in , , ,

MANCHESTER UNITED 1 – TOTTENHAM – 0

*Tulichokiona Old Trafford*

 

Tottenham waliuanza mchezo kwa kujiamini na wakafanya mashambulizi kadhaa ndani ya dakika za mwanzoni ila hakukuwa shuti lililoweza kuzaa bao

Manchester United hawakuweza kupiga shuti lolote mbaka kufikia dakika ya 20 ya mchezo.

 

Hata hivyo waliweza kuwadhibiti vyema viungo wa Tottenham na hatimaye wakashindwa kuitoa mipira kutoka kwenye nusu yao na kuisambaza kwa washambuliaji.

 

Mbinu hii nafikiri ndio ilikuwa siri kubwa ya ushindi wa Manchester United kwenye mchezo wa leo.

 

Kiungo Nabil Bentaleb alijikuta mara kadhaa akikosa mianya ya kusambaza mipira. Hili likamshinikiza kufanya kosa lililoigharimu timu yake kwenye dakika ya 21 ya mchezo.

 

Alipiga pasi ambayo viungo wa United waliiteka kabla haijamfikia mlengwa na kumsambazia Ashley Young aliyekuwa pembeni upande wa kulia.

 

Young akampigia Rooney krosi safi ya chini chini ambayo ilimfikia vyema kabisa.

 

Hata hivyo Rooney hakuweza kuitumia nafasi hii ya kujipatia bao lake la kwanza la msimu ambalo lingekuwa bao la kwanza la EPL msimu huu. Kyle Walker akakimbia alipokuwa Rooney na mpira.

Katika jitihada za kumzuia Rooney asiupige mpira ule langoni Walker akajikuta anausukuma kwenye nyavu za lango la timu yake. Bao hilo likawa bao la ushindi kwa Manchester United.

 

Hata hivyo Walker ni mchezaji ambaye ameonesha kiwango kuwazidi wachezaji wote wa Tottenham kwenye mchezo wa leo ingawa alifanya kosa hilo.

 

Baada ya mchezo Walker alisema, “Nilijaribu kuweka mguu wangu ili Rooney aupige badala ya mpira, ila kilichotokea ni bahati mbaya.”

 

Kabla ya kipindi cha kwanza cha mchezo kumalizika Manchester walipiga mashuti kadhaa kupitia kwa Mata na Memphis Depay lakini hayakuweza kuzaa matunda.

 

Kwenye kipindi cha pili wachezaji wa United waliendelea kuwazuia vizuri walinzi na viungo wa Tottenham na hatimaye wakashindwa kusambaza mipra kwa washambuliaji.

 

Kwenye dakika ya 53 kocha Mauricio Pochetino akaamua kumtoa Bentaleb na kumuingiza Mason. Huu ulikuwa uamuzi sahihi kwani Bentaleb hakuwa vizuri kwenye mchezo wa leo.

 

Alishindwa kung’ara dhidi ya mbinu za United waliokuwa wakimkaba mara moja kila alipopata mipira.

 

Kwa ujumla mchezo wa leo haukuwa wa kuvutia sana kwani washambuliaji wa timu zote mbili hawakufanya vizuri.

Nafikiri kille alichosema Rooney kabla ya mchezo kuwa kitu muhimu kwenye mchezo wa leo kilikuwa ni alama tatu na kuwa hawakukusudia kuonyesha soka safi kilitimia ndani ya dimba la Old Trafford.

 

Waliong’ara zaidi walikuwa ni walinzi wa timu zote mbili hasa walinzi wa pembeni.

 

Matteo Darmian alicheza vizuri mno hasa kwenye kipindi cha kwanza. Alipandisha vyema mashambuizi ya United kwenye upande wa kulia.

 

Pia Chris Smalling na Daley Blind walifanya kazi mzuri hasa kwenye kipindi cha pili. Waliwazuia ipasavyo Kane na wenzie na hawakuweza kuleta madhara kwenye ngome ya Manchester United.

 

Kwa upande wa Spurs Kyle Walker alikuwa vizuri siku ya leo. Pasipo kujifunga bao nafikiri angekuwa nyota wa mchezo.

 

Alimdhibiti vyema Young kwenye upande wake na United hawakuweza kufurukuta kabisa kwenye upande huo kwenye dakika zote za mchezo.

 

Mwisho wa mchezo Manchester United wakafanikiwa kuondoka na alama tatu muhimu kwenye mchezo wa ufunguzi.

 

Wamefanikiwa kujiepusha na matokeo mabaya kwenye mchezo wa kwanza ambayo yaliwapata msimu uliopita kwenye mchezo wa kwanza kama wa leo dhidi ya Swansea City.

 

Wengi walitarajia kuwa Harry Kane angekuwa kivutio Old Trafford leo hii. Hilo halikuweza kutokea.

 

Wayne Rooney alisema kabla ya mchezo kuwa nyota huyo wa Spurs atakuwa na msimu mzuri ila msimu huo mzuri usingeanzia leo. Na hicho ndicho kilichotokea.

Report

Written by Kassim

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

‘Wilshere ataendelea kuumia’

Chelsea waanza vibaya