KUBEBA jukumu la kufundisha timu iliyoshuka daraja ni uamuzi mzito sana. ni uamuzi ambao unajumuisha matumaini makubwa kwa washabiki na viongozi kuwa timu yao itarudi Ligi Kuu England kama walivyozea. Leicester City ni miongoni mwa timu kongwe katika historia ya mpira wa miguu. Ni timu ambayo miaka kadhaa iliyopita iliwashangaza miamba ya England na mashabiki kwa kutwaa taji la Ligi Kuu nchi hiyo ikiwa chini ya kocha Claudio Raineri. Hii ni timu iliyozalisha wachezaji wengi kama vile Ngolo Kante, Riyaz Mahrez na wengineo.
Hii ni timu ambayo imesisimua misimu kadhaa kutokana na matokeo ya kushangaza ikiwemo kuzinyanyasa timu kubwa kwenye Ligi Kuu.
Hata hivyo msimu uliomalizika Leicester City imeshuka daraja hadi la kwanza ikiwa chini ya kocha Ruud Vanm Nistelrooy. Kocha huyo aliingia Leicester City kuokoa jahazi lakini timu hiyo ilikuwa kwenye nafasi ngumu kuepuka kushuka daraja hivyo kushindwa kuibakiza. Ruud Van Nistelrooy ni mshambuliaji mkongwe wa zamani wa Manchetser United na kocha wa zamani wa PSV ya Uholanzi ambako alifanya vizuri akiwa mwalimu wake.
Kutokana na kazi nzuri aliyeofanya akiwa PSV, alichukuliwa na Man United kuwa kocha msaidizi. Hata alipofukuzwa kocha mkuu, Eric Ten Hag uongozi wa timu hiyo ulimkabidhi timu Nistelrooy kwa muda mfupi hadi mkataba wake ulipomalizika. Lakini kuondoka kwake Leicester City kulikuwa na maana moja tu; hawezi kufundisha timu inayocheza lIgi daraja la kwanza na pia imetoa fursa kwa kocha mwingine kuja kuifundisha timu hiyo kongwe.
Kocha huyo ni Marti Cifuentes ambaye ameteuliwa kuongoza jahazi la Leicester City na kuirudisha Ligi Kuu England. Tangu uteuzi wake maelfu ya mashabiki wa kandanda wanatamani kumfahamu kocha huyo ni nani ametokea wapi na amefanya kazi hiyo sehemu zipi na mafanikio yake yakoje.
MARTI CIFUENTES NI NANI
Marti Cifuentes aliangukia kwenye mapenzi ya mpira wa miguu akiwa na umri wa miaka mitano tu na tangu hapo hajawahi kuacha kupenda mchezo huo. Alianza kazi ya ukocha miaka 20 iliyopita, akiwoangoza wachezaji chipukizi ambao hakupihana nao umri. Wengi wa wachezaji hao hakupishana nao umri, labda ungesema ni hawakuachana sana rika lao, lakini aliwaongoza kiufundi na kuhakikisha anakuwa kocha mzuri kwao. Miongo miwili baadaye alifanikiwa kufundisha timu mbalimbali katika nchi za Hispania, Norway, Denmark, Sweden, na sasa ameingia katika soka la England akiwa amepokea kibarua cha kuinoa Leicester City.
Marti ni kocha ambaye anapenda kukaa muda mrefu kuipanga timu na kuunda mwelekeo ambao utaleta matunda kwa timu husika. ni aina ya makocha ambao hutumia muda mwingi kuunda timu kabambe ambayo inaleta ushindani.
Hivyo yeye si kocha wa muda mfupi, kwani anapenda kutengeneza utambulisho wa timu yake katika uchezaji kitu ambacho kinahitaji muda mrefu zaidi.
Akiwa kocha wa Queens Rangers (QPR) alichukua timu hiyo ikiwa na pointi 6 katika msimamo wa ligi, akashinda mechi 8 na kutoka sare 4 kati ya michezo 14 na kuiondoa katikahatari ya kushuka daraja. Lakini lengo lake halikuwa kuinusuru kushuka daraja bali kuhakikisha timu hiyo ina utambulisho wake kiuchezaji, kimfumo na kuwafurahisha mashabiki wa soka England.
Mfumo wake wa ufundishaji umetokana na falsafa ya Cruyffismo, ambayo iliibuliwa na Johan Cruyff.
Falsafa hiyo inaifanya timu icheze kwa pasi nyingi kutegemea na nafasi za wachezaji pamoja na kuunda kiungo chenye kazi ya ubunifu wa kurahisha upatikanaji wa ushindi. Falsafa hiyo ilitumika zaidi kwenye dimba la Camp Nou miaka 1990 ambako Barcelona walikuwa wanacheza soka maridadi na kuwa kivutio cha wengine.
Falsafa hiyo ilimvutia Marti Cifuentes na kuamini ndiyo sahihi katika ufundishaji wake wa soka kuanzia kutanua kiufundi, muundo wa wachezaji wanaohitajika kutekelezajukumu ya falsafa yenyewe na mashambulizi mfululizo yenye kuwapa uhuru wa kiubunifu katika lango la adui ni mhimili mkubwa kwenye ufundishaji wake kila mahali alikopita.
Marti anaamini kuwa kila timu inatakiwa kuwa na mfumo rasmi wa kiuchuezaji, na wachezaji wanapaswa kufahamu namna ya kutumikia mfumo huo pasipo kuharibu vipaji vyao.
Akiwa nchini Sweden alifundisha klabu ya Hammarby, Sandefjord (Norway), QPR (England) na amekuja Leicester City kutengeneza mfumo madhubuti na kuendeleza wachezaji kutoka ngazi ya chini au wale wenye vipaji ambao hawajapata nafasi ya kutambulika zaidi duniani.
Kwa umahiri wake alisaidia kupatikana kwa maendeleo ya soka nchini Sweden na kuondokana na mfumo wa 4-4-2 na kuanza kucheza mifumo ya kisasa zaidi yenye manufaa kwa timu.
Cifuentes hajawahi kuondoka kwenye klabu yoyote kwa sababu ya matokeo mabaya. Kama anaondoka kwenye klabu anayofundisha ni kwa sababu ya kutothaminiwa an kutoelewana kati yake na viongozi w aklabu husika. ni kocha muungwana ambaye hakubali kuyumbishwa kwneye kazi na imani yake katika mfumo w aufundishaji wa soka kwenye klabu yoyote.
Lililo muhimu kwake ni kutengeneza mfumo mzuri wa kuipa mafanikio klabu anayofundisha. Kukuza wachezaji wenye vipaji na kutambulika zaidi na zaidi kuhakikisha anatengeneza timu sio kutegemea ubora wa mchezaji mmoja mmoja. Mwisho anapenda kuwashirikisha mashabiki kwenye kila hatua na kuwaambia umuhimu wa kile kinachofanywa, jambo ambalo limempa idadi kubwa ya watu wanaompenda kutokana na kazi hiyo. Huyo ndiye Marti Cifuentes kocha mpya wa Leicester City.


Comments
Loading…