HATIMAYE yule kocha mahiri aliyeng’arisha klabu ya Yanga amerejea tena katika Ligi Kuu Tanzania. Miguel Gamondi amejiunga na klabu ya Singida Black Stars ya mkoani Singida na kuwa kocha mkuu wa miamba hiyo ya kanda ya Kati. Singida Black Stars imemwajiri mwalimu huyo raia wa Argentina kuongoza benchi la ufundi kwa msimu ujao pamoja na mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika. Kwa mujibu wa taarifa ya klabu ya Singida Black Stars, Miguel Gamondi ameingia mkataba wa mwaka mmoja kukinoa kikosi hicho. Umahiri wa kocha huyo si wa kutiliwa shaka na dhahiri ujio huo utakuwa na majukumu makuu mawili. TANZANIASPORTS inachambua majukumu mawili makuu ya Miguel Gamondi katika ujio wake wa pili nchini Tanzania. Katika benchi la ufundi Miguel Gamondi atasaidiana na David Ouma na Moussa N’Daw.
Mafanikio Kombe la Shirikisho
Bila shaka yoyote uongozi wa klabu ya Singida Black Stars umenuia kuipaisha timu hiyo kwenye mashindano ya Kimataifa. Singida Black Stars wana kibarua katika mashindano ya Kombe la Shirikisho ambako wataungana na wakali wengine kama Azam F.C, huku Yanga na Simba zikiwa kwenye kinyang’anyiro cha mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Miguel Gamondi anjiungana timu ambayo imejionea mahasimu wake wa Ligi Kuu kama vile Yanga na Simba zikicheza fainali ya Kombe la Shirikisho na kulikosa kombe hilo katika dakika za majeruhi.
Yanga waliazna kuweka rekodi kwenye Kombe la Shirikisho, lakini msimu uliomalizika Simba walifikia rekodi hiyo na kuweka nyingine ya kulileta kombe linaloandaliwa na CAF hapa nchini. Singida Black Stars wana kila sababu ya kuamini watafanya vizuri mwenye mashindano ya Kimataifa kutokana na aina ya wachezaji walionao pamoja na ujio wa mwalimu huyo.
Huyu ni kocha ambaye aliongoza Yanga kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa ambako walitupwa nje na Mamelodi Sundowns ya Afrika kusini. Hii ni kazi ambayo Miguel anatakiwa kudhihirisha uwanjani kwa kuipaisha timu hiyo na kufuata nyayo za Yanga na Simba. Miaka ya nyuma timu za Tanzania kufika hatua ya fainali ilionekana kama jambo lisilowezekana, lakini hali ya mambo imebadilika, ambapo klabu hizo zimefanikiwa kutinga fainali.
Si hilo tu klabu za Tanzania zinasifika kwa kuwachachafya vigogo wa soka barani Afrika na hivyo kuangaliwa ka jicho la tatu. Vigogo vya soka barani Afrika vinatazama timu za Tanzania kama tishio lingine kwenye mbio zao za kunyakua mataji ya CAF. Miguel Gamondi atakuwa na kibarua cha kuhakikisha Singida Black Stars inacheza kwa ufanisi kwenye mashindano ya CAF pamoja na Ligi Kuu Tanzania.
Kisasi dhidi ya Yanga
Miguel Gamondi hakuondoka kwa namna nzuri katika klabu ya Yanga. Wakati akitangazwa kufukuzwa kazi klabuni hapo kulikuwa na masikitiko makubwa kwa sababu mashabiki walikuwa wakiamini kocha huyo ndiye mtu sahihi kuivusha timu hiyo. Yanga walimfuta kazi huku akitupiwa lawama nyingi kutokana na ushindi mwembamba ambao wanaupata katika mechi za Ligi Kuu.
Kuondoka kwake bila kupenda, ni dhahiri ujio huu wa pili atakuwa na kibarua cha kudhihirisha kuwa yeye ni mwalimu wa mchezo wa soka na fundi wa kazi hiyo. Kwa sababu ya kuajiriwa kufundisha tena Ligi Kuu, na kwa mazingira ya kawaida kabisa kocha huyu anakuja kuwaonyesha Yanga kwanini walikosea kumfukuza kazi. Silaha pekee ya kuwatambia Yanga itakuwa kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho pamoja Ligi Kuu Tanzania.
Gamondi atakuwa na kibarua cha kuwashawishi mashabiki wa SIngida Black Stars kuwa aliondoka Yanga kwa mizengwe na hivyo anao uwezo mkubwa wa kufundisha soka. Kisasi hiki ndicho kitaonyesha kuwa ana uwezo wa kuwazidi Yanga akiwa nje au alikuwa anabebwa na vipaji vya wachezaji wa klabu hiyo ambayo aimetwaan taji hilo.
Mashabiki wa Yanga mbele ya Gamondi
Hakuna ubishi kuwa mashabiki wa Yanga walikuwa wanampenda sana Miguel Gamondi kwa sababu aliwafanya wawe wanatabasamu na alifanya kazi yake vizuri ya kuwafunga Simba mara nne mfululizo. Katika uongozi wake Yanga waliwakuwa wanaishinda Simba kadiri wanavyojisikia.
Haikuwa rahisi kuifunga Yanga ya Gamondi. Lakini sasa mashabiki wa Yanga watakuwa na kazi kubwa kumzomea kocha waliyempenda ambaye atakuwa anachuana na timu yao ikiwezekana kuifunga na kuinyima pointi katika mechi watakzokutana. Mechi ya Singida Blacka Stars na Yanga haitakuwa kati ya timu hizo bali itakuwa pia Miguel Gamondi dhidi ya Yanga.
Na hasa mchuano utakuwa Gamondi dhidi ya uongozi wa Yanga. Wakati mashabiki wakitaka kuona kocha huyu hawafanyii mtimanyongo kwa kuwafunga lakini atakuwa na kazi ya kutetea kibarua chake hivyo atalazimika kuifunga Yanga na kuwahuzunisha mashabiki huku akiwa na nia ya kuhakikisha analinda kazi yake kwa kuipa mafanikio Singida Black Stars. Hii itakuwa miongoni mwa mechi kali msimu ujao. Mechi kati ya uongozi wa Yanga na Miguel Gamondi binafsi na kisha Singida Black Stars dhidi ya Yanga kwa wachezaji na washabiki.
Ligi Kuu katika vita ya ufundi
Ujio wa Miguel Gamondi pia unaonesha kuwa kutakuwa na vita vya ufundi kati ya timu za Ligi Kuu Tanzania. Simba wanaye kocha wao mahiri Faldu Davids, huku Azam FC wakimwajiri Florent Ibenge, na Yanga wapo kwenye msako wa kocha mpya. Hii ni kwamba vigogo wote waliofuzu mashindano ya Kimataifa watakuwa wanaongozwa na makocha wenye ujuzi wa hali ya juu na hivyo kuifanya Ligi Kuu Tanzania kuwa yeney ushindani wa hali ya juu.
Comments
Loading…