FISTON Mayele anakipiga katika klabu ya Pyramids ya Misri. Yeye ndiye mshambuliaji namba moja wa klabu hiyo. Nyota huyo ni raia wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na ambaye anatoka katika Ligi Kuu Tanzania. Mayele alikuwa mshambuliaji mkali katika kikosi cha Yanga na alitamba kwenye mashindano ya CAF huku akitupia mabao kadiri anavyojisikia. Baada ya kutamba Ligi Kuu Tanzania na mashindano ya CAF, vigogo wa klabu ya Pyramids walibisha hodi kwenye mlango wa klabu ya Yanga kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo.
Haikuwa muda mrefu Pyramids wakatangaza kufikia makubaliano ya kumsajili Fiston Mayele. Wakati Pymarids wakifanya hivyo, misimu kadha anyuma klabu ya Al Ahly ilimwaga fedha katika katika klabu ya Simba kumsajili kiungo mshambuliaji Louis Miquissone raia wa Msumbiji.
Al Ahly hawakutaka kurembesha maneno bali waliweka fedha ili kumsajili nyota huyo. Kana kwamba haitoshi Simba walijikuta wanamwagiwa fedha nyingine na klabu ya RS Berkane ambao walimsajili kiungo wao Cletous Chota Chama. Simba na Ligi Kuu walipoteza mastaa wawili wa Ligi Kuu kwenda kwa vigogo wa Kiarabu.

Tathmini ya TANZANIAPSORTS inaonesha kuwa kadiri vilabu hivyo vinavyopata mafanikio kwenye mashindano ya CAF, ndivyo vinavyorahisisha biashara ya kuuza wachezaji wake kwani vigogo wa soka wanashindwa kuvumilia na hivyo kumwaga noti za kutosha kusajili wachezaji wao.
Yanga walimuuza Tuisila Kisinda na mastaa wengine. Lakini sasa kwa mara nyingi Yanga wanalazimika kumwachia kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki kwenda Wydad Casablanca ya Morocco. Wydad Casablanca ndiyo timu ambayo amewahi kuichezea winga wa zamani wa Yanga, Simon Msuva.
Stephane Aziz Ki anaondoka klabu ya Yanga huku akiwakilisha nembo nyingine ya Ligi Kuu Tanzania. Katika usajili huo Yanga wananufaika kwa kujitangaza zaidi barani Afrika kwa vigogo wa soka. Lakini pia Ligi Kuu Tanzania inatangazika kwa kuibua vipaji ambavyo vinatamba katika soka.
Wydad Casablanca imemsajili pia Abdallah Selemani Mwalimu kutoka Fountain fc ya Tanzania ambapo naye anawakilisha nembo ya Ligi Kuu.
Aziz Ki amekuwa mchezaji kipenzi cha makocha wengi ambao wanatamani angekuwemo kwenye vikosi vyao. Kocha aliyeondoka Wydad Casablanca, Rhulani Mokwena alikuwa anamhitaji sana nyota huyo tangu alipokuwa Mamelodi Sundowns. Isivyo bahati Rhulani Mokwena anaondoka Wydad huku mchezaji kipenzi chake Stephane Aziz Ki anawasili klabu hapo.
Usajili huo unatoa taswira muhimu kwa maendeleo ya Ligi Kuu Tanzania. Kwamba wapo wachezaji wenye vipaji ambao wanaweza kupata nafasi katika klabu kama Wydad moja kwa moja bila kufanyiwa majaribio. Ingawaje Cletous Chama na Luois Miquissone hawakudumu katika klabu zao lakini waliwakilisha ishara nzuri ya Ligi Kuu Tanzania.
Hivi sasa wachezaji wanaonekana kwenye mashindano ya CAF, vipaji vyao vinatazamwa kupitia Ligi Kuu Tanzania pia.
Kwahiyo kila uchwao makocha na viongozi wanatupia macho Ligi Kuu kwa madhumuni ya kugundua wachezaji wenye viwango na wanaostahili kuchezea klabu zao. Kwa maana hiyo wapo wachezaji Ligi Kuu wana nafasi ya kupenya kwenye vikosi kama vya Mamelodi Sundown, Al Ahly, Pyramids, Raja Casablanca, Esperance na vigogo wengine.
Vilevile usajili wa Stephane Aziz unaonesha kuwa Ligi Kuu Tanzania ni daraja zuri kwa wachezaji wenye vipaji kuonekana kwenye mashindano na kusajiliwa. Kwamba wachezaji hao wanapoonesha vipaji vyao kupitia Ligi Kuu wanaweza kusajiliwa na timu kubwa zaidi. Hivyo basi klabu za Yanga, Simba, Azam Singida Black Stars zinatupiwa macho na vigogo mbalimbali na mawakala wa soka ili kuvuna vipaji vyao.
Katika hatua hiyo, wachezaji wa kigeni wanatamani kuja kucheza Ligi Kuu Tanzania wkaiwa na imani ni sehemu mwafaka ya kuanzia na kupenya kwenye vilabu vikubwa. Vilevile wanatazama Ligi Kuu Tanzania kama mtaji wao na njia ya kutengeneza majina yao kisoka.
Wakati Ligi kuu za nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi zikiwa hoi, Ligi Kuu Tanzania inazidi kuchanja mbuga na usajili wa Aziz Ki kwa Wydad ni ushahidi tosha. Huyu ni mchezaji ambaye ataendelea kuwakilisha vyema Ligi Kuu Tanzania, ambapo historia yake itabainisha bayana kuwa alisajiliwa toka Tanzania. Hapo ndipo wataalamu wa soka wanapotupia macho Ligi Kuu Tanzania na kusaka vipaji. Na ndipo tunapoona uwakilishi mwema wa Stephane Aziz Ki.
Tunakutakia kila la heri kwenye klabu yako mpya ya Wydad Casablanca ambako ataungana na nyota wa Kitanzania Seleman Mwalimu.


Comments
Loading…