KLABU ya Manchester City inasifika kuwa na fedha nyingi ambazo zinawafanya wasajili wachezaji kwa bei mbaya kila kona ya Dunia. Usajili wa kufuru pamoja na uwezo wa kutwaa mataji chini ya kocha mahiri umeifanya klabu hiyo kuwa miongoni mwa vigogo vya soka barani ulaya, lakini wamejikuta wakiingia katika anga za Simba na Yanga za Ligi Kuu Tanzania. TANZANIASPORTS inafahamu kuwa klabu ya Manchester City licha ya kusifiwa kwa uendeshaji wenye faida na viwango vya juu lakini nayo ina matatizo ambayo yameiingiza klabu hiyo kwneye kapu moja na vigogo wa soka barani Afrika, Simba na Yanga. Uamuzi wa waendeshaji wa Ligi Kuu England kuishughulikia klabu ya Manchester City umeibua mjadala na kuonesha taswira yao nyingine ya kushindwa kusimamia vema kanuni za soka.
Je, nini kimetokea?
Klabu ya Manchester City imeliwa faini ya pauni milioni moja na wasimamizi wa Ligi Kuu England kwa makosa mawili makuu. Kwa mujibu wa taarifa ya waendeshaji wa Ligi Kuu England wamesema kuwa klabu hiyo ilifanya kosa la kuchelewesha muda wa kuanza mchezo na kosa lingine ni kuchelewa kurudi uwanjani wakati wa kuendelea na kipindi cha pili cha michezo ya Ligi ya England.
Makosa hayo yamefanyikaje?
Kila timu inatakiwa kuzingatia muda wa kuanza mchezo, hivyo inapochelewesha kuna adhabu huwa inapewa timu husika, ambayo ni faini ya kulipa fedha. Klabu ya Man City imetuhumiwa kukiuka sheria za Ligi katika michezo 9 msimu uliopita. Uongozi wa Ligi Kuu umesema Man City walivunja sheria hizo ambazo zilikubaliwa na vilabu vyote vinavyoshiriki Ligi Kuu na ambavyo vilisaini kuwa kanuni za Ligi. Hata hivyo Man City imekutwa na hatia ya kuvunja sheria hizo katika kipindi cha mechi za mwezi Oktoba mwaka 2024 na Februari 2025.
Kwa mujibu wa kanuni za Ligi ya England, mchezo unaochelewa kuanza haupaswi kuwa zaidi ya dakika hata moja. Lakini Man City ilichelewa kwa dakika 2 na sekunde 24 katika mchezo wao na watani wa jadi Man United uliochezwa mwezi Desemba. Uongozi wa Ligi Kuu pia umeeleza kuwa Man City wamekiri makosa hayo na kukubali kulipia faini ya kuchelewa kuingia uwanjani katika mechi tajwa. Adhabu ya kuchelewa kuingia uwanjani maana yake Man City wanatakiwa kulipa jumla ya pauni milioni 1.08. Vilevile sheria hiyo inabainisha kuwa Man City wanatakiwa kulipa fedha hizo ndani ya siku 14.
Taarifa ya Ligi Kuu inasema nini?
Bodi ya Ligi Kuu England imeeleza kuwa, “kanuni inayohusiana na muda wa kuanza mchezo na muda wa kuingia uwanjani kipindi cha pili inasaidia kusimamia ushindani unawekwa katika kiwnago cha juu, na kila timu inatakiwa kuzingatia masharti na kusimamia taaluma inapotoa burudani kwa mashabiki na kuhakikisha matangazo ya Ligi Kuu yanatekelezwa kulingana na muda uliopangwa,”
Man City wamewahi kuadhibiwa msimu uliopita kwa kulipishwa faini ya pauni milioni 2 kwa kukiuka kanuni za Ligi mara 22 kuhusu muda wa kuanza mchezo na kurudi kiwanjani kipindi cha pili. Klabu hiyo kwa sasa ipo kwenye mashindano ya kombe la dunia la klabu na afisa mtendaji wao mkuu Ferran Soriano amesema anafurahishwa na mashindano hayo ambayo ynahusisha timu 32 na kutangaza mchezo wa soka katika ulimwengu mzima. Afisa mtendaji huyo raia wa Hispania anaamini Man City imefurahishwa na ratiba ya mashindano hayo na kwamba muundo wake ni mzuri na wenye umuhimu katika kuwaburudisha mashabiki wao wa soka.
Kikosi cha Pep Guardiola kilianza mashindano hayo kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wydad ya Morocco jumatano wiki hii katika mchezo uliochezwa huko Philadephia. Man City ndiye bingwa mtetezi ambaye alitwaa taji hilo miaka miwili iliyopita wakati mashindano hayo yalipohusisha timu 7.
Soriano alisema kuwa, “tuna furaha sana kushiriki mashindano haya, tunawapa nafasi nyingine kufurahia timu yao pamoja na kuitanagza kimataifa klabu yetu kupitia mchezo namba moja duniani. Lakini unaweza kushiriki mashindano ya ligi na mengine nyumbani ila linapofika mashindano kama haya moja kwa moja unajitangaza kimataifa. Kwenye kimataifa unapaswa kuonesha uwezo na ubora wako katika mashindano kama haya, ambayo tunaamini yanaonesha umuhimu wa mchezo wa soka duniani. Ni mkusanyiko mzuri ambao unafanya kazi vizuri sana na kwa hakika tunapaswa kujivunia mashindano haya,”
Man City waliwafunga Wydad kupitia magoli ya Jeremy Doku na Phil Foden huku mchezaji wake mpya Tijjan Reijnders na Rayan Chekri wakipewa nafasi kuonesha uwezo wao katika kandanda. Wachezaji hawa wawili ni wapya ambao wameingia kikosini humo na kuibua changamoto ya ushindani wa namba.
Yanga na Simba
Katika Ligi Kuu Tanzania mara nyingi vilabu vya Yanga na Simba vimekuwa vikitozwa faini kwa makosa mbalimbali siku ya mchezo. Mathalani makosa ya Yanga na Simba yanakuwa kutumia mlango usio sahihi, kufanya fujo, kuvunja kanuni za Ligi kuu na mengineyo mengi. Katika maizngira hayo Man City wamekuwa kama klabu ya Ligi Kuu Tanzania kwa kuvunja kanuni hivyo kuonesha kama vile hawana kiwango cha kusimamia taalamu yao ya soka.

