyofanya katika kombe la dunia la mwaka 2014?
Kwangu Mimi ninavyoona nafasi ya Argentina kufanya vizuri katika kombe hili dunia ni finyu sana kwa sababu zifuatazo.
Kuna umbo moja ambalo linaonekana katika kikosi cha timu ya Taifa ya Argentina, nalo ni umbo la ubaunsa. Kikosi cha timu ya Taifa ya Argentina kina umbo la ubaunsa yani juu wamejaa afu chini wameisha, wana wachezaji nyota katika eneo la mbele lakini katika maeneo mengine hawana wachezaji nyota.
Kwa kifupi timu yao ya Taifa haina uwiano mzuri kwenye maeneo muhimu ndani ya uwanja.
Eneo la mbele lina wachezaji nyota wengi kama kina Sergio Aguero, Gonzalo Higuain, Paulo Dybala, Lionel Messi, Angela Di Maria.
Lakini katika idara zingine hazina wachezaji ambao ni wa daraja la juu. Mfano eneo la golikipa lina makipa ambao hawapewi nafasi kubwa sana katika vilabu vyao, mfano Sergio Romeo na Caballero ambao hawana nafasi kubwa katika vikosi vya Manchester United na Chelsea.
Katika safu ya ulinzi wanabeki wazuri wa eneo la katikati kama Fazio, Nikolas Otamendi. Lakini mabeki wao wa pembeni hawana ubora ya kuleta uwiano wa kushambulia na kuzuia.Hata viungo wao siyo viungo ambao wanaweza kuleta uwiano kwenye timu katika eneo la kuzuia na kushambulia.
Baadhi ya wachezaji kupata majeraha kutapunguza kasi ya Argentina?
Golikipa wao chaguo la kwanza Sergio Romeo amepata majeraha ambayo yatamfanya asiwepo katika michuano hii, hivo watamtegemea Caballero ambaye hata umri unamtupa, miaka 36 na ikizingatia pia hapati nafasi katika timu ya Chelsea, hii inaweza kusababisha kiwango chake katika michuano hii ya kombe LA dunia kutokuwa kizuri.
Majeraha ya Manuel Lazini yatawaathiri pia, ambaye alionekana kama kiungo ambaye anaweza kuleta uwiano mzuri eneo la katikati lakini amepata majeraha siku chache kabla ya kwenda kombe la dunia.
Kuna madhara ya timu kutengenezwa kwa kumzunguka Lionel Messi?
Tumeona katika timu Barcelona ambavyo ilishindwa kuweka rekodi ya kumaliza msimu bila kufungwa kwa sababu ya kukosekana kwa Lionel Messi.
Messi ndiye mtengeneza nafasi, mpiga pasi, mpiga faulo, mpiga kona, mkokota mpira, mfungaji, mchezeshaji timu kwa kifupi messi ndiye kila kitu , akikosekana chakula kinachoitwa Argentina hukosa ladha.Hivo Lionel Messi ikibanwa ni sawa imebanwa Argentina, hawana njia mbadala. Pamoja na kwamba wana wachezaji wengi nyota hasa hasa eneo la mbele lakini timu haijajengwa kucheza kitimu.
Wapinzani wake Argentina watakuwa kikwazo kwa Argentina kufanya vizuri kama mwaka 2014?.
Hapana shaka katika michuano hii ya mwaka huu wa 2018 Kuna timu imara zaidi kuzidi Argentina katika michuano hii ya kombe la dunia, mfano Ujerumani, Brazil, Hispania na France. Hawa wana vikosi imara kuzidi Argentina na wamekuwa na kiwango kizuri kwa siku za hivi karibuni kuzidi timu ya taifa ya Argentina.
Kuwa na wachezaji ambao wanaonekana wana umri mkubwa inaweza kuwa na madhara kwa timu ya taifa ya Argentina?
Wanaweza kupata madhara hasi sana kwa sababu ya kuwa na wachezaji ambao kasi yao imepungua kutokana na umri wao.
Wachezaji wa eneo la mbele wana wastani wa kuwa na miaka 30 kila mmoja. Hii inaweza kupunguza kasi katika timu na kuwafanya wawe na wakati mgumu wanapokutana na timu ambazo zimejaza vijana wenye umri mdogo na wenye kasi.