FLORENT IBENGE ndilo jina linalovuma kwa sasa katika mijadala mbalimbali ya soka kuanzia mtaani, kwenye vyumba vya habari kama vile redio, televisheni na vile vya mitandaoni. Vyombo vya habari vingi vimekuwa vikisifia kazi ya kocha huyo maarufu ambaye amewahi kuongoza timu ya Taifa ya DRC. Umahiri wa Florent Ibenge si wa kutiliwa shaka, na hatua ya kuifundisha timu ya Taifa ya Kongo maana yake ni uwezo wa juu kisoka. Kufundisha timu ya Taifa ya DRC ina maana kuwaongoza makumi ya wachezaji wa wanaosakata soka la kulipwa barani Ulaya na wengi wao katika vilabu vikubwa. Chama cha soka cha DRC kilionesha mfano mzuri wa kuwaamini makocha wazawa katika kuongoza timu za Taifa. Hata baada ya kuondoka na kwenda katika vilabu vya soka hasa Al Hilal ya Sudan, Florent Ibenge amekuwa kocha mwenye sifa nyingi na kuhitajika na vilabu vingi. Mara mbili au tatu amewahi kuhusishwa na kazi ya kuinoa Yanga na Simba kwa nyakati tofauti. Wakati huo Simba ilipokuwa chini ya Afisa Mtendaji Mkuu, Barbra Gonzalez aliwahi kukutana na kocha huyo kwenye moja ya shughuli za kisoka na kupiga naye picha, hatua ambayo wengi walitafsiri kama jaribio la kushawishiw akuja kuifundisha timu ya Simba. Hali kadhalika Yanga nao wamewahi kuhusishwa na kumnyakua kocha huyo huku uongozi, lakini hakukuwa na taarifa rasmi ya kukanusha au kukubaliana na tetesi hizo.
Uchunguzi wa TANZANIASPORTS imebaini kuwa vilabu vingi barani Afrika vimekuwa vikishindwa kumwajiri kocha huyo kutokana na gharama kubwa za mishahara na marupurupu. Inaelezwa kuwa Florent Ibenge ni kocha ghali sana, lakini ni miongoni mwa bidhaa nzuri katika benchi la timu.
Sasa Florent Ibenge ni kocha aliyetangazwa kuajiriwa na mabwanyenye wa Chamanzi, Azam FC. Ibenge atakuwa kocha mkuu wa Azam akiandaa timu hiyo kwneye mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho Afrika. Je Florent Ibenge ni kocha wa namna gani? Hilo ndilo swali ambao wanajiulzia wengi na namna gani anaweza kuinua hali ya mafanikio ya klabu ya Azam. Ikumbukwe Azam imepitia makocha wengi akiwemo mwenye mafanikio Stewart Hall ambaye aliifanya Azam kuwa timu yenye nguvu na imara zaidi.
Mbinu za ‘Kimourinho’
Hakuna siri moja ya mkakati wa Florent Ibenge katika timu yake ni kucheza vile anavyotaka dhidi ya mpinzani. Kwa muda waliofundisha timu ya Taifa hakuonekana kuifanya icheze kama ilivyokuwa Al Hilal. Kwa DRC alikuwa na mastaa wengi wanaoelewa na wenye ujuzi wa Kimataifa hivyo kazi yake ilikuwa rahisi mno. Katika ngazi ya klabu ndiko Ibenge alionesha makucha ya kucheza mbinu za Jose Mourinho. Mourinho anafahamika kwa mifumo migumu ya timu zake, na mara nyingi ni ile ya kujihami. Kwahiyo Ibenge ni kocha anayetumia dakika 45 za mchezo kujihami kisha kubadilika katika kipindi cha pili kuwapunguzia majukumu ya kukimbia umbali urefu wachezaji wake. Al Hilal ilikuwa timu ambayo inacheza kwa mbinu za kujahami na kushambulia kwa kushtukiza hali ambayo ilisababisha wapinzani wawe wanafungwa katika matukio machache yanayotengenezwa na Al Hilal.
Ibenge sio kama Gamondi
Alipokuwa kikosi cha Yanga, Miguel Gamondi alipendelea kuwaondoa kwenye mfumo wake mawinga asilia. Ni sababu hii Dennis Nkane alikuwa na wakati mgumu sana kupata namba katika kikosi cha Yanga. Kwa mfano Pacome Zouzoua na Max Nzengeli wangeweza kupangwa kama viungo wa pembeni na kuwoandoa kwenye mfumo mawinga asilia. Katika mfumo huo timu hucheza 3-1-4-2, ambapo mabeki watatu, kiungo mkabaji mmoja, viungo wanne na washambuliaji wawili.
Katika safu ya ushambuliaji ndiko anaweza kumweka kiungo namba kumi ambaye atamsaidia mshambuliaji kiongozi. Hali kadhalika katika mfumo huo wachezaji wanne wa kiungo wanakuwa si mawinga asilia. Katika mfumo huo unaweza kubadili kwa kupanga 3-5-2 ambapo katikati ya dimba ndiko kunakuwa na vita kali kupenya huku msingi ukiw ani kushambulia kwa kushtukiza. Katika mfumo huo wachezaji wanakuwa wanakimbia umbali mrefu huku mpira ukiwa ni ule wa pasi ndefu. Kwa mfumo huu unaweza kupiga pasi tatu tu timu inakuwa langoni mwa adui. Hata hivyo kocha anaweza kubadilika na kuwa na mfumo tofauti kulingana na aina ya wachezaji alionao kikosini. Kwa mfano Azam FC ina wachezaji wenye kucheza soka la pasi fupi na wanafurahia mfumo wa kutandaza soka la burudani. Hii ina maana kocha mpya atakuwa na jukumu la kukubaliana na aina ya uchezaji wa wachezaji wake kisha kuingiza mbinu au wachezaji wakubali kubadilika na kuingiza mbinu mpya.
Mabosi wa Azam wachagua kipi?
Ifahamike Ibenge ni kocha wa Kimataifa, labda tuseme ni wa daraja la juu katika mchezo wa soka hapa Afrika mashariki. Kwahiyo waajiri wanapompa kazi ni dhahiri wanafahami mifumo na mbinu zake anazotumia kwenye timu. Ni lazima tukubaliane kuwa upo wakati kocha huyo huchezesha timu yake kucheza michezo michafu yaani mbinu za kila aina ili tu kupata ushindi. Hii ni tabia ya kocha Jose Mourinho ambaye kwake ushindi lilikuwa jambo muhimu kuliko kingine, haijalishi timu inacheza vizuri au vibaya. Haijalishi mbinu zimekuwa sahihi au sio sahihi ilmradi timu imeibuka na ushindi.
Ibenge ataichoka Azam au Azam watamchoka Ibenge?
Makocha wengi wamepita Azam bila kunyakua taji la Ligi Kuuu. Ni muda mrefu tangu Azam ilipotwaa taji la Ligi Kuu Tanzania bara, kwhaiyo ni klabu yenye njaa ya mafanikio. Hata hivyo makocha waliopewa mikataba ya muda mfupi au mrefu wamekuwa na mafanikio madogo mno kulinganisha na uwekezaji uliofanywa na mmiliki wa klabu hiyo. Wakati furaha ikiwa ni kubwa kumpata kocha huyo, ni muhimu kuchambua kuwa kwa kutumia mifumo yake ya ufundishaji ni nani atamchoka mwenzake, Azam u Ibenge? Pia kwa kutumia hadhi yake na sifa ya kuwa kocha mkubwa atamudu kudumu Azam au Azam itashindwa kummudu kocha huyo? Haya na mengine ndiyo mambo ambayo yanatakiwa kuchambuliwa kwa kina wakati Azam itakapoanza msimu mpya na ikiwa kwenye mashindano ya CAF.
Comments
Loading…