in , , ,

Mancini kaondoka na rekodi

Hatimaye vumbi la miezi kadhaa juu ya kufutwa kazi au la kwa Kocha Mkuu wa Manchester City, Roberto Mancini limetulizwa na wamiliki wa Kiarabu kwa kumfukuza kazi Mtaliano huyo.
Sababu kubwa wanayotoa ni kwamba ameshindwa kutimiza malengo aliyowekewa na bodi ya wakurugenzi, na yeye mwenyewe amekaririwa akisema kwamba hatua hiyo ni jambo la kawaida kwenye soka.
Mancini mwenye umri wa miaka 48 amepoteza kazi yake, licha ya rekodi kubwa aliyoweka mwaka jana ya kuwapatia City ubingwa wa England kwa mara ya kwanza katika zaidi ya miaka 40. Tatizo kubwa katika ufikiaji malengo aliyowekewa inaonekana ni mawasiliano na uhusiano, doa kubwa zaidi la karibuni kufungwa na wanyonge Wigan kwenye fainali ya Kombe la FA.
Inaelezwa kwamba pamekuwapo mpasuko kati yake kwa upande mmoja na wachezaji, viongozi wenzake na pia bodi, ambapo uhusiano haukuwa mzuri na mawasiliano yalilega lega au huenda hayakueleweka vyema. City wanasema kuondolewa kwake licha ya kazi nzuri kumefanywa baada ya kuangalia ujumla wa mambo katika muda aliokuwepo.
Pamoja na mambo mengine, Mancini alipata kuzikunja na Mtaliano mwenzake, Mario Balotelli na kukosana na Carlos Tevez akidai alikataa kupasha ili aingie uwanjani kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Amewahi pia kukosana na golikipa namba moja, Joe Hart kwa kumzodoa hadharani juu ya uzembe wake uliosababisha mabao. Nahodha wa timu, Vincent Kompany amekuwa akipinga kwamba kuna tatizo kwenye timu.
Mancini pia ameshindwa kutetea kombe alilotwaa kwa tofauti ya mabao mwaka jana katika mechi ya mwisho wa msimu, ambapo ameachwa na mabingwa wapya, Manchester United kwa pointi 12 hadi alipokuwa anafukuzwa. Aibu zaidi ilikuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo kati ya mechi 12, walishinda tatu, wakatoka sare nne na kufungwa tano na kutoka kabla ya hatua ya makundi.
Hata hivyo, kati ya timu 20 za Ligi Kuu, Mancini alifanikiwa kuwapeleka City juu ya nyingine 18, City wakishika nafasi ya pili, wameshafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya na wana rekodi nzuri ya kutofungwa mechi, japokuwa walipoteza pointi zao kwenye sare. Mancini analaumiwa pia kwa kushindwa kuendeleza vipaji vya chipukizi, wakati yeye akiilaumu bodi hadharani kwa kutosajili nyota wa kutosha.

DALILI ZA KUONDOKA KWAKE ZILIANZA MAPEMA

20130511-223648.jpg

Dalili za kuondoka Mancini zilianza mwaka jana, baada ya bilionea wa Emirates kumwajiri aliyekuwa mkurugenzi wa ufundi wa Barcelona, Txiki Begiristain kuwa mkurugenzi wa soka kusimamia usajili wa wachezaji wakati Ferran Soriano alichukuliwa Nou Camp pia na kufanywa ofisa mtendaji mkuu wa City, na hawakwenda vizuri sana na Mancini.
Mtu anayetajwa kuwa atamrithi Mancini ni kocha wa Malaga ya Hispania, raia wa Chile, Manuel Pellegrini, ambaye katika mazingira ya kutatanisha alikanusha kuwa na mpango huo, japokuwa alisema wamekubaliana na Malaga asizungumze chochote.
Vyombo vya habari vilishatangaza jana jioni kwamba Mancini aliyekuwa na timu jijini London kwa mazoezi angeendelea na kazi yake kwenye mechi dhidi ya Reading Jumanne hii, lakini usiku ikatangazwa kwamba amefukuzwa.
Pamoja na kufanya vibaya Ulaya, City wana kundi la wachezaji walionunuliwa kwa bei kubwa, chini ya Mancini mwenyewe na mtangulizi wake, Mark Hughes, hivyo labda tatizo lingeweza kuwa mtu wa kuunganisha vipaji na uzoefu wao kama timu.
Katika misimu miwili iliyopita, Manchester City wametumia dola milioni 230 kununua wachezaji, ambapo pamoja na kutwaa ubingwa wa England, wamiliki na wadau wengine waliona ndio mwanzo wa kupaa kwa vijana hao wa Eastlands, ambao bili yao ya mishahara inatisha. Walitupwa nje ya mashindano ya Ulaya mapema mno.
Nyongeza ya wachezaji waliotarajiwa kuwapaisha zaidi kwenye soka nyumbani na kimataifa ni Jack Rodwell, Maicon, Scott Sinclair, Matja Nastasic na Javi Garcia lakini ama hawakuonyesha cheche, hawakuchezeshwa ipasavyo au kukawa na majeruhi.
Wapinzani wa Mancini wanamnyooshea kidole kuwa ndiye tatizo, wakimtaja pia kwa jinsi mafanikio yake hayakufika mbali alipowafundisha Inter Milan ya Italia. Hata hivyo, pamoja na matatizo yake, wapo wengine wanaodhani angepewa muda zaidi au walau kumalizia msimu huu. Lakini kwa watoaji fedha, ni vigumu kuvumilia hasara ya manoti hayo.

MAKOCHA WENGINE WALIOSHINDWA KUTIMIZA NDOTO

IMG_03921-e1353885585607

Mancini alisema mapema kwamba kutaka Manchester City wafanye vyema Ulaya ilikuwa ndoto ya mapema mno, na kwamba walihitaji muda zaidi. Si Man City peke yao waliofanya vibaya Ulaya, wapo wengine, ambapo wakati mwingine huwa ni vigumu kuelewa kama kosa ni la kocha, wachezaji au wamiliki wa klabu.
Kila mwanzo wa msimu klabu na wadau wao huwa na ndoto ya mafanikio, na kadiri ligi na mashindano mengine yanavyoendelea, mbivu na mbichi hubainika, na wachambuzi kuanza kutafsiri nani anakwenda sawa, nani kapotea na kipi kifanyike kuiweka mambo sawa. Si kila anayetoa fedha nyingi za usajili au mishahara atalipwa kwa ushindi na vikombe, lakini hayo ndiyo matarajio.

FERGUSON ALIKUWA NA MAPUNGUFU PIA

Alex Ferguson wa Manchester United anatajwa kuwa kocha mashuhuri zaidi katika soka ya Uingereza, ambaye katika miaka yake 26 Old Trafford ametwaa mara mbili Kombe la Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, kadiri muda ulivyokwenda, na kwa jinsi alivyokuwa maarufu, mambo yalianza kumwendea ndivyo sivyo, na ndiyo maana hata Arsene Wenger wa Arsenal aliwaambia wafanyakazi wenzake kwamba anadhani huu ungekuwa msimu wa mwisho wa Sir Alex.
Heshima ya Manchester United ilifika mahali ikaanza kukatikia kwenye maji yanayozunguka Uingereza tu, ambapo hawakufua dafu Ulaya, licha ya kutumia dola milioni 103 majuzi kupata wachezaji watakaowapeleka vizuri, kama Robin van Persie na golikipa David De Gea.
Tuliona wote, United mwaka jana walirudi nyumbani katika hatua ya makundi wakijisikitikia wenyewe kwa uchovu wao na mwaka huu hawakuweza hata kufika robo fainali. Fergie alionekana kushitushwa sana na kufungwa na Real Madrid nyumbani kwake Manchester, na kilichofuata muda si mrefu ni kutangaza kujiuzulu.

LUCIANO SPALLETTI ALIPEWA MAPESA AKAKWAMA

Mtaliano Luciano Spalletti alijiunga na klabu ya Zenit St. Petersburg ya Urusi mwaka 2009, akishangiliwa na kila mtu kwa ahadi zake na jinsi alivyoonekana kuwa tayari kuwaletea mataji mengi.
Alimwagiwa pesa kiasi cha dola milioni 140 mwaka jana tu kwa ajili ya kuongeza jeuri ya wachezaji, ambapo alisajili kadhaa, wakiwemo Mbrazili mzuri kwenye ufungaji, Hulk na Alex Witsel wa Ubelgiji.
Hakuna walichofanya Zenit, walijitutumua kidogo kwa ushindi wa mechi mbili kati ya sita za makundi, Hulk akafunga kabao kamoja tu kwenye mechi tano, timu ikafungwa jumla ya mabao tisa, wakalala. Leo anatajwa huenda akajiunga Chelsea, Roma au AC Milan.

KAFARA YA ROBERTO DI MATTEO ILILIPA?

Roberto Di Matteo aliwashangaza wengi alivyokiongoza kikosi alichoachiwa kama kaimu kocha kwa kusonga mbele vizuri kwenye EPL na Ulaya baada ya kuondoka Andre Villas-Boas na japokuwa walikosa nafasi nne za juu mwaka jana, walitwaa kombe la Ulaya na kuwa tiketi ya kushiriki msimu huu.
Lakini kama ilivyokuwa kwa Mancini, Matteo aliweka rekodi ya kutwaa kombe hilo Chelsea kwa mara ya kwanza, lakini pia msimu huu akaweka rekodi chafu ya bingwa mtetezi kutolewa katika hatua ya makundi.
Mmiliki Mrusi, Roman Abramovich hakuwa na subira, kabla hata Matteo hajatua London kutoka Italia walikopigwa, alitangaza kupitia watu wake kwamba kocha amefukuzwa mara moja, akamchukua aliyekuwa kwa mahasimu wao Liverpool zamani, Rafa Benitez.
Hata hivyo, Mhispania huyu anaondoka hivi karibuni, na atakayechukua nafasi yake anatarajiwa kuweka jitihada ili mwakani wafanye vizuri zaidi, sio kama mwaka jana na mwaka huu ambapo nafasi ya nne inapiganiwa mpaka dakika ya mwisho. Ikumbukwe kwamba katika miezi 12 iliyopita, Abramovich amemwaga dola milioni 153 kuongeza nguvu ya wachezaji, lakini hakuna kikubwa kinachoonekana kuwazidi wengine.

Enhanced by Zemanta

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

Fergie aagwa, Newcastle, Norwich zaokoka

Arsenal jeuri