* West Ham Yapeta
* Aston Villa yaona mwezi
Magoli mawili ya Wayne Rooney aliyofunga kwenye mchezo wa jana dhidi ya Newcastle United hayakuweza kutosha kuipatia ushindi Manchester United kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England uliopigwa hapo jana ndani ya dimba la St. James Park.
Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya mabao matatu kwa matatu ambapo bao lingine la United lilifungwa na Jesse Lingard huku Georginio Wijnaldum, Aleksandar Mitrovic na Paul Dummett wakifunga yale ya Newcastle United.
United ndio waliotangulia kupata bao mapema kwenye dakika ya 9 ya mchezo kupitia mkwaju wa penati baada ya mlinzi Chancel Mbemba kuzuia kwa mkono mpira wa kichwa uliopigwa na Marouane Fellaini.
Maamuzi hayo ya Mike Dean yalikuwa yenye utata kiasi cha kupelekea malalamiko kutoka kwa wachezaji wa Newcastle lakini malalamiko hayo hayakuweza kumzuia nahodha Wayne Rooney kuipatia United bao la kuongoza.
Mnamo dakika ya 38 ya mchezo kiungo mshambuliaji chipukizi Jesse Lingard akaipatia Manchester United bao la pili kabla ya kiungo Mholanzi Georginio Wijnaldum kuyafanya matokeo kuwa 2-1 dakika tatu kabla ya kipenga cha mapumziko kupulizwa.
Mwamuzi Mike Dean akazawadia mkwaju mwingine wa penati kwenye dakika ya 67, safari hii ikawa zamu ya Newcastle United kufuatia mshambuliaji Aleksandar Mitrovic kufanyiwa madhambi na Chris Smalling aliyemuangusha ndani ya eneo la hatari. Mserbia huyo aliuweka mwenyewe mkwaju huo ndani ya wavu na kuirejesha timu yake mchezoni matokeo yakiwa 2-2.
Wayne Rooney akawaweka tena United mbele dakika 11 kabla ya mchezo kumalizika akimalizia nafasi aliyoipata kufuatia shuti la Memphis Depay kuwagonga walinzi na kurerejea alikokuwepo nahodha huyo.
Ndani ya dakika za nyongeza shuti kali la Paul Dummett lililomshinda David De Gea likauamua mchezo huo kumalizika kwa sare ya mabao matatu kwa matatu. Matokeo hayo yanaifanya United kuwa na jumla ya alama 34 wakiwa kwenye nafasi ya 6 (wameshuka kwa nafasi moja).
Kwenye mchezo mwingine uliopigwa hapo jana West Ham wakitoka nyuma kwa bao moja walifanikiwa kusawazisha na kuwatandika AFC Bournemouth mabao matatu kwa moja na kupaa juu kwa nafasi moja ambao sasa wapo kwenye nafasi ya 5 wakiwa na alama 35.
Bao la Bournemouth lilifungwa na Harry Arter huku yale ya West Ham yakifungwa na Dimitr Payet aliyefunga lile la kusawazisha na Enner Valencia aliyefunga mawili yaliyoihakikishia West Ham ushindi mnono.
Aston Villa wao walipata ushindi kwa mara ya kwanza baada ya kuutafuta bila mafanikio kwenye michezo 16 mfululizo. Mlinzi Joleon Lescott aliifungia Aston Villa bao pekee la mchezo huo dhidi ya Crystal Palace. Ushindi huo unaifanya Aston Villa kuwa na jumla ya alama 11 lakini bado wakiwa wanaburuza mkia kwenye msimamo wa EPL.