in , , ,

Man U waendeleza mchezo wao

Man Utd waongeza "gap"

*Wachekelea kileleni kwa tofauti ya pointi saba

*Chelsea safi, Man City, Liverpool wacharazwa

Manchester United wanachekelea kileleni kwa tofauti ya pointi saba, wakirudia mchezo wa kuachia mabao, kusawazisha na kushinda.

Katika mechi za mzunguko wa 19, Man U walinusurika kufungwa na Newcastle, na alikuwa Javier Hernandez ‘Chicharito’ aliyeingia na kuokoa jahazi na kuwafikisha pointi 46.

Kocha Alex Ferguson aliyenusurika kuadhibiwa na FA kwa kuwasogelea na kuwakaripia waamuzi akipingana na uamuzi wao, anasema mchezo wao ni wa hadhi ya mabingwa.

Kwingineko Sunderland walikunjua makucha yao kwa mabingwa watetezi, Manchester City na kuwachapa bao 1-0, na kumtia simanzi kocha Roberto Mancini.

Hizo ni mechi zilizochezwa siku ya pili ya Krismasi, ambapo ni mapokeo katika Ligi Kuu ya England (EPL) kuwa na mechi nyingi siku hiyo.

Chicharito aliwapatia bao la nne United katika dakika ya 90, ambapo amefikia kupachikwa jina la ‘super sub’, kwa jinsi alivyokwishaingia mara nyingi na kuwanusuru vijana wa Old Trafford na kichapo.

Newcastle walikuwa wanapigania ushindi baada ya kufanya vibaya mechi kadhaa zilizopita, ambapo karika raundi ya 18 walifungua nyota njema kwa kuwachapa Queen Park Rangers (QPR).

United walitoka nyuma mara tatu ili kufikia ushindi huo, kwani Newcastle walicheza kwa nguvu, wakawa wa kwanza kupata bao, kabla ya kusawazishwa, lakini nguvu ya vijana hao wa St James’ Park ikaishia bao la tatu.

Mabao mengine ya United yalifungwa na Jonny Evans, Patrice Evra na Robin van Persie. Yale ya utangulizi ya Newcastle wanaofuliwa na Alan Pardew yalifungwa na James Perch, Papis Cisse na awali Evans alijifunga mwenyewe.

Kama Newcastle wangewafunga United, ungekuwa ushindi wao wa kwanza tangu 1972 katika dimba la Old Trafford.

Hii ilikuwa mara ya nane kwa vijana wa Ferguson kujikokota kutoka kufungwa, kusawazisha hadi kushinda, na kuweka hai matumaini ya kutwaa taji la 20 la EPL.

Kwa upande wa Sunderland, bao lake liliwekwa kimiani na winga Adam Johnson, akiifunga timu yake ya zamani, ambapo hakuamini kama bao lilitinga wavuni.

Mancini anatiwa katika wakati mgumu, kwani hivi karibuni ataanza kuwakosa wachezaji wake muhimu, Yaya na Kolo Toure wanaokwenda kujiunga na timu ya taifa ya Ivory Coast.

Chelsea waliendeleza wimbi la ushindi, japo kama ilivyotarajiwa walikabwa vilivyo na Norwich, na kupata bao moja lililopachikwa na Juan Mata.

Chelsea waliofikisha pointi 35 wamebaki nafasi ya tatu nyuma ya City wenye pointi 39 na bado wana mchezo mmoja mkononi, ingawa hautawasaidia kuzivuka wakiucheza sasa.

Nafasi ya nne imekwenda kwa Tottenham Hotspur,

Everton na West Bromwich Albion ambao wote wapo pointi mbili nyuma ya Chelsea.

Spurs walipanda baada ya kuwafunga Aston Villa mabao 4-0, Everton wakawatungua Wigan 2-1 na West Brom wakawashinda QPR kwa idadi hiyo hiyo ya mabao.

Kwa kufungwa huko, QPR wamerudi kuungulia mkiani mwa ligi, kwani wagonjwa wenzao Reading walitoa suluhu na Swansea, huku Southampton wakitoka sare ya 1-1 na Fulham.

Liverpool walionesha unyonge tena, baada ya kukandikwa mabao 3-1 na Stoke City. Kwa matokeo hayo, Wigan, Reading na QPR wapo kwenye eneo la hatari ya kushuka daraja.

 

Report

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

What do you think?

71 Points
Upvote Downvote

Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Loading…

0

EPL Leo…….

Walcott kiwango, kazi kwa Arsenal